Ticker

7/recent/ticker-posts

JUKWAA LA WAHARIRI LAITAKA POLISI KUWAACHIA WAANDISHI WATATU BILA MASHARTI

 


NA MWANDISHI WETU

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limelitaka jeshi la Polisi bila mashariti kuwaachia mara moja waandishi wa Habari watatu linalowashikilia.

 

Waandishi wanaoshilikiliwa na Jeshi hilo kwenye kituo cha Polisi cha Mbalizi mkoani Mbeya, ni Ramadhani Hamisi  na Fadhili Kirundwa wa Jambo TV na Francis Simba ambae ni mpiga picha wa Chanzo TV.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, jukwaa hilo limepata taarifa ya kukamatwa kwa waandishi hao wakiwa nje ya ofisi za Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jijini Mbeya wakisubiri kufanya mahojiano na viongozi wa chama hicho.

Imeelezwa kuwa viongozi wa CHADEMA walikuwa wanaendelea na kikao cha ndani kwenye ofisi hizo.

 

TEF imeweka wazi kuwa waandishi hao walikuwa wakitekeleza matakwa ya Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inatoa haki kwa watu kukusanya, kuchakata na kusambaza taarifa bila kujali mipaka ya nchi.

 

“Sambamba na Katiba, kifungu cha 7(1)(a)(b) na (c) cha sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2026 na marekebisho yake ya mwaka 2023 kinatoa haki kwa waandishi wa Habari kufanya kazi ya uandishi wa Habari.

 

“Ni jukumu la Waandishi wa Habari kuhabarisha umma juu ya kila jambo linaloendelea, hivyo mwandishi hapaswi kukamatwa au kuadhibiwa kwa kufanya kazi hii,”imeeleza taarifa hiyo.

 

Taarifa hiyo imeweka wazi kuwa Jukwaa la Wahariri pamoja na kuendelea na mawasiliano na viongozi na taasisi mbalimbali, linavisihi vyombo vya dola kuwaachia waandishi hao mara moja bila mashariti kwa sababu kuwapo kwao katika eneo la tukio kwani linaamini walikuwa wanafanya kazi na si sehemu ya siasa au chochote kilichokuwa kinaendelea.

 

TEF ilikwenda mbele zaidi kwa kulaani matukio ya kukamatwa kwa waandishi wa Habari na kwamba matukio hayo yanaharibu heshima kubwa ya Tanzania katika kulinda Uhuru wa Vyombo vya Habari alioujenga Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani, ambapo amerejesha uhusiano mzuri na vyombo vya Habari.

 

“Sisi Jukwaa la Wahariri Tanzania, tusingependa kuona Tanzania ikirejea katika enzi za giza za kamatakamata, waandishi waliokamatwa waachiwe haraka.”

Post a Comment

0 Comments