Wakina mama wakiweka alama kwenye maotea waliyochagua kwa kufunga kitambaa chenye rangi |
NA SIDI MGUMIA, DODOMA
Utunzaji wa mazingira ni juhudi za kulinda na
kuhifadhi mazingira ili kuhakikisha kunakuwepo na uendelevu wa rasilimali asili
na ustawi wa viumbe vyote.
Hii inahusisha shughuli na mikakati mbalimbali
iyolenga kupunguza athari mbaya za shughuli za kibinadamu kwenye mazingira na
kukuza matumizi endelevu ya rasilimali.
Moja ya vipengele muhimu vya utunzaji wa
mazingira ni hatua za kulinda, kudhibiti na kurejesha mifumo ya asili na
iliyorekebishwa ambayo inashughulikia changamoto za jamii kwa ufanisi na wakati
huo huo kunufaisha jamii.
Kwakulitambua hilo, Shirika
lisilo la Kiserikali ya LEAD Foundation linalojihusisha
na kukuza uongozi bora, utunzaji wa mazingira na maendeleo ya jamii, limejikita
katika kurudisha mamilioni ya miti mkoani Dodoma kwa njia ya asili ya Kisiki
Hai.
Akielezea njia hiyo kwa kina alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) wanaotekeleza mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la USAID waliotembelea Ofisi za Shirika hilo mjini Dodoma hivi karibuni, Meneja Kumbukumbu na Mratibu wa mafunzo, Hagali Mbulla, alisema Kisiki Hai ni njia ya kilimo msitu inayotumika ili kuotesha tena miti na kusaidia mimea mipya inayokua kwa asili kukua.
“Kwa kutumia njia ya Kisiki Hai na kuanzisha tena njia ya uvunaji
wa maji ya mvua, tunakusudia kurejesha udongo, kulifanya eneo kuwa la kijani
tena na kuboresha uzalishaji wa ardhi katika mkoa wa Dodoma, katikati mwa
Tanzania,” alisema Mbulla
Aliongeza kuwa njia ya
Kisiki Hai imekuwa mkombozi wa mazingira hasa katika maeneo kame kwasababu kuu
nne ambazo ni gharama nafuu, endelevu, rahisi kwa mtu yoyote kuifanya pia ina matokeo
ya muda mfupi.
Mbulla amesisitiza kuwa wao wanajikita sana katika utunzaji wa
mazingira kwa kutumia njia za asili kwa ajili ya kustawisha uoto wa asili, na
hii ni baada ya tafiti zilizofanywa kuonyesha kuwa ndio njia sahihi ya kukuza
miti katika maeneo yenye ukame.
Hali ilivyokuwa kabla na hali ilivyo sasa |
“Tulianza kwa kutoa elimu mwaka 2017 na utekelezaji ulianza mwaka
2018 kwa Wilaya ya Kongwa na baadae wilaya ya Mpwapwa na baada ya matokeo
mazuri ndipo tulipoanza kwenda na maeneo mengine,” aliongeza
“Hii miti tunayoitunza kwa njia ya asili tuna uhakika wa kuihudumia
na baadae kuwa miti mikubwa kwasababu mpaka mwezi Juni mwaka huu 2024 tayari
kuna miti milioni 22 imekua.
“Na katika kila kijiji tunachokwenda tunawafundisha wanakijiji
wasiopungua wanne kulingana na ukubwa wa kijiji na lengo ni mkulima mmoja
asimamie kaya 150, kwahiyo unakuta katika kila kijiji sasa tuna wakulima wanne
ambao wamepewa mafunzo yakutosha halafu na wao wanakwenda kuwafundisha wenzao,”
alisemaa Mbulla.
Alifafanua kuwa kwa wakulima waliopata mafunzo, hawatakuwa na kazi
ya kuwafundisha wenzao tu bali kila mkulima anakabidhiwa kaya 150 za
kuzisimamia, kila mwezi anakuwa anaripoti jinsi kazi inavyokwenda na
kuorodhesha idadi ya miti waliyootesha kutoka kwa kila mkulima.
