ILI kuhakikisha timu ya taifa la Tanzania, Taifa Stars inafuzu kucheza fainali za AFCON, Rais wa nchi hiyo Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza kutoa kiasi cha shilingi milioni 10 taslimu kwa kila goli litakalofungwa kwenye mchezo wao wa marudiano dhidi ya timu ya taifa ya Uganda, utakaochezwa Machi 28,mwaka huu kwenye uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Mbali na kutoa fedha kwa ajili ya goli, lakini pia Rais Dkt. Samia amenunua tiketi 7000 ili zigawiwe kwa watanzania watakaokwenda uwanjani kuishangilia timu yao.
Hatua hiyo ya Rais Dkt. Samia inaongeza hamasa zaidi kwa wachezaji wa Taifa Stars ambao jana waliwapa furaha Watanzania baada ya kuifunga Uganda kwenye uwanja wao wa 'nyumbani' nchini Misri.
Katika siku za karibuni Rais Dkt. Samia amekuwa mstari wa mbele katika kutoa hasa kwenye soka la Tanzania, ambapo alifanya hivyo kwa klabu za Simba na Yanga zinazoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa upande wa Simba na Kombe la Shirikisho kwa upande wa Yanga.
Rais Dkt. Samia amekuwa akitoa kiasi cha shilingi milioni tano kwa kila goli na hadi hatua ya makundi inakamilika ameshatoa zaidi ya milioni 80 kwa timu hizo mbili.
0 Comments