Makene Ngoroma
NI kijana, kijana mpole anaeonekana kutokuwa na makuu,pamoja na kuwa na fikra na akili komavu, lakini hana mbwembwe wala tashtiti.
Makene Ngoroma anashikilia wadhifa wa Mhifadhi wa Wanyamapori tarafa ya Mikumi wilayani Kilosa, mkoani Morogoro.
Ukimuona kwa mara ya kwanza akiwa amevaa mavazi ya kawaida kabisa unaweza kusema huyu mwamba hana lolote!
Anapatikanaje?
Itakuchukua wastani wa saa moja kutoka Morogoro mjini hadi Mikumi, wilayani Kilosa na utalazimika kusafiri umbali wa maili 67 kutoka Morogoro mjini ili kumfikia Ngoroma.
Anapatikana Mikumi mjini na ukifika eneo hilo, hutapata tabu kumpata kijana huyu ambaye mwaka 2021 aliingia kwenye orodha ya viongozi vijana 100 bora Afrika wanaojihusisha namasuala ya uhifadhi.
Ngoroma anajulikana kama Mmarekani mweusi, jina hili ni kwa mujibu wa baadhi ya vijana waliozungumza na Afrinews Swahili.
Wanamuita hivyo kutokana na lafudhi yake, Ngoroma anaongea lugha ya Kiswahili vizuri, lakini lafudhi anayoitumia ni kama ya mmarekani aliyelowea Mikumi.
Ukimsikia kwa mara ya kwanza bila kumuona, unaweza kusema kuna mmarekani kwenye eneo hilo na ukipata nafasi ya kumuona na kumsikia akiongea unaweza kusema anaigiza, ila hivyo ndivyo alivyo.
Ngoroma (kulia) akiwa na Jimmy Kiango (mwandishi wa makala haya)
“Hapana kaka, mimi sijaishi Marekani (kicheko) hao vijana wanaoniita hivyo siwajui na sijawahi kusikia wakiniita hivyo,” anasema Ngoroma.
Pamoja na lafudhi yake hiyo,lakini ukipata dakika moja tu ya kuzungumza nae, hatuaacha kutafuta kiambaza ama kimbweta ili uegame kisha umpe muda zaidi wa kumsikiliza.
Anajibu maswali yote yanayohusu uhifadhi wa wanyama kwa upole bila kigugumizi, majibu yake yamejaa maarifa na yanayoshawishi utake kujua zaidi kuhusu uhifadhi, Ngoroma ni darasa la uhifadhi wa wanyama linalotembea.
Ana akili na maarifa mengi kwenye eneo la uhifadhi wa wanyama na bila shaka ukweli huo ndio ulimfanya kukabidhiwa jukumu la kuwalinda kazi iliyompatia na tuzo kadhaa.
Ngoroma anawahifadhi wanyama kivitendo bila kujali ni aina gani ya wanyama, lakini pia anashirki kusafisha eneo la hifadhi, kifupi ana masimulizi mengi yanayohusu uhifadhi.
Kabla na hata baada ya kuwa mtumishi wa serikali kwa mikono yake ameweza kuwaokoa wanyama mbalimbali wakiwemo Mamba, Kaka kuona na Tembo.
AOKOA KAKAKUONA 12
“Kwa mikono yangu na kwa nyakati tofauti nimeokoa Kakakuona 12 ambao wanatoka hifadhini na kuingia kwenye maeneo yaliyozunguka hifadhi.
“Kila ninapopata taarifa za wanyama kutoka hifadhini, huwa sichelewi kufika eneo la tukio, nikifika ninachokifanya ni kuhakikisha wanarudi kwenye makazi yao rasmi.”
Mara nyingi Ngoroma amewakamata Kakakuona wanaokimbilia Kijiji cha Vikweme ambacho kinapakana na Hifadhi ya Taifa Mikumi.
ASAFIRI NA MAMBA
Katika hali isiyotarajiwa Ngoroma akiwa katika heka heka zake za kuokoa wanyama, aliweza kusafiri na mamba mkubwa kwenye pikipiki bila hofu.
ILIKUWAJE?
