Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Salimu Msemo
NA SIDI MGUMIA, DODOMA
Ujangili nchini umeendela kushughulikiwa kwa mbinu mbalimbali kwa
ushirikiano wa vyombo vya dola,wanasheria na wadau wengine wa uhifadhi. Matukio ya ujangili wa tembo yamepungua kwa kiasi kikubwa jambo
ambalo limeleta matokeo chanya kutokana na nguvu kubwa na mikakati madhubuti
iliyowekwa kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na ushirikishwaji wadau katika masuala
ya uhifadhi. Hayo ni kwa
mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Salimu Msemo alipozungumza na Waandishi wa Habari
kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) wanaotekeleza
mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa
na Shirika la USAID waliotembelea Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mjini Dodoma hivi
karibuni. Msemo, alisema kuwa mkakati uliopo sasa ni kuendelea kuboresha
namna za kupambana na ujangili kwasababu majangili nao wana mbinu mpya na
mipango kwahiyo wao kama taasisi na wadau wengine wanajipanga kuona namna
yakupambana nao. “Sisi kama taasisi na wadau wetu wengine wa uhifadhi tunajipanga
kuona namna ya kupambana na majangili,
teknolojia imekuwa kubwa kupata ushahidi ya utendekaji wa makosa haya, kuna
namna nyingi sana teknolojia na mambo mengine inatumika kabla ya kufika kwenye
kuua wanyama wetu,” alisema Msemo aliongeza kuwa taasisi imeendelea kujiimarisha katika
jitihada za utatuzi wa changamoto za ujangili na hatua zilizochukuliwa ili
kudhibiti hali hiyo ni pamoja na Sheria na Adhabu: Muundo wa
sheria umebadilishwa ili kuwa na adhabu kali kwa wale wanaovunja sheria za
uhujumu uchumi na makosa ya wanyamapori. Mwaka 2016 sheria ya makosa ya uhujumu
uchumi na makosa yakupanga, ilibadilishwa kwenye eneo la adhabu. Adhabu ya
kifungo ni kati ya miaka 20 hadi 30, jambo ambalo linatisha wahalifu. Ushirikiano wa Taasisi: Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inafanya kazi kwa pamoja na vyombo vya
sheria, polisi, na taasisi nyingine kama Shirika
la la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Wanyamapori
Tanzania (TAWA), ili kufikia mafanikio katika vita dhidi ya ujangili. Ofisi pia
imekuwa ikitoa miongozo mingi inayowasaidia kupata ushahidi kutoka nje ya nchi. Mafanikio ya Kiuchunguzi: Juhudi za uchunguzi na ukamataji wa wahalifu wa ujangili
zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa, na watu wengi wanaohusika na mitandao ya
ujangili wapo gerezani. Hii ni pamoja na kukamatwa kwa viongozi wa ngazi mbalimbali katika
biashara hii. Lakini pia kufanikiwa kuwatia hatiani watu kwenye ile mitandao
maana yake inapunguza nguvu ya mitandao na wakati mwingine kuna mitandao ambayo
imekufa kabisa. Suala hilo limepelekea nchi kuwa na taswira nzuri na wenzetu
wanakuja kujifunza, hivi karibuni tumekuwa na wageni kutoka Msumbiji wamekuja
kujifunza namna Tanzania inavyofanikiwa kwenye kupambana na makosa haya ya
ujangili. Wengi wanakuja lakini na sisi pia tumekuwa tukijifunza kutoka kwao. Mkakati Mpya:
Kuna mpango wa kukabiliana na migongano kati ya wanyama na binadamu, ambapo
hali ya wanyama inazidi kuimarika. Mikakati inaonekana kulenga kuboresha namna
ya kupambana na changamoto hizi, ikiwa ni pamoja na teknolojia za kisasa kwa
ajili ya uthibitishaji wa vitendo vya uhalifu. Biashara ya Ujangili: Kulingana na ripoti zilizopo, nchi ya China ndio inaongoza katika
biashara hii, huku meno ya tembo yakikamatwa mara nyingi. Hii inaonyesha kuwa
uhalifu huu unafanya kazi kwa mitandao ya kimataifa. Mchakato mzito wa
kupambana na ujangili umeanza kuzaa matunda. Kwa kuimarika kwa sheria na adhabu
kali, uhalifu wa ujangili umepungua tofauti na ilivyokuwa mwaka 2012 mpaka 2014,
na hivyo kunatoa nafasi kwa wanyamapori kuongezeka. Kwa upande mwingine,
Msemo alisema kuwa hivi karibuni, kumekuwepo na ongezeko la wingi wa nyamapori
katika maeneo mengi nchini Tanzania, ambayo yanaweza kuashiria mabadiliko
katika matumizi ya rasilimali za wanyama. “Kwa kawaida, wanyama
kama swala, nyumbu na wengineo wanatumika kama chakula katika jamii, lakini
hali hii inahitaji kuangaliwa kwa makini kwani inaweza kubeba changamoto na
fursa mpya. Kwa kushirikiana na wadau, tunanaweza kuhakikisha kuwa rasilimali
hizo zinatunzwa kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Msemo Kwa ujumla, ujangili umepungua kwa juhudi za uhifadhi wa
mazingira na maliasili. Ni muhimu kuendelea na mikakati hii ili kuhakikisha
wanyama na mazingira vinapatikana na kuishi kwa usalama. |
|
0 Comments