Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) Prof. Elifas Bisanda, ametoa wito kwa wanajumuiya wote wa OUT kutekeleza azimio la chuo Kikuu Huria cha Tanzania kupanda miti ifikapo Aprili Mosi 2023.
Prof. Bisanda, ametoa wito huo wakati akizindua kampeni hiyo katika kituo cha mkoa wa Manyara kilichopo mjini Babati, Machi 23, 2023 alipofika kuhudhuria mkutano wa 42 wa Bunge la Wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania unaoendelea katika kituo hicho.
"Nawakumbusha wakurugenzi wote wa vituo vya OUT nchi nzima, kuendelea kupanda miti kote nchini, Aprili Mosi kila mwaka ni siku rasmi ya OUT kupanda miti, tunazindua hapa sababu tumekutanishwa na Bunge la 42 Wanafunzi, ila maeneo ambayo mvua zinaendelea kunyesha waanze kupanda miti pia. Upandaji huu uwe endelevu mpaka maeneo yetu yote yawe kijani cha kuvutia.” amesema Prof. Bisanda.
Aidha, Prof. Bisanda, ameishukuru Taasisi ya Misitu Tanzania (TFS), ambao wamekuwa wakiipatia OUT miche ya miti bila malipo yoyote. Alisitiza pia, kwa vituo vya mikoa ambavyo havina nafasi ya kupanda miti wanapaswa kuangalia eneo la jamii ambalo watakwenda kupanda miti na watimize azma ya OUT ya kuifanya Tanzania kuwa ya kijani.
Akizungumzia zoezi hilo, Naibu Makamu Mkuu wa OUaT– Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam, Prof. Deus Ngaruko, amesema miti ni uhai hivyo kwa mwaka huu chuo kitahakikisha miti yote inayopandwa inapata ustawi wa viwango vya juu kabisa.
"Mwaka jana tumepanda miti 1800 japo baadhi ya miti ilikufa kutokana na ukame mkali hasa maeneo katikati ya nchi yetu, mwaka huu kwa sababu tuna maeneo ya kwetu ambayo ni makubwa tunajikita zaidi katika kupanda miti katika hayo maeneo yetu.” amesema Prof. Ngaruko.
Aidha, Prof. Ngaruko, ameongeza kuwa ni vyema kila Mtumishi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania awe na angalau miti kumi katika maeneo yake inayohudumiwa vizuri.
Naye Rais wa Serikali ya wanafunzi wa OUT, Felix Lugeiyamu, amesema wanaunga mkono kampeni ya chuo ya kupanda miti ambayo lengo ni kuhakikisha mazingira ya nchi yanakuwa salama na yenye kuvutia.
"Hapa kila mkoa unawakilishwa na wabunge wawili, tukimaliza bunge hili rai anayobeba kila mbunge ni kwenda kuelimisha wananchi wote wanakotoka kuhakikisha mazigira yanatunzwa na moja ya utunzaji wa mazingira ni kupanda miti.” Alimaliza kusema Ndg. Lugeiyamu.
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kupitia azimio lake la upandaji miti kimekuwa kikitekeleza kwa vitendo azimio hilo kwa kupanda miti nchi nzima ili kuhakikisha mazingira ya Tanzania yanakuwa mazuri na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Kwa mwaka 2022, OUT ilifanikiwa kupanda miti zaidi ya 1,800 na mwaka huu 2023 makadirio ni kupanda idadi sawa na hiyo.
0 Comments