Alipata taarifa kuwa mamba amevamia kwenye kijiji cha Vikweme, haraka akatafuta namna ya kufika huko na njia pekee na rahisi ilikuwa ni pikipiki (bodaboda) pasi kuchelewa akapanda usafiri huo.
Baada ya kufika aliruhusu kijana mwenye utaalamu wa kutega mamba kutoka rufiji kumtega kwa waya.
Nia ya wananchi ilikuwa ni kutaka kumuua lakini dhamira yake kuu ilikuwa ni kuhakikisha anamuokoa Mamba huyo kwani mara zote furaha yake ni kuona mnyama hauwawi, lakini pia haleti madhara kwa binadamu na mali zake.
Mara baada ya kufika eneo la tukio, alimkuta mamba akitamba na kutambuka kwenye maeneo hayo, kwa utaalamu alionao na kwa kushirikiana na mtalamu wa kutega Mamba, alifanikiwa kumuokoa na hasira za wanakijiji kisha akamfunga kwenye pikipiki ambayo yeye alikuwa ni abiria.
"Dereva wa pikipiki pamoja na kuwa mbele ya Ngoroma lakini hakuwa na amani, nilimwambia awe na amani kwa sababu isingekuwa rahisi kutokea madhara ya aina yoyote ile.”
MAUAJI YA TEMBO
Ngoroma anasema kwa sasa hali ni shwari, serikali imefanya kazi kubwa ya kukabiliana na majingili na kupambana na ujangili.
Anasema awali wananchi wengi wa maeneo yanayozunguka hifadhi walikuwa wakiwaua sana tembo kwa kuwawekea sumu ama kuwapiga mikuki, hali sasa iko tofauti kabisa.
Ngoroma anasema vijiji vya Ihombwe, Mhenda na Kitundueta na vitongoji vya Kikwalaza, Tambuka Reli na Magoma vilikuwa ni tishio kwa ujangili, lakini sasa ndio vimekuwa mstari wa mbele kulinda wanyama na baadhi ya vijana waliokuwa majangili ndio wamekuwa waongoza watalii wanaotumia baiskeli.
“Mimi nilianza kazi hapa 2011, hali haikuwa nzuri, ujangili ulikuwa ni mkubwa sana, nikajaribu kufikiria cha kufanya ili kuondokana na changamoto hii.
“Njia pekee niliyoiona ilikuwa ni kuwabadilisha fikra vijana, ili kuwatoa kwenye kushiriki vitendo vya kijangili na kuwafanya kuwa wahifadhi.
“Unajua mara zote majangili hushirikiana na wenyeji, hawawezi kutoka huko wanakotoka na kufanya ujangili, bila kujua njia za panya za kuingia na kutoka hifadhini.
KIUNGO CHA VIJANA NA HIFADHI
“Mwaka 2015 nikaanza kushirikiana na vijana kwa kuunda vikundi kazi, tunapaswa kuelewa jambo la msingi, mtu hawezi kuona faida ya kulinda kitu ambacho hakimsaidii.
“Huko nyuma kulikuwa na mgogoro mkubwa kati ya wanyama na wananchi, na tembo ndio alikuwa mwathirika mkuu.
“Wananchi walikuwa wanalalamikia wanyama kuharibu mali zao.
“Kimsingi hakukuwa na urafiki baina yao na hawakuona faida za kuwalinda maana walikuwa hawafaidiki nao.
“Nikaamua kutengeneza urafiki kati ya wananchi na hifadhi na hilo limesaidia kuleta urafiki kati ya wananchi na wa vijiji vinavyozunguka hifadhi na wanyama pia.
“Nilianzisha hamasa ya kuwatoa vijana kwenye ujangili na kuwaingiza kwenye uhifdhi, nilianzisha kikundi cha Mikumi Environment Conservation & Community Development (MECODE).
“Kikundi hiki nilikianzisha pamoja na kuhifadhi mazingira, lakini pia nilitaka kiwe na tija kwa jamii ya mikumi.
“Sasa kingepataje maendeleo wakati hatuna mfadhili wala mdhamini?
