Ticker

7/recent/ticker-posts

'ZOEZI LA KUREJESHA TEMBO HIFADHI YA TAIFA RUAHA NA PORI LA AKIBA MPANGA-KIPENGELE NI LA KUDUMU'


NA. MWANDISHI WETU
Kufuatia wanyamapori hasa tembo kutoka hifadhini na kuingia kwenye maeneo ya makazi ya watu,serikali imeahidi kuendelea kuwarejesha wanyamapori hao kwenye maeneo yao wanayostahili kuwepo.

 

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki  Mei 9,2024 wilayani Mbarali mkoani Mbeya wakati wa uzinduzi wa zoezi la kurejesha tembo katika maeneo yao.

 

Zoezi hilo linahusisha Kata tano za Igava, Mawindi, Miyombweni, Imalilosongwe na Rujewa ambazo ndio waathirika wakubwa.

Katika uzinduzi wa zoezi hilo Waziri Kairuki amewahakikishia wananchi wa Mbarali  na Watanzania kwa ujumla kuwa zoezi hilo ni endelevu na serikaoi inaamini litaleta tija na ufanisi kwa wananchi wanaokaa pembezoni mwa Hifadhi  ya Taifa Ruaha na Pori la Akiba Mpanga-Kipengele.

 

"Zoezi hili si la muda mfupi, ni la kudumu ni matumaini yangu litaleta tija na ufanisi mkubwa kwa wananchi, najua changamoto mliyokuwa nayo ndio maana Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeamua kulishughulikia kwa haraka. Ndani ya muda mfupi mtaona mabadiliko makubwa."

 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la kurejesha tembo hifadhini.

Alisema kwa siku mbili wataalam wamefanikiwa kuwaswaga na kuwarudisha hifadhini takribani tembo 61, ambapo Mei 8 2024 makundi matano yenye tembo 43 yakirejeshwa hifadhini na Mei 9,2024 tembo 18 wamerejeshwa wanakostahili kuwa.

 

Hata hivyo alitoa tahadhari ka wananchi kuwa tembo wanapovamia maeneo yeo wasijichukulie sheria mkononi kwa kuwauwa.

“Kwa kawaida tembo huwa ana tabia  ya kulipiza kisasi, lazima mtambue kuwa hata ikipita miaka mingi tembo hasahau eneo alilouwawa mwenzao au alipopata kadhia na bughuza, akipita eneo hili na akakutana na binadamu lazima alete taharuki na kujueruhi."

 

Mbali na kuwarejesha tembo hao hifadhini, zoezi hilo linaenda sambamba na ufungwaji wa mikanda maalum ya mawasiliano kwa tembo kiongozi kwenye kila kundi. 

 Kwa namna mikanda hiyo ilivyo ya kisasa pindi watakavyosogea karibu na maeneo ya watu, mikanda hiyo yenye vifaa vya kielektroniki itatuma taarifa ya uwepo wao kwa wahifadhi ambao watafika mara moja kabla  hawajavuka maeneo yaliyohifadhiwa na hivyo kusaidia jamiii kuondokana na changamoto za uharibifu wa mali.

 

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Bahati Ndingo  aliishukuru Wizara na taasisi zake: Niwapongeze wataalam kutoka TANAPA, TAWA, TAWIRI na TFS kwa kufanya kazi usiku na mchana, matokeo yameonekana, hivyo wana Igava, Ikanutwa na maeneo mengine ambapo zoezi hili linafanyika tutapata ahueni."

Zoezi la kuwaondoa tembo hao katika mashamba ya wananchi na kuwarejesha hifadhini lilianza jana Mei 8, 2024 na linaendelea.



 

 

Post a Comment

0 Comments