Waandishi wa Habari kutoka JET wakisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja Hagali Mbulla |
“Kiuhalisia hali imebadilika kwasababu hata ukiangalia historia kidogo ya Dodoma miaka ya zamani kabla ya 2000 ilikuwa ikifika Oktoba ama Novemba kulikuwa na kimbunga kikali kilichopewa jina la Kimbunga cha Kongwa kwasababu kilikuwa kinatoka maeneo ya Kongwa ambako hakuna miti mpaka kinafika mjini, lakini sasa hivi wenyeji wa Dodoma wanashangaa hawakioni kile kimbunga na hii ni kwasababu tayari miti imeshaongezeka huko, imekuwa ya kutosha kwahiyo upepo unazuiliwa na kuzuia hicho kimbuga,” alisema Mbulla
Akiongelea kuhusu suala la ushiriki wa wanawake katika kukabiliana
na mabadiliko ya tabia nchi kupitia mradi wa Kisiki Hai, ameeleza kuwa
wanashiriki kikamilifu katika mradi huo na kwamba Shirika lao pia linazingatia zaidi
suala la jinsia kwahivyo hata wakulima wale wanaowafundisha kule vijijini ni
lazima kuwa na idadi sawa yani kama wanachukuliwa wanaume wawili katika kijiji
basi na wanawake lazima wawe wawili.
“Katika utekelezaji wa miradi yetu kila siku bado tunawahimiza
wanawake pia wawepo, na wanawake hawa sasa wanakiri kuwa wamepunguziwa adha ya kwenda
kutafuta kuni mbali na hii ni kwasababu sasa akienda shambani kwake tu anarudi
na mzigo wa kuni na sio kwenda mbali,” alisema Mbula
Pamoja na njia hiyo ya asili, wanatumia pia njia ya kuchimba
mitaro ambayo inaitwa makinga maji ili kuyakinga maji na kuyahifadhi shambani,
wanaitumia katika maeneo ya ukame. Maji yanayohifadhiwa hutumika mara baada ya
mvua kukatika ambapo hunywea taratibu chini ya ardhi na kuifanya ibaki na
unyevu.
Kwa upande wake Angelina Tarimo ambaye ni Afisa Ufuatiliaji,
Tathimini na Kujifunza Ukijanishaji Kidijitali alisema kuwa mafaniko ya mradi
ya Kisiki Hai yanaonekana na kwamba kwa upande wa kijiji cha Eslalei Wilayani
Monduli, kijani imerudi kwa majani ya asili,wanyama lakini pia kurudi kwa mimea
ambayo walikuwa wameshaisahau katika hilo eneo.
“Kutokana na kuwepo kwa miti mingi sasa wanyama waliotoweka kutokana na ukame wameanza kurudi. Wanyama hao ni digidigi, simbilisi, sungura na vipepeo,” alisema Tarimo
Nae Afisa Masoko na Mawasiliano wa shirika hilo, Godlove Kihupi
alilisisitiza kuwa katika miradi yao ya utunzaji wa mazingira wametumia pia
njia ya kuchimba mashimo ya umbo la nusu mwezi kwa ajili ya kukinga maji,
wamefanya kwenye maeneo yenye ukame kwa mfano Wilaya ya Monduli kwenye kijiji
cha Eslalei lakini wamefanya pia Meserani.
“Tunatumia mbinu za asili ambazo ni rahisi kutumika na jamii
ambayo tunafanya nayo kazi, lakini pia
kwa kusikia maelekezo tu mtu anaweza akatekeleza zoezi hilo katika eneo lake.
Na kwasasa maeneo ambayo tumekuwa tukiyaangazia zaidi ni kwenye ukame ili
kusaidia kutunza maotea ya miti yanapochipua kutokana na Kisiki Hai au mbegu za
miti zilizodondoshwa ardhini na vinyesi vya wanyama au ndege,” alisema Kihupi
Akielezea mafanikio ya mradi huo, mkazi wa kijiji cha Pembamoto,
Dickson Saluni alisema kuwa kijiji chao kimekuwa na jangwa kwa muda mrefu
lakini mambo yamebadilika mara baada ya kuja kwa mradi kwani sasa wamepata
nyasi, miti na sasa kijiji chao kinapendeza.
Kwa upande wake Mariam Mungane ambae ni mkazi wa kijiji cha
Pembamoto alisema kwasasa wanapata kipato kwa kuuza nyasi zinazoota kwenye
maeneo yao na imewapunguzia adha kwenda mbali kutafuta kwakua sasa wanazipata
kwenye mashamba yao wenyewe.
0 Comments