Ticker

7/recent/ticker-posts

WIMBI LA UTEKAJI WATOTO, DIWANI KIMWANGA AFANYA MKUTANO NA WAZAZI NA WAALIMU

Diwani wa Kata ya Makurumla iliyopo ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, Bakari Kimwanga, akizungumza na wananchi wa Kata hiyo.Na MWANDISHI WETU 

-DAR ES SALAAM 

Matukio ya utekaji wa watoto yaliyoshamiri katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam, na kwenye baadhi ya mikoa, yameibua hofu na taharuki kubwa kwa wazazi hali inayowasukuma viongozi wa ngazi mbalimbali kutafuta mwarobaini wa tatizo hilo.

 

Diwani wa Kata ya Makurumla iliyopo ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, Bakari Kimwanga, ni miongoni mwa viongozi walioiona haja ya kukutana na wananchi wa kata yake ili kutafuta suluhu ya pamoja.

 

Alikutana na wananchi wa Kata yake  Julai 23,2024 na mkutano huo ulishirikisha wazazi, walezi na walimu wa shule za Msingi za Mianzini,  Karume na Dk. Omari na viongozi mbalimbali wa kata hiyo ikiwa ni pamoja na jeshi la polisi.

 

Kabla ya mkutano huo ilizuka taharuki ya kutekwa kwa watoto kwenye shule hizo na kuibua taharuki kwa wazazi kulazimika kuvamia shule ili kuona usalama wa watoto wao.

Katika mkutano huo Diwani Kimwanga aliwataka wazazi na walezi kuwa watulivu na kwamba jeshi la polisi liko makini kuhakikisha suala hilo linadhibitiwa.

 


Kimwanga alisema ingawa kwenye Kata yake hakujaripotiwa taarifa yeyote ya kutekwa ama kupotea kwa mtoto, lakini ameiona haja ya kukutana na wananchi wenzake ili waangalie kwa pamoja namna ya kukabiliana na jambo hilo mapema.

“Wakati sahihi wa kujilinda ni pale unapojiona uko salama, kwenye Kata yetu hakujatokea tatizo hili, lakini hii haitufanyi tusitafute namna sahihi ya kuhakikisha halitokea kabisa,”amesema.

 

Kimwanga alisema njia ya kwanza ya kukabiliana na jambo hilo ni kuhakikisha kila mwana jamii anakuwa mlinzi wa mtoto wa mwenzie anapokuwa mitaani.

 

"Tangu zilipoibuka taarifa hizi za Julai 22, 2024 (Jumatatu), tumefuatilia kwenye shule zetu, jeshi la Polisi limetuhakikishia hali iko shwari.

 


"Wale waliopata taharuki na kuja shule,  hawajakosea kwa sababu wamefanya hivyo kwa lengo la kutaka kujua usalama wa watoto, najua uchungu walionao akima mama. Wazazi wenzangu naomba tuwe na tulivu hali iko shwari, kubwa tusisahau wajibu wetu wa malezi na usalama kwa watoto hata wanapokuwa nyumbani," amesema Diwani Kimwanga

 

CHAKULA SHULENI

Katika kuhakikisha watoto wanakuwa salama zaidi, Diwani Kimwanga aliwataka wazazi kutoacha kuchangia kiasi cha shilingi 500, walichokubaliana kwa ajili ya chakula.

 

“Wazazi wenzangu ni lazima tuweka mkazo kwenye suala la lishe kwa watoto kwa kuhakikisha tunachangia shilingi 500 ya chakula kama mlivyokubaliana kwenye mikutano ya wazazi, jambo hili litamsaidia mtoto kupata chakula shuleni na kuacha kuzurula mitaani wakati waÃ¥ mapumziko.”

 

Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi, Manispaa ya Ubungo, Denis Nyoni amewataka wazazi kuwa na utulivu kwani hadi kufikia jana hakuna taarifa za watoto kutekwa katika shule kwenye manispaa hiyo.

 

"Naomba walimu msisahau wajibu wa kuandika mahudhurio ya watoto kila siku wawapo darasani na hata wakati wanapomaliza masomo kwa siku majina yaitwe. Hatua hii ndio njia ya kuendelea kudhibiti usalama wa watoto wetu," amesema Nyoni

 

Polisi Kata ya Makurumla, Insp Emmanuel Humba.

Naye Polisi Kata ya Makurumla, Insp Emmanuel Humba, amesema kuwa katika Kata ya Makurumla hali ni shwari hakuna tukio la utekaji wa watoto huku akiwaomba wazazi wawe wepesi wa kutoa taarifa pale wanaposikia uwepo wa tukio hilo.

 

Post a Comment

0 Comments