Wanahabari wakipata chakula kilichopikwa kwenye majiko Maalum yanayopunguza gharama za umeme |
Na Jimmy Charles,
WILAYA, mikoa na miji mbalimbali nchini imeshauriwa kuuona umuhimu wa kutenga maeneo maalum yatakayotumika katika uwekezaji wa miradi ya uzalishaji wa niashati jadidifu na nishati mbadala za aina mbalimbali.
Hatua hiyo imetajwa kuwa itasaidia kutoa nafasi kubwa zaidi ya kuchochea na kuvutia wawekezaji wa ndani nan je ya nchi kwenye sekta ya Nishati.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa kitengo cha mazingira kutoka wizara ya Nishati, Emillian Nyanda alipozungumza wakati wa semina maalum iliyowahusisha waandishi wa Habari za mazingira, TaTEDO na serikali.
Katika semina hiyo pamoja na mambo mengine Nyanda alizungumzia nia njema ya serikali katika kutafuta namna sahihi ya kuongeza vyanzo vya nishati nchini vitakavyomsaidia mwananchi kuondokana na uharibifu wa mazingira kwa kukata miti hovyo.
Alisema lengo la serikali ni kuona kunakuwa na kasi ya uwekezaji kwenye eneo la nishati jadidifu.
“Nia
ya serikali ni kuona nchi inaondokana na matumizi makubwa ya kuni na mkaa, ili
kulifanikisha suala hili ni lazima kuwepo na vyanzo mbadala vya nishati.
“Na tutafikia azma hii kama kila halmashauri itatenga maeneo maalum yatakayotumika kwa uwekezaji wa kuzalisha nishati mbadala.”
Alisema kwa sasa hakuna utamaduni wa kutenga maeneo maalum yatakayotumika kuzalisha nishati jadidifu, lakini wakati wa kufanya hivyo umefika, ni vema maeneo hayo yakatengwa ili kuwavutia wawekezaji.
Hata hivyo alibainisha kuwa pamoja na halmashauri nyingi kutotenga maeneo hayo, lakini tayari zipo chache ambazo zimeshaona umuhimu wa kutenga maeneo hayo.
Aliitaja miji ambayo tayari imeona umuhimu wa kutenga maeneo hayo kuwa ni Same mkoani Kilimanjaro, Manyoni na Shinyanga.
Katika kuonesha dhamira njema ya serikali katika kusaka vyanzo vingi vya nishati, Nyanda alisema mwaka 2023 kuna uwezekano mkubwa wa kujengwa mtambo mkubwa wa kuzalisha umeme wa mwanga wa jua utakaozalisha megawati 150, ambapo kwa kuanzia mtambo huo utazalisha megawati 50.
Mtambo
huo unatarajiwa kujengwa Kishapu na kwamba kuna kila sababu ya kuongeza uelewa
kwa jamii pamoja na wafanya maamuzi ili kufanikisha dhana ya uzalishaji wa
nishati jadidifu kwa maendeleo ya taifa.
0 Comments