NA MWANDISHI WETU
Mwenendo usio faa wa usambazaji wa taarifa zisizo na ukweli za mauaji na utekaji wa watoto umelishtua Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na kuchukua jukumu la kukemea tabia hiyo ambayo inazua taharuki kwa jamii.
Katika miezi ya hivi karibuni, kumekuwa na kasi kubwa ya usambazaji wa taarifa za kupotea kwa watoto na utekaji wa watu huku baadhi ya watu wakienda mbali zaidi kwa kuhusisha matukio hayo na Jeshi la Polisi.
Hata hivyo Julai 15,2024 Mkuu wa Jeshi hilo, IGP- Camillius Wambura alikanusha jeshi lake kuhusika na matukio hayo na kuweka wazi kuwa ni kweli matukio hayo yapo, lakini si kwa kiwango kinachosambazwa mitandaoni.
IGP- Wambura alisema wapo baadhi ya watu wasio waaminifu wanajiteka na kujipoteza kwa nia ya kupata fedha kisha wanatumia mitandao ya kijamii kusambaza taarifa potofu zinazoibua hofu kwa jamii.
Mwenendo huo ambao umebeba sura ya kuichafua taswira ya nchi umelifanya Jukwaa la Wahariri Tanzania, leo Julai 22,2024 kutoa tamko kwa umma likikemea kitendo hicho cha kusambaza taarifa potofu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Mwenyekiti wa TEF, Deudatus Balile, imeweka wazi kuwa Wahariri wanafuatilia kwa karibu tabia iliyoibuka hivi sasa ya baadhi ya watu kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu kuuawa au kutekwa kwa watoto katika maeneo mbalimbali nchini.
“Yamekuwapo matukio kadhaa ya taarifa za aina hii katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, huko Kigamboni, Mbagala naKipawa, ambayo yameleta taharuki kubwa hadi wazazi wakafuata watoto shule, lakini baadaye ikathibitika kuwa siyo kweli.
“Tabia hii ya kupokea na kusambaza taarifa ambazo hazina uhakika au ukweli, husababisha taharuki, usumbufu, na mshtuko kwa wazazi, walezi, watoto, na wananchi kwa ujumla.
“TEF inawaomba Watanzania kutoa taarifa ambazo wana uhakika nazo ili kuepuka kusababisha taharuki na hofu kubwa.Tunaomba wananchi wasisambaze taarifa ambazo hawana uhakika nazo au kufahamu undani wa ukweli wake, kwani ni kosa la jinai kisheria na siyo maadili ya uandishi wa habari kuisumbua jamii,” imesomeka taarifa hiyo.
Hata hivyo TEF, imetoa wito kwa kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kuwatunza na kuwalindawatoto wao, lakini pia imelitaka jeshi la Polisi kuongeza ulinzi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuendelea kuaminika kwa wananchi na wajione wako salama.
0 Comments