Ticker

7/recent/ticker-posts

HAYATI SOKOINE MANENO KIDOGO,VITENDO VINGI

Picha hii ilipigwa Mtaa wa Jamhuri miaka kadhaa iliyopita kwa fundi viatu huyo kwenye sehemu yake ya kazi aliweka picha ya ‘ Shujaa’ wake. 

Bongo Hapo Zamani: 

Siku Ile Alipokufa Sokoine...

Ni tarehe kama ya leo. (12-4-2023)

Tuliokuwepo bado tunakumbuka tulikuwa wapi  na tulikuwa tunafanya nini. 

Ni siku ile habari zilipotufikia kwa mara ya kwanza; kwamba Waziri wetu Mkuu, Edward Moringe Sokoine ameifariki dunia.  

Nakumbuka siku ile ya April 12, miaka 39 iliyopita,  nilikuwa nikitembea kwa miguu nikitoka shuleni  Tambaza kurudi nyumbani. Tuliishi Kinondoni ‘ B’ eneo la Biafra.

Nilipofika Kinondoni ‘A’ eneo la Msikiti wa Mtambani, basi,  nikasikia wimbo wa taifa ukipigwa. Ilikuwa majira ya saa kumi. 

Nikasogea karibu  na duka ambalo wimbo ule ulisikika. Raia wengine walijikongoja jirani na duka lile. 

Kila mmoja alijua, kuwa kuna jambo kubwa limetokea. Shughuli zote za kuuza na kununua bidhaa zilisimama pale dukani. Ni wakati kama huo, unadhani wimbo wa taifa ni mrefu sana kuusubiri umalizike. 

Naam, unataka uishe uisikie sauti inayokuja.  Sauti itakayotutangazia Watanzania jambo kubwa. Yaweza kuwa msiba wa kiongozi mkuu wa nchi  au hata kuwa nchi yetu imevamiwa, au Serikali imepinduliwa.

Enzi hizo wimbo wa taifa ulisikika asubuhi saa kumi na mbili wakati redio ikifungua matangazo, na saa nne usiku, mwisho wa matangazo. Aidha, ni kwenye mechi ya mpira timu yetu ikipambana kimataifa.

Ukisikika mchana wa jua kali au wakati mwingine wowote kupitia redio, basi, ujue kuna jambo la kitaifa. Jambo la dharura. Hapo Wimbo wa Taifa huwa mithili ya ‘ Kengele ya Hatari’.

Wimbo ule wa Taifa ukaisha. Kila mmoja wetu pale dukani alivuta pumzi kuusubiri ujumbe. Ikasikika sauti ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Naikumbuka kuisikia kama vile ni jana tu. Ilikuwa ya mtu anayeongea pole pole na aliyejawa na huzuni....

Ndugu zangu Watanzania, 

Leo majira ya saa saba, tumempoteza Waziri wetu Mkuu, Ndugu Edward Moringe Sokoine. Ni kwa ajali ya gari eneo la Dakawa alipokuwa njiani  akitokea Dodoma...

Mwalimu aliendelea kuzungumza, lakini, ujumbe ulishatuingia kwenye vichwa vyetu.

Tuliokuwepo pale nje ya duka ikawa kama tumenyeshewa na mvua. Haikuwa taarifa iliyozidi dakika tano.  Ulisikika tu wimbo wa Taifa ukipigwa tena kusindikiza taarifa ile ya huzuni.

Jamhuri na watu wake ikawa imepigwa na butwaa. Si butwaa tu, ni kama vile Jamhuri ilikuwa imegubikwa na wimbi kubwa la mvua lililofanya kiza ardhini. Hali ile nilikuwa sijapata kuishuhudia tangu kuzaliwa.

Mapema asubuhi siku ya pili yake tulifika shuleni pale Tambaza, lakini, ajabu ya siku ile, kwa walimu na wanafunzi, ni kama wote tulikuwa hatujui siku ile tunaipitishaje katikati ya huzuni kuu ya kitaifa.  

Ndugu Edward Moringe Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa Watu na Kiongozi wa Kanuni. Aliishi kama alivyohubiri. Tuliokuwa shuleni wakati huo, kuna tuliotamani tuje kuwa kama Sokoine.

Naam, yaliyofuatia yanabaki kuwa ni historia, na hata leo, baada ya miaka 39 ya kifo chake, Sokoine bado anaishi kwenye mioyo ya Watanzania.

Sokoine amekuwa ‘ Kipimo’ kisicho rasmi cha viwango vya Mawaziri Wakuu waliofuatia baada yake. Kila ajaye, kuna walioulizana wakinong’ona;

" Hivi nani anafanana fanana na Sokoine?”

Atakumbukwa Daima.

Ni shujaa wetu sote. Kiongozi wetu mpendwa, Edward Moringe Sokoine.

Mwandishi wa makala haya ni Maggid Mjengwa.

Post a Comment

0 Comments