Ticker

7/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA ATAKA HATUA ZA HARAKA KUCHUKULIWA KWA WANAHARAKATI WA NJE WANAOINGILIA MAMBO YA NDANI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Ndani, pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za haraka dhidi ya watu wanaotumia mitandao na teknolojia vibaya. 

Mbali na hilo, Rais Dkt. Samia amekemea vikali wingi wa wanaharakati kutoka nje ya nchi wanaojaribu kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania na kuhatarisha amani.

Akizungumza Mei 19, 2025, wakati wa uzinduzi wa Sera mpya ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la Mwaka 2024), Rais Dkt. Samia amesema kuwa sera hiyo sasa ina misingi minane badala ya saba ya awali.

Mabadiliko hayo yamelenga kuvutia uwekezaji mkubwa wa mitaji ili kuchochea biashara na kukuza hadhi ya taifa kimataifa kwa kutumia vizuri rasilimali za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

Aidha amewaonya wanaharakati kutoka nje ya nchi wanaokuja kuvuruga amani na utulivu wa Tanzania, akisisitiza kuwa tusikubali kuwa shamba la bibi.

“Tusiwe shamba la bibi, mtu hawezi kuja Tanzania na kusema analotaka bila mipaka. Tumeshuhudia wanaharakati wakianza kuvamia na kuingilia mambo yetu. Wameshavuruga kwao, sasa wanataka kuvuruga nah uku, tusikubali watuharibie hapa kwetu.”

Rais Dkt. Samia pia amesema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakimsema vibaya, akisisitiza kuwa:

“Ninalolifanya ni kulinda nchi yangu, hatutatoa nafasi kwa yeyote kutoka nje au wa ndani kuja kutuvuruga.”

Amezitaka wizara husika kutoa ufafanuzi wa mara kwa mara kuhusu taarifa mbalimbali zinazotolewa na wanaharakati na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa endapo kuna ukweli wowote unaohusu sekta zao.



Aidha, ameelekeza kuwa taasisi za umma zipewe mafunzo ya kina juu ya maudhui ya sera hiyo na namna inavyogusa majukumu yao ya kila siku. Vilevile, mabalozi wa Tanzania walioko nje ya nchi wametakiwa kuisoma, kuielewa na kuitangaza sera hiyo kwa lengo la kuonyesha matokeo chanya ya utekelezaji wake.

Ameeleza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo alilolitoa Bungeni Aprili 2021, ambapo mabadiliko hayo yamezingatia mageuzi makubwa yaliyotokea ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miaka 20.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amepongeza uzinduzi wa sera hiyo, akiwataka Watanzania kuitumia kama nyenzo ya kulinda na kuitetea nchi duniani pamoja na kukuza ushirikiano wa kimataifa wenye manufaa kwa taifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano, Mahmoud Thabiti Kombo, amesema kuwa vipaumbele vya sera hiyo ni pamoja na kuimarisha nafasi ya Tanzania kimataifa kupitia diplomasia ya uchumi, kulinda maslahi ya taifa, na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa. Ameongeza kuwa sera hiyo inatambua nafasi ya Kiswahili kama bidhaa ya taifa na kuwapa Watanzania waishio ughaibuni nafasi maalum katika ajenda za kidiplomasia

 


Post a Comment

0 Comments