Ticker

7/recent/ticker-posts

ELIMU INAYOTOLEWA NA TAWA YALETA TIJA UKEREWE, WANANCHI WAMWAGA PONGEZI

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Joshua Bituri Manumbu 

NA MWANDISHI WETU

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA imewasaidia wananchi wa Wilaya ya Ukerewe mkoani mwanza sasa kuishi kwa amani baada ya kuwapa elimu ya kujihadhari na viumbe hivyo hasa mamba na viboko.

Hatua hiyo imewasaidia wananchi kutokuwa na hofu tena ya kudhuriwa na wanyamapori hao hatari wanaoingia kwenye maeneo ya makazi ya watu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Joshua Bituri Manumbu ameyasema hayo alipokuwa akitoa pongeza kwa TAWA kutokana na jitihada zao endelevu za kuelimisha jamii namna ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu na namna ya kuwadhibiti pale wanapoonekana kