Katika kuhakikisha usimamizi wa Mazingira na utunzaji wa mazingira unakuwa si nadharia, bali ni vitendo zaidi, Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ameahidi kusimamia hatua ya kulifanya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linakuwa mamlaka kamili.
Waziri Mkuu ametoa ahadi hiyo Mei 28,2026 katika Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Mazingira lililokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 40 ya kuanzishwa kwa NEMC.
Kongamano hilo la siku mbili linalofikia tamati leo Mei 29,2026, linafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataia cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mwigulu mesema jukumu la kulinda mazingira linapaswa kuongezewa meno ili kuhakikisha kiwango cha utunzaji na uhifadhi wa mazingira kinaongezeka.
“Tuna kila sababu ya kuifanya NEMC kuwa Mamlaka kamili, hii itasaidia kuliongezea nguvu ya kusimamia mazingira ya nchi.”
Hatua hiyo imepongezwa na wadau mbalimbali wa mazingira, ambapo Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Nchini (JET) John Chikomo alisema ni hatua nzuri kwa NEMC kuwa NEMA (National Environment Authority), kwamba hatua hiyo itaongeza ufanisi katika utendaji wa baraza hilo.
Katika siku za karibuni kumekuwa na mchakato wa kuifanya NEMC kuwa NEMA, ambapo muswada wa kulifanikisha hilo unatarajiwa kuwasilishwa bungeni wakati wowote kuanzia sasa.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Reuben Kwagilwa, aliwahi kusema hayo jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao kazi kati ya NEMC na wadau wenye viwanda.
Amesema serikali kwa upande wake imeshakamilisha mchakato mzima wa kuifanya NEMC iwe mamlaka kamili kwa kufanya mashauriano na wadau mbalimbali na wataalamu washauri.
Amesema mchakato huo utawasilishwa bungeni na baada ya hapo wananchi watapewa nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu muundo wa mamlaka hiyo na kutaka wananchi kujitokeza kutoa maoni wakati huo
“Niwatoe hofu wananchi na wadau kwamba kwa NEMC kuwa mamlaka haimaanishi kwamba itakuwa inafanyakazi kwa mabavu mabavu au kwamba itamwonea mtu, badala yake ndipo itafanyakazi zake kistaarabu zaidi kwa hiyo msiogope,” amesema
Aidha, ameitaka NEMC kuhakikisha wananchi watakapoitwa kwenda kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya muswada huo kujitokeza kwa wingi wakiwemo wadau muhimu wenye viwanda.
“Nawaomba sana NEMC kipindi hicho kitakapofika wananchi na wadau wa viwanda wapewe taarifa waje kutoa maoni yao ili tutakapotunga sheria hiyo iwe shirikishi kwa watu wote kusiwepo na malalamiko kwa wananchi wetu,” amesema.
Naibu Waziri amesema amefurahi kuona namna wenye viwanda walivyojitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo muhimu na akaitaka NEMC ihakikishe vikao kama hivyo vinafanyika mara kwa mara.
Naibu Waziri, amesema amefurahi kuona mjadala umekuwa na manufaa makubwa sana kwani wamezungumza kuhusu mambo mengi yakiwemo ya uzingatiaji wa sheria na vibali vya tathmini ya athari kwa mazingira EIA.
“Tumejadiliana kwa kina kuhusu uwepo wa mambo ya mipango ya ardhi na mwingiliano na jamii ambayo haihusiani na viwanda kwenye maeneo ya viwanda tumejifunza mengi na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira inawapongeza kwa kushiriki mkutano huu na kutoa maoni yenu,” amesema
Amesema kwenye mkutano huo wamejadiliana kuhusu mifumo kusomana akitolea mfano kuwa wadau hao wameshauri NEMC na Osha ziweze kusomana kwenye mifumo yake ili kuwapunguzia mzigo wenye viwanda.
“Nawapongeza sana NEMC kwa kuanda kikao hiki, tunanaelekea uchumi wa Dola trilioni moja sasa ili tufike huko vikao kama hivi ni muhimu sana si tu kwamba kwasababu tu tunaenda kwenye miaka 40 tuwe tunafanya vikao kama hivi kila baada ya muda flani,” amesema
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi amesema amefurahi kuona wenye viwanda wamejitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo na kwamba ameyapokea na atafikisha maoni yao kunakohusika.
Amesema changamoto zilizotolewa na wenye viwanda zitafikishwa sehemu husika ili mwaka ujao wa fedha waweze kuanza wakiwa na utaratibu mzuri wa kutunza mazingira pamoja na viwanda.
“Nawashukuru sana mmetoa maoni ya kuboresha, NEMC ni mama na kazi ya mama ni kulea tumepewa kazi ya kuwalea watumiaji wa mazingira ili kuhakikisha wanapozalisha kuna kuwa hakuna uhalibifu wa mazingirana wote tunapata manufaa makubwa,” amesema
“Mapenzi ya mama wakati mwingine ni kufinya kwaajili ya kurekebishana. Hatutaki kuwaumiza tunataka tufuate sheria na kanuni, sisi tunataka kufanya kazi ya kusimamia mazingira kidijitali ili tutoe huduma sahihi na kwa wakati na yenye haki,” amesema
“Kwa sasa tuna mfumo wetu wa ukaguzi kidijitali unaitwa mazingira APP na mfumo wa zamani tunauboresha tunafanya kazi ya kuboresha mfumo wa tathmini athari kwa mazingira,” amesema
Amesema mwishoni mwa mwezi wa tano NEMC inaenda kuzindua mfumo wa ukaguzi wa kupima athari za viwango vya uchafuzi wa mazingira, hali ya hewa na hali ya mitetemo.
“Mfumo huo wa kidijitali utapima kwenye APP yetu wote tutaona hakutakuwa na uonevu na mwisho wa mwezi huu tutazindua mfumo unaoitwa Tanzania Online Continues Assessment Environment Emission System,” amesema
Amesema mfumo huo umeshaanza kufanyakazi kwenye nchi za Afrika kama Ghana, Nijeria na Kenya hivyo alisema wanataka mifumo yao iwe inasomana na kwamba unatarajiwa kuanza kutumika kuanzia mwezi Julai.
0 Comments