Mwenyekiti Maya wa DCPC, Bakari Kimwanga
NA MWANDISHI WETU, AFRINEWS SWAHILI -DSM
Migogoro isiyokwisha ndani ya Klabu ya Waandishi wa Habari wa jiji la Dar es Salaam (DCPC) ambao sasa wanajulikana kama Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam (DPC), imemkera mwenyekiti mpya wa klabu hiyo Bakari Kimwanga na kuwataka wanachama wake kuacha 'utoto’.
Kauli hiyo ameitoa Februari 28,2025 jijini Dar es Salaam, mara baada ya wanachama wa klabu hiyo kukamilisha zoezi la uchaguzi lililomweka madarakani Kimwanga kwa kupigiwa kura 68 za ndio.
"Ndugu zangu tunatia aibu, utoto ni mwingi mno, hatuwezi kuwa na klabu ya migogoro kila mara, tunachaguana hapa, halafu baada ya muda mfupi tunaanza kufukuzana, huu ni utoto, tunapaswa kuuacha.
"Njia pekee ya kufikia maendeleo ni kuwa wamoja, kushirikiana na kupendana, tukiweka vitu hivyo mbele, basi tutafanikiwa, lakini pia ni muhimu tukiweka uwazi na usawa kwenye kila jambo.
"Haiwezekani sisi mlezi wetu awe ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, halafu hatuna hata kipande cha ardhi, tunashindwaje kuzungumza nae na kuona ni namna gani tutajikwaamua kutoka kwenye hali ngumu, nawahakikishieni tunaweza, muhimu tushirikiane."
Kimwanga ambae alikuwa ni mgombea pekee wa nafasi ya uenyekiti, aliahidi kushirikiana na kujifunza namna sahihi ya kuongoza kutoka kwa viongozi wa vyama vya kihabari vilivyofanikiwa kama.vile Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Kwa ushindi huo Bakari anakuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo ambayo ina wandishi wa Habari wa Dar es salaam wapatao 178.
Matokeo ya ushindi wa Bakari yametangazwa na Mwenyekiti wa Kamati huru ya uchaguzi, Wakili wa Kujitegemea, Raphael Awino.
Mkutano huo wa uchaguzi ambao umehudhuriwa na wandishi wa Habari wa Dar es salaam wapatao 96 pia umemchagua, Mary Geofrey, kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kura 70 za ndiyo huku kura saba zikiwa za hapana na nne zikiharibika.
Wajumbe watano wa bodi waliochaguliwa na kura zao kwenye mabano ni Selemani Jongo (69), Penina Malundo (62), Andrew Msechu (67), Khamis Miraji (59) na Veronika Mrema (69), mgombea ambaye kura zake hazikutosha ni Selemani Msuya (43).
Uchaguzi huu umehitimisha uongozi wa Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Sam Kamalamo na Katibu wake, Fatma Jalala ambao walibaki na Mjumbe wa bodi mmkja Salehe Mohammed baada ya viongozi wengine kujiuzuru bila sababu za msingi na baadhi yao kukiri waziwazi kuwa walijiuzuru kwa kufuata mkumbo.
Waliojihudhuru kutok ni pamoja na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Salome Gregory, Naibu Katibu Mkuu, Chalila Kibuda, Mweka hazina Patricia Kimelemeta, Shabani Matutu, Njumai Ngota, Taus Mbowe na Ibrahim Yamola.
Hatua hiyo ya utoto imezungumzwa pia na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo walipokuwa wakiwauliza maswali wagombea.
Hata hivyo kuchaguliwa kwa Kimwanga kunatazamwa kama ni hatua nzuri ya kuifanya DCPC kuwa klabu imara na hasa ukizingatia kuwa mwenyekiti huyo mpya ana uzoefu wa uongozi ndani ndani ya vyumba vya Habari na hata kwenye majukwaa ya kisiasa.
0 Comments