Washiriki
wa mkutano ambao ni wadau wa mazingira kutoka taasisi mbalimbali nchini wakiwa katika
picha ya pamoja |
NA SIDI MGUMIA, TANGA
Mkutano wa wadau wa mazingira nchini uliofanyika hivi karibuni mjni Tanga umebaini kuwa juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi bado zinahitajika na iko haja ya kuongeza ushirikiano wa kitaifa na kimataifa.
Mkutano huo ni sehemu ya Mradi wa Uhifadhi mzuri wa
maeneo makubwa ya bahari kwa ajili ya maendeleo endelevu ya watu, hali ya hewa na viumbe (ReSea)
unaotekelezwa na shirika la Mission Inclusion (Mi) na Shirika la Umoja wa
Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) nchini Comoro, Kenya, Madagascar,
Msumbiji na Tanzania.
Mradi huo unalenga kuimarisha uwezo wa kustahimili
hali ya kijamii na kiuchumi kwa watu wanaoishi katika jamii za pwani na
kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi Mkurugenzi Idara ya
Misitu Zanzibar, Said Juma Ali amesema “Sisi kama wadau wa mazingira tunahitaji
kushirikiana kikamilifu na tuwe wawakilishi wema kwa jamii zetu na kwa kupitia
mradi huu wa ReSea tuwe mfano mzuri hata kwa wengine kwakua tayari tunayo mambo mengine mengi
ambayo tunajivunia kama waanzilishi na kuwa mfano wa kuigwa.
Afisa Uvuvi kutoka Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Abdalla Hemed akiwasilisha yaliyojiri kikao kilichopita walipojadili maeneo yaliyopendekezwa kwa ajili ya mradi Pemba |
Ameongeza kuwa mradi huo umekuja kwa ajili yakusaidia
kurejesha mifumo ya ikolojia, hivyo ikiwa hai basi kila kitu kinakuwa sawa. Pia
amewasihi wanajamii kuacha kufanya matumizi yasiyo ya msingi kwenye maeneo yao,
wasimamie mazingira ili kurejesha uoto wa asili kwa manufaa ya nchi.
“Ukweli ni kwamba Tanzania itajengwa na sisi
wenyewe, watu watakuja kutusaidia tu na itakuwa ni kuendeleza pale tulipofikia
hivyo tuna kila sababu kusimama imara kama wataalamu na kushiriki kutoa
michango yetu yenye tija ili kuhakikisha mradi huu unasonga mbele kwa faida ya
nchi nzima,” alisisitiza Ali
Awali akiongelea lengo kuu la mkutano huo Afisa NbS
kutoka IUCN, Selemani Mohamed amesema wamekutanisha wadau ili watoe ushauri na
kujadili juu ya kutambua na kuanzisha maeneo ambayo yatatumika kama shamba
darasa katika kutumia suluhisho za asili (Nature based Solutions-NbS) katika kukabiliana
na uharibifu wa mazingira kwa kuzingatia masuluhisho ya urejeshaji wa mfumo
ikolojia jumuishi katika bahari ya Tanga-Pemba.
Aliongeza kuwa mkutano huo pia ulilenga kujadili kuundwa
kwa mtandao ambayo itakuwa ni maalumu kwa ajili yakuendesha na kusimamia
shughuli za mradi wa ReSea katika maeneo yaliyopendekezwa kwa lengo la kuhakikisha
mradi unafanyika kikamilifu lakini pia ili ulete matokeo chanya kwa jamii na
nchi kwa ujumla.
Akitoa mchango wake Afisa Mazingira Mkoa wa Tanga, Mary Faustine amewasihi wadau wa mazingira ambao wameshiriki katika mkutano huo kuwa mabalozi wazuri wa mradi kwa kutoa elimu kwa wana jamii lakini pia kuendelea kutoa ushirikiano kwa mradi ili waweze kutimiza malengo yake.
“Lazima jamii na wataalamu wa serikali na mradi tufanye
kazi kwa pamoja kwa kuwapa ushirikianao wanajamii pale wanapohitaji msaada wetu
ili mradi huu ulioko chini ya IUCN uweze kuwa endelevu na uweze kuleta matokeo
chanya.”
“Pia kwakua hii inahusiana na madadiliko ya tabia
nchi niwaombe IUCN kupitia mradi huu wa ReSea ikiwapendeza muongeze maeneo ya
kuyafanyia kazi kwakua kuna maeneo mengine mengi yameathirika kama Handeni na
kwingineko ili kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kusukuma gurudumu la taifa.
