Waziri Mkuu Kassim Majaliwa |
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema suala uhifadhi wa mazingira ni muhimu kwa nchi na akamtaka kila Mtanzania azingatie uhifadhi wa mazingira.
Ametoa kauli hiyo Machi 16, 2023 wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa sekta ya maji na mamia ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Mradi wa Ujenzi wa Mfumo wa Usambazaji Maji kati ya Makongo na Mji wa Bagamoyo uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Tegeta A, jijini Dar es Salaam. Pia alizindua Wiki ya Maji kwa mwaka 2023.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali za kuboresha miundombinu ya ukusanyaji na usambazaji wa maji, ni jukumu la kila Mtanzania kutunza vyanzo vya maji. “Tuna jukumu kubwa nalo ni la kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji; na eneo hili tuna mgogoro mkubwa kwani vyanzo vyetu vya maji vinaharibiwa, ni wajibu wetu kutunza vyanzo hivi.”
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe |
“Suala la uhifadhi ni muhimu sana. DAWASA isimamie suala hili kwa karibu na kutoa taarifa mapema. Wakurugenzi wa Mabonde ya Maji nchini kama vile Ruvuma, Rufiji, Malagarasi na mabonde mengine yote hakikisheni mnafanya ukaguzi wa mara kwa mara ili vyanzo hivi visiharibiwe. Wananchi tulinde vyanzo hivi na mtu akionekana anaharibu, kama ni kisima au chanzo kingine, tuchukue hatua, tusisite kwa sababu huo ni uhujumu.”
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira iliyokuwepo, Waziri wa Maji. Jumaa Aweso alimwagiza Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Bw. Kiula Kingu ahakikishe wananchi wote walioomba maji wafungiwe mita ndani ya siku saba kama Mkataba wa Huduma ya Wateja unavyosema.
Akielezea utekelezaji wa miradi ya maji kwenye wizara yake, Waziri Aweso alisema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwenye wizara hiyo ambazo ni mahsusi kwa utekelezaji wa miradi ya maji. “Mheshimiwa Rais kwa sasa ametoa asilimia 90 ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maji, wakati awali utekelezaji ulikuwa ni kati ya asilimia 50 hadi 60 tu,” alisema.
Alisema ili kukabiliana na uhaba wa maji, Wizara hiyo inapanga kujenga mabwawa kwenye maeneo mbalimbali ili kutengeneza akiba ya maji. Akitoa mfano, alisema Bwawa la Kidunda limeshapatiwa malipo ya awali ya sh. bilioni 49.
Akitoa maelezo kuhusu mradi huo katika eneo la Mivumoni, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Bw. Kiula Kingu alisema ujenzi wa mfumo wa usambazaji maji kutoka matenki ya DAWASA yaliyopo Chuo Kikuu cha Ardhi hadi Bagamoyo ni mradi wa kimkakati uliotekelezwa na Serikali kupitia DAWASA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia.
“Mradi huu ambao umegharimu sh. bilioni 71.9 na kukamilika kwa asilimia 100, umelenga kuunganisha wateja wapya 35,000 na kwamba hadi sasa wateja 20,618 wamenufaika.
Alisema mradi huo umehusisha ujenzi wa matenki matatu makubwa yenye ujazo wa lita milioni tano kila moja, yaliyojengwa Vikawe, Mbweni na Tegeta A, ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma maji vilivyojengwa eneo la Vikawe na Mbweni pamoja na ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji ndani ya eneo lote la mradi,” alisema.
Kwa upande wa Vikawe, alizitaja kata zitakazonufaika na mradi huo kuwa ni Mapinga, kwa Matumbi na Vikawe bondeni. Kwa Mabwepande, ni kata za Bunju B, Mabwepande na Mbopo ilhali kata ya Salasala, mradi utahudumia Salasala, Kinzudi, Mbezi, Goba na Kilongawima.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bibi Preeti Arora alisema mradi huo ulilenga kuongeza upatikanaji wa maji na kwamba ameridhishwa kuona fedha zilizotolewa zinasimamiwa kwa karibu na Serikali ili kutimiza lengo lililokusudiwa.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji yameanza Machi 16 na yatahitimishwa Machi 22, mwaka huu yakiwa na kaulimbiu isemayo: “Kuongeza Kasi ya Mabadiliko katika Sekta ya Maji kwa Maendeleo endelevu ya
0 Comments