Ticker

7/recent/ticker-posts

WAHARIRI WAIPONGEZA JET, GIZ KWA KUWAPA ELIMU YA HABARI ZA UHIFADHI

Wahariri kutoka vyombo vya habari mbalimbali nchini wakiwa katika picha ya pamoja na wawezeshaji wa mafunzo kutoka JET na GIZ 

NA JIMMY KIANGO

Moja ya habari zinazopaswa kutazamwa kwa jicho la tatu na kupewa kipaumbele zaidi ni zile zinazohusu masuala la mazingira na uhifadhi.

Kwa kulijua hilo Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) Septemba 5-6, 2024 kiliwaweka pamoja wahariri zaidi ya 20, wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani na kuwapa mafunzo maalum ya kuripoti kwa tija habari za kupunguza Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori.

Wahariri walipata siku mbili za utulivu wakikutanishwa na waalimu wabobevu wa masuala ya mazingira na uhifadhi, hatua iliyowafanya wafurahie nafasi hiyo kutokana na kujifunza vitu vingi vipya.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deudatus Balile ni miongoni mwa wahariri walioshiriki mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na JET  kwa ufadhili wa Mradi wa Kupunguza Migongano Baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania, unaotekelezwa na  Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani kwa ufadhili wa BMZ.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deudatus Balile

Akizungumza na AFRINEWSSWAHILI, Balile amesema mafunzo kama hayo ni muhimu kuwa endelevu kwa Waandishi na Wahariri kwa sababu yanasaidia kuongeza uelewa hatua itakayosaidia vyombo vya Habari kuwa chachu ya kupunguza migongano hiyo.

 "Ni mafunzo mazuri na nikiri wazi kuwa nimejifunza mambo mengine mazuri na nimpongeze ofisa wa TAWA  (Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania) Isack Chamba kwa kutoa elimu sahihi juu ya namna ya kukabiliana na migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori.

"Wataalamu kama hawa ndio wanatakiwa kupewa nafasi kwenye vyombo vya Habari ili kujibu maswali, si kuwapa nafasi hiyo maofisa wasio na uwezo wa kujibu maswali kwa ufasaha. Nimefurahishwa na mafunzo haya ingawa ni ya muda mfupi, lakini nimeondoka na kitu."

Kwa upande wake Mhariri wa gazeti la Machinga na mtandao wa kijamii wa Best Media, Bakari Kimwanga amesema, mafunzo hayo yaliyotolewa na JET yana umuhimu mkubwa na hasa ikizingatiwa kuwa Wahariri ndio wahusika wakuu wa kupokea, kuchakata na kuruhusu habari iende hewani au kuchapishwa gazetini.

Wahariri Bakari Kimwanga (katikati) kutoka Best Media na Jimmy Kiango (kulia) wa AFRINEWSSWAHILI

Upendo Urembo ni Mhariri Mkuu wa Upendo Media, yeye ameweka wazi kuwa amefurahishwa na hatua ya JET ya kuandaa mafunzo ya namna hiyo kwa Wahariri.

"Ni mafunzo muhimu kwa Wahariri, sisi ndio wapokeaji wa Habari ni wazi tukijua kwa undani juu ya masuala haya ni rahisi kupitisha kitu chenye tija kwa jamii," alisema Upendo.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEF, Anita Mendoza alieleza kuwa JET inapaswa kuwa ni mfano wa kuigwa na taasisi nyengine za kihabari kutokana na uamuzi wake wa kuwanoa Wahariri juu ya masuala ya Uhifadhi.

"Nimeyafurahia haya mafunzo, ni mafunzo muhimu na naamini yameniongezea uelewa juu ya masuala ya uhifadhi na hasa kwenye eneo la migongano Baina ya Binadamu na Wanyamapori, imani niliyonayo ni kuyatumia mafunzo haya kwa tija."

TAWA YAPUNGUZA MIGONGANO...

Ofisa daraja la Kwanza kutoka TAWA, Isack Chamba akifafanua jambo kwa wahariri washiriki wa mafunzo 

Kwa upande mwengine Ofisa daraja la Kwanza kutoka TAWA, Isack Chamba amesema kuwa mamlaka hayo yamekuwa yakifanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha inapunguza migongano hiyo.

Miongoni mwa jitihada zake ni kuua wanyamapori 221 ambao walikuwa wakidhuru binadamu.

