Dk. Egina Makwabe
Hii hapa chini ni sehemu ndogo ya mahojiano mazito na Mwenyekiti wa Chama cha wamiliki wa Hospitali binafsi nchini, mahojiano kamili yatapatikana kwenye jarida la TZ&BEYOND….
TZ&BEYOND: APHFTA imeanza lini na ina wanachama wangapi hadi sasa?
DKT. MAKWABE: APHFTA ilianza mwaka 1995/96 miaka michache baada ya serikali kuridhia sekta binafsi kushiriki kwenye kutoa huduma kwenye eneo la afya.
Mpaka sasa hivi tuna wanachama zaidi ya 20,000 hapa ukijumulisha hospitali 1600, Zahanati na vituo vya afya nchi nzima zaidi ya 1000, maabara zinazojisimamia zaidi ya 1000, maduka ya dawa zaidi ya 1000 na maduka ya dawa baridi zaidi ya 18,000 nchi nzima.
Mmiliki wa Hospitali ya TMJ, Dkt. Tyaval Mohamed Jafferji (kulia) akizungumza na mwandishi wa makala haya Jimmy Kiango
TZ&BEYOND: Unaweza kuzitaja kwa uchache hospitali ambazo zinaunda APHFTA?
DKT. MAKWABE: Baadhi ya wanachama wetu ni TMJ, Hindumandal, Aghakhan, Seife, Regency, Rabininsia, Kitengule, Kairuki na hospitali nyengine nyingi zilizopo kwenye mikoa yote nchini na mimi ndie Mwenyekiti wao, wameniamini niwaongoze.
TZ&BEYOND: Majukumu ya APHFTA ni yapi?
DKT. MAKWABE: Majukumu yetu ni kuunganisha nguvu ya pamoja kwa Hospitali zote binafsi nchini, tunatambua kuwa Wizara ya Afya ndio mwamvuli na mlezi wa sekta nzima ya afya kwa upande wa serikali, lakini sisi tumeiona haja ya kuwa na kitu kinachotuunganisha ili linapokuja suala la kusema, wote tuwe na kauli moja, lakini pia tumeiona haja ya kuwa pamoja ili tutoe huduma bora za afya kwa watanzania wote.
Kwa sasa ndio tunachukua nafasi kubwa ya kutoa huduma ya afya kwa watu wengi nchini, ambapo kwa Dar es Salaam pekee, yenye watu zaidi ya milioni tano, tunahudumia asilimia 80% ya watu hao na asilimia 20 iliyobaki inahudumiwa na Serikali.
TZ&BEYOND: APHFTA inakabiliwa na changamoto gani?
DK.MAKWABE: Changamoto kubwa ni kupungua kwa mapato, hii imesababishwa na vipindi tunavyopitia hasa Covid19 na Vita vya Ukraine na Urusi.
Mambo haya yametuteteresha sana, kumbuka tulilazimika kushiriki kikamilifu kwenye mapambano ya Covid 19, tumetumia rasilimali zetu nyingi katika kuwasaidia watanzania.
Dkt. Makwabe (kushoto) akiwa na Wahariri wa TZ&BEYOND, Sidi Mgumia na Jimmy Kiango (kulia)
Kwa kiwango kikubwa kutetereka kwa uchumi wetu kumesababisha kushindwa kununua vifaa vikubwa zaidi vya kitabibu , kuajiri wataalamu zaidi, kutoa mafunzo kwa wataalamu tulio nao na kushindwa kuboresha miundo mbinu mipya.
Lakini pia tunakabiliwa na kodi, kama unavyofahamu sisi ni watoa huduma ambazo kwa muda mrefu tumekuwa tukihudumia watu wengi, tunalipa VAT na kodi nyingine, tunalipa tozo mbalimbali kama za OSHA na Fire, kwakweli tozo ni nyingi, ukiziorodhesha zote kodi na tozo kwa ujumla zinafika asilimia 52. Hiki ni kikwazo kwetu.
0 Comments