Ninashukuru na kuwapongeza kwa lengo zuri la mradi ambalo linaendana kabisa na
vipaumbele vya taifa letu”, alisema Faustine
Mtaalamu kutoka Taasisi ya Sayansi za Bahari, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, Edward Paul akiongea na washiriki wa mkutano |
Kwa upande wake Afisa Uvuvi Wilaya ya Pangani, Joel
Mabagale akitoa mrejesho wa maeneo yaliyopendekezwa kwa ajili ya kutekeleza
mradi, alisisitiza kuwa zoezi hilo limefanywa kwa kuzingatia jamiii kwakua
wanatambua mchango wao na kuwathamini, hivyo wana jamii walishirikishwa
kikamilifu kwenye zoezi hilo muhimu.
“Zoezi hili limewashirikisha wanajamii kwa asilimia
zote kwakua wao ndio walengwa wakuu katika mradi, wanayafahamu kwa undani
maeneo wanayoishi na wanajua ni maeneo gani yanahitaji kuzingatiwa zaidi. Vilevile,
baadhi yao wameshaanza kufanya urejeshaji kwenye baadhi ya maeneo na matokeo
yameanza kuonekana,” alisema Mabagale
Aidha, Mabagale alisema kuwa kwa upande wa Tanga
katika maeneo ya Pangani na Mkinga walipendekeza baadhi ya maeneo kama vile Kwa
Mchaga, Jangwa la Mchawi, Kwa Mngumi, Kipwani, Wanaunguja, Mtoni na Mwaluseba. Kwa
Pemba walipendekeza eneo moja moja kutoka katika wilaya zote nne za Micheweni,
Wete, Chake Chake na Mkoani. Maeneo hayo
yalipendekezwa kwakua ndio yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi na
yanahitaji kufanyiwa kazi.
Akieleza changamoto wanazokutana nazo kwenye jamii, Afisa
Urejeshaji Mikoko kutoka taasisi ya Mwambao, Catherine Fridolin anasema kuwa changamoto
juu ya masuala ya NbS ni kwamba uelewa bado ni mdogo, wengi hawafahamu kwa nini
mikoko itunzwe na inafaida gani.
“Bado tunaona kuna uhitaji wa kuongeza elimu kwa
jamii lakini pia kuongeza ushirikiano kati ya taasisi zisizo za kiserikali na
za kiserikali kama vile Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kwenye kueneza elimu na
ujuzi juu ya upandaji na uoteshaji wa mikoko. Pia tunaona katika maeneo tunayofanya
nayo kazi hamasa hakuna, watu wa kamati ya kutunza mikoko bado hawayatambui
majukumu yao vizuri,”
Aliongeza kuwa, “elimu hiyo itolewe kwakuwaelimisha
juu ya masuala ya kufanya doria za mikoko, kuchukua takwimu na taarifa muhimu
za aina ya miche, idadi yake na kujua lini wamepanda na ni kwa muda gani ili
kuhakisha kwamba wanakuwa mstari wa mbele kuzimiliki na kuzitunza hizi
rasilimali na kuzirejesha katika uhalisia wake kwa ajili ya maisha yetu lakini
pia kwa vizazi vijavyo,” alisema Fridolin
Kuhusu ushiriki wa wanawake, Fridolin alisema kadri
mambo yanavyokwenda wanaona muitikio wa wanawake umekuwa mkubwa na hata
ushiriki wao katika Umoja wa Usimazi wa Rasilimali za Bahari (BMU) ni mkubwa
ukilinganisha na hali ilivyokuwa hapo awali, kifupi ni kwamba idadi ya wanawake
kushiriki kwenye kuzitunza rasilimali zilizopo hasa mikoko inaridhisha.
Washiriki wa mkutano wakifuatilia mawasilisho kwa makini |
Naye Afisa Misitu kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI,
Felista Kagembe ameshauri kwamba ni vyema wakati wa zoezi wataalamu wazingatie
kutokutumia mimea vamizi kwani ni hatari na huharibu kabisa mimea asilia ambapo
inaweza pia kuharibu viumbe hai vya majini na kusababisha vikatoweka kabisa.
Pamoja na mambo mengine wadau hao walikubaliana kwa
pamoja kuendelea kutoa ushirikiano kwa ajili ya kuunga mkono mradi katika hatua
zote muhimu zinazoendelea kwakua imani kubwa waliyonayo ni kwamba ili mradi
ufikie malengo yake ni vyema wadau wote wakashiriki kikamilifu.
Washiriki wa mkutano wakifuatilia jambo |
Mkutano huo wa siku mbili uliandaliwa na IUCN na
kuhudhuriwa na wadau wa mazingira kutoka taasisi mbalimbali kama vile Chama cha
Waandishi wa Habari za Mazingra Tanzania (JET), Shirika lisilo la kiserikali la
Sea Sense, CAN Tanzania, Shirika la UZIKWASA, Maafisa Uvuvi kutoka Tanga na
Pemba pamoja na Mtandao wa Jamii za Pwani, Pemba, Unguja na Tanga.
0 Comments