Ticker

7/recent/ticker-posts

BODI YA IDHIBATI YA WAANDISHI WA HABARI YAWAONYA MAKANJANJA

  

Mwenyekiti wa JAB, Tido Mhando,

NA. JIMMY KIANGO,Dar es salaam.

BODI ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imewaonya Watu wanaojihusisha na kazi ya uandishi wa Habari, huku wakijua wazi hawana sifa za kufanya hivyo wasithubutu kuwasilisha vyeti feki ili wapate usajili rasmi.

 Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa JAB, Tido Mhando, Mei 19,2025 kwenye ofisi za bodi hiyo, jijini Dar es Salaam, alipozungumza na Waandishi wa Habari na Wahariri.

Tido alisema zoezi la kusajili Waandishi wa Habari limeanza rasmi na kuwataka wale wenye vigezi kuanza kujisajili rasmi kwenye mfumo.

“Nataka kutangaza kuwa usajili umeshaanza na vitambulisho vinatoka, hata hivyo nataka niwaonye wale waandishi waliojichomeka na wanajua hawana sifa, wasitujaribu maana tumejipanga vizuri, kama huna vyeti halali, usithubutu kufoji, muda upo nenda kasome, ukitujaribu usije kuleta lawama, maana huku kwetu hakuna kujuana,”alisema Tido.

Alisema zoezi la usajili linamuhusu Mwandishi mwenyewe na wala si la taasisi husika, ingawa barua ya taasisi itahitajika, waandishi watakaosajiliwa watapatiwa vitambulisho maalum  (Press Card) vitakavyowawezesha kufanya kazi zao kwa heshima na uadilifu.

Aliongeza kuwa JAB itawaongezea hadhi na heshima waandishi wa Habari kama ilivyo kwa wanataaluma wengine.

“Waandishi wa habari waliothibitishwa watakuwa huru kutekeleza majukumu yao, na wale ambao watakuwa hawajasajiliwa hawatakuwa na haki ya kufanya kazi ya uandishi wa Habari kwani wakifanya bila kusajiliwa watakuwa wanatenda kosa la jinai na wanaweza kushtakiwa na kuchukuliwa hatua stahiki.

“Kuwathibitisha waandishi wa habari ni hatua muhimu katika kuhakikisha taaluma ya uandishi wa habari inakuwa na hehima kama walivyo Madktari, Wanasheria na Wahandisi.


Amefafanua kuwa kusajiliwa rasmi kutawasaidia waandishi kulinda haki zao wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.

Tido ameongeza kuwa Waandishi wa habari wanaotambulika rasmi wana nafasi nzuri ya kulindwa dhidi ya vitisho, manyanyaso, na madhila wanayoweza kukumbana nayo kazini.

“JAB imekuja kwa ajili ya kuimarisha mazingira salama ya uandishi wa habari, tunaamini hatua hii itakuza hadhi na heshima ya taaluma ya uandishi wa habari. Kama ilivyo kwa taaluma nyingine kama sheria na udaktari, uandishi wa habari unapaswa kutambuliwa rasmi kama taaluma yenye hadhi na umuhimu mkubwa katika jamii,”alisema.

Amesema maombi ya ithibati na vitambulisho (Press Cards) yatafanyika kupitia Mfumo unaoitwa TAI-Habari unaolenga kuboresha huduma, kuimarisha usimamizi wa taaluma ya Uandishi wa Habari na kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho kwa waandishi waliothibitishwa.

“Waandishi wanapaswa kuingia kwenye kiunganishi https://www.taihabari.jab.go.tz na kufuata maelekezo ya kujisajili.

“Baada ya kujaza taarifa kwa usahihi, mwombaji atapokea msimbo (code) kupitia SMS na kiungo kwenye barua pepe ili kuendelea nahatua za kujaza wasifu, kufanya maombi, kupata ankara ya malipo, kulipia na kuwasilisha maombi ya kupata Kitambulisho (Press Card),”amesema.

 







Post a Comment

0 Comments