“Nilichokifanya ni kuanza kutafuta kazi za kufanya usafi hifadhini, kweli nikafanikiwa, MECODE ikapewa tenda ya kusafisha kilomita 50 za barabara inayopita hifadhini.
“Haikuishia hapo, wakaja wakapata tenday a kusafisha mji wa Mikumi, hatua hiyo ikasaidia sana kuwaaminisha wakazi wanaoizunguka hifadhi kuamini kuwa jukumu la kuilinda hifadhi ni lao pia maana kuna kitu wanapata.
“Baada ya kuona MECODE inafanya vizuri, nikaona haja ya kuanzisha kikundi kingine, mwaka 2017 nikashiriki kuasisi kikundi cha Mikumi Eco and Cultural Tourism Enterprise.”
Kikundi hiki jukumu lake ni kufanya utalii wa utamaduni, ambapo wanatengeneza bidhaa mbalimbali za kitamaduni na kuwauzia watalii na fedha inayopatikana ni ya kwao.
Kikundi hicho kinaundwa na zaidi ya vijana 25 kutoka vitongoji vya Kwalaza, Magoma,Tambuka Reli na Mikumi, ambao wengi wao walikuwa mchana wakiendesha bodaboda na usiku kujiingiza kwenye ujangili.
Ngoroma anasema haikuwa rahisi kuwapata vijana hao, lakini walipambana na walianza kwa kuwafuata kwenye maeneo yao kama vile kwenye vijiwe vya bodaboda n ahata kwenye viwanja vya michezo na kuwaelimisha juu ya uhifadhi na faida zake.
Anasema baada ya kuwa na mwamko zaidi akaamua kuvigawanya baadhi ya vikundi na moja kati ya alivyovigawa ni kikundi cha Mikumi Eco, ambapo, ambapo alizalisha kikundi cha Masai Boma Culture Tours.
Kikundi hiki kinahusisha wamasai, ambao kazi yao ni kufanya shughuli za utamaduni ambazo zinawavutia watalii pia.
Neema Mngarambe akiwa na Jimmy Kiango, wakiwa kwenye mabaki ya jengo Hoteli ya kwanza iliyojengwa kwa Saruji, Mikumi.
Ngoroma anasema mbali ya wamasai, lakini pia makabila ya Wavidunda, Wasagara, Wakaguru na Parakuyo Masai wanaopatikana Mikumi, wote wanashiriki kwenye utalii wa asili, ambao unajumuisha mila na desturi za makabila yao.
“Kikubwa kinachofanywa na vikundi hivi vinavyojihusisha na utalii wa kitamaduni ni kutengeneza vifaa vya kitamaduni, vyakula vya kitamaduni, ngoma na kuuza nguo za kitamaduni.”
Anasema kuna vivutio vya asili kama vile mti wa asili unaofanana na mnazi ambao wenyewe wanauita Mkoche, ambao ndio uliobeba jina la asili la Mikumi, ni kuwa miti hiyo ilikuwa mingi kwenye eneo moja, wenyeji wakawa wanaliita Mikoche omikumi.
Katika eneo hilo mtalii anapata fursa ya kuona sehemu za matambiko na mti mkubwa wa kutisha unaojulikana kama Mkuyu maarufu kama Mdele ambao uko katika kitongoji cha Kotam ambako kuna historia ya watu wa kale walikokuwa wanafanya matambiko yao na kutoa sadaka, kukeketa wanawake na kuwapa mafunzo n ani eneo linaloaminika kuwa maalum kwa uchawi.
Pia kuna utalii wa kutazama matofari ya udongo, eneo la Lukande ambalo lilitumika kuzikia na hoteli ya kwanza kujengwa kwa tofari za saruji Kilosa mjini, inayojulikana kama Green Star Hotel, ambayo kwa sasa imegeuzwa kuwa ofisi ya Mtendaji wa Kata Mikumi.
Aidha vikundi hivyo vya utalii wa kitamaduni, vinawapeleka watalii kuangalia kikundi cha ngoma kikongwe kuliko vyote Mikumi cha Kisamasi Vitua ngoma , ambacho kilianzishwa mwaka 1974 na kwa muda mrefu kimekuwa kikiongozwa na kabembele Kabembele kikiwa na uwezo wa kupiga ngoma za makabila tisa ya Tanzania.