Chamba alisema zoezi hilo limetekelezwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2023/24 ambapo wanyama hao walikua wakidhuru wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchni.

Chamba amesema pamoja na kuua wanyapori 221 pia wamehamisha wengine zaidi ya 60 lengo likiwa ni kupunguza  madhara kwa jamii inayozunguka hifadhi, mapori tengefu na mapori ya akiba.

Chamba  amesema katika operesheni hiyo wamefanikiwa kuua viboko 63, fisi 43, nyati 27, simba 10, nyani na chui, huku wakifanikiwa kuhamisha simba 70, chui mmoja na fisi wawili.

Chamba amesema kwa mujibu wa sheria ya uhifadhi wa wanyamapori sura namba 283 kifungu cha 73 kinatoa mamlaka kwa afisa wa wanyamapori kuua mnyamapori yoyote ambaye  anahatarisha maisha ya watu.

 “Maisha ya binadamu ni muhimu na tunayapa kipaumbele kuliko maisha ya kiumbe yoyote yule anayeonekana  anahatarisha maisha ya watu, lengo ni  kuhakikisha jamii inakuwa salama na kuishi kwa amani” amesema Chamba.

Amesema kuwa TAWA inaendelea kuimarisha usalama kwa wananchi katika maeneo yote, huku akieleza kuwa mwaka 2023 idadi kubwa ya wanyamapori waharibifu waliouawa ni Kiboko pamoja na Mamba.

Chamba amesema wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori waharibifu ikiwemo kufanya doria ya mwitikio wa haraka kwa kushirikiana na askari wa hifadhi, askari wa wanyamapori wa kijiji.



Amesema pia kwa miaka ya hivi karibuni wameweza kuwaondoa tembo zaidi ya 500 katika makazi ya watu na kuwarejesha katika hifadhi.

"TAWA imekuwa ikitekeleza majukumu yake ya kuhakikisha wanyamapori na wanadamu wanakuwa salama, hivyo katika kufanikisha hilo tumeweza kuuwa viumbepori 221 wakorofi, tumehamisha viumbepori zaidi ya 60 na mengine mengi," amesema.

Akizungumzia zoezi la kuwaondoa tembo amesema wilaya zilizohusika ni  Nachingwea, Liwale, Bunda, Mwanga, Same, Mvomero pamoja na Mbarali.

Amebainisha kuwa changamoto iliyopo inatokana na uwepo wa shughuli za kilimo na mifugo katika maeneo ya mtawanyiko wa wanyamapori na kusababisha migongano baina ya wakulima na wanyamapori wanapokuwa wakipita katika maeneo hayo.

“Changamoto ni shughuli za kilimo hasa katika Wilaya ya Tunduru, Liwale, Nachingwea, Mvomero, Manjoni, Bunda, Serengeti ambazo zimekuwa na muongezeko wa matukio kutokana na shughuli za kibinadamu na matumizi ya wanyamapori katika maeneo hayo” amesema Chamba.

Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha jamii inayoishi katika maeneo hayo inakuwa salama kwa kuendelea kufanya doria ya kudhibiti wanyamapori kwa kuwarejesha katika hifadhi.

Ameeleza kuwa wameendelea kutoa elimu ya hifadhi kwa jamii ikiwemo namna bora ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori kipindi wanapovamia katika makazi yao.

“Lengo la elimu ni kuimarisha maisha ya  pamoja kati ya binadamu na wanyamapori hususani katika maeneo yenye muingiliano wa matumizi ya ardhi baina ya binadamu na wanyamapori,” amesema Chamba.

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru amesema chama hicho kimejipanga kutoa elimu kwa kundi la wanahabari ili kuhakikisha linatumia nafasi yake kuleta mabadiliko.

Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru akisisitiza jambo wakati wa mafunzo

Dkt. Otaru amesema iwapo waandishi wa habari watakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu migongano baina ya binadamu na wanyapori ni wazi kuwa suluhisho litapatikana.

Mkurugenzi wa JET, John Chikomo amesema mradi huo unaotekelezwa na GIZ unahusisha Ukanda wa Ruvuma na Lindi katika Wilaya ya Liwale, Tunduru na Namtumbo.

Mkurugenzi wa JET, John Chikomo

Amesema JET imekuwa ikitumia waandishi kwenda na kuona kinachofanyika katika kukabiliana na migongano baina ya binadamu na wanyamapori na kwa asilimia kubwa kuna matokeo chanya.


 

 






Post a Comment

0 Comments