KAULI ZA VIJANA JUU YA UJANGILI
Omari Said (sio jina lake halisi) anasema yeye miaka ya nyuma alikuwa ni jangili na alishiriki kikamilifu kuua tembo, alifanya hivyo kwa sababu hakuwa na njia ya kuingiza kipato na aliona ujangili unampatia fedha za kuendesha maisha yake.
“Niwe mkweli si jambo rahisi kwa majangili kutoka mbali ya maeneo yaliyozunguka hifadhi, maana kama huijui hifadhi huwezi kutoka salama, sasa mimi nilikuwa najua maeneo walipo Simba, Chui, Tembo na wanyama wengine wakali, basi kilichokuwa muhimu kwangu ni uhakika wa soko tu.
“Nikijua nina uhakika wa kuuza meno ya Tembo basi najiandaa na kuingia msituni ili kufanikisha kazi yangu, sikuwa na muda, mimi nilikuwa na uwezo wa kuingia hifadhini muda wowote ule.
“Unajua hifadhi ni kubwa, sio rahisi kwa hawa jamaa kutembelea maeneo yote na uzuri hata wao wenyewe wengi ni waoga, kwa hiyo mimi na wenzangu kwakuwa tulikuwa na uzoefu basi wala hatukuwa tunasumbuka.”
Said alisema kwa sasa yeye na wenzake wengi wameacha na wameacha kwa sababu wanauhakika wa kipato kutoka kwenye vikundi vyao.
“Kaka mtu anafanya uhalifu kwa sababu ya kusaka kipato, unadhani akiwa na uhakika wa kipato halali atakuwa tayari kujihatarisha maisha yake?
“Ujangili ni hatari maana unawindwa na serikali na unawindwa na wanyama wakali, unadhani wakikuwahi wanyama watakuacha salama!
“Jambo la kushukuru sasa nimeacha na naingiza kipato changu halali kwa kutumia hifadhi ambayo zamani ilikuwa naingia kwa siri, lakini sasa naingia kwa uwazi kuongoza watalii ama kufanya usafi, niko huru kabisa na naipongeza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kusaidia vikundi hivi ambavyo hakuna ubishi Makene ndie ameshiriki kuviasisi.”
Kwa upande wake Nuhu Ole Mereni ambae ndie mwenyekiti wa kikundi cha Masai Boma, alisema kwa sasa wao ndio wamekuwa mabalozi wazuri wa masuala ya uhifadhi wa wanyama.
Alisema utalii wa kitamaduni unawaingizia hela nyingi, lakini pia TANAPA inawasaidia kwenye masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwapatia kiasi cha shilingi milioni 6.6 kama pesa mbegu za kikundi chao.
“Pamoja na kupewa pesa mbegu, lakini pia tumeomba pesa za mradi na tuna uwezekano wa kupata shilingi milioni 29 kutoka TANAPA.”
Kwa upande wake Neema Kizinja ambaye ni mratibu wa vikundi Mikumi, alisema wanashirikiana na TANAPA katika kusaidia vikundi hivyo.
Alisema mradi wa Regrow umekuwa na msaada mkubwa kwa vikundi kwani kwa mwaka huu umetoa kiasi cha shilingi milioni 191 kwa miradi 300.
Ngoroma pia ni mtaalamu wa kutengeneza mabomu ya pilipili yanayotumika kufukuza tembo
KAULI YA TANAPA
Afisa Mhifadhi mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Herman Mtei alikiri uwapo wa vikundi hivyo kuwa na faida kubwa kwa uhifadhi wa wanyama kwenye hifadhi hiyo.
Mhifadhi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Herman Mtei.
Mtei alisema TANAPA imeiona haja ya kushirikiana na vikundi hivyo ili kuwapa nafasi ya kufurahia kuwa sehemu ya hifadhi na fedha wanazozitua zimekuwa ni kichocheo kikubwa cha kupambana na ujangili.
Makala haya yameandaliwa kwa hisani ya Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tannzania (JET) kwa udhamini wa Internews.
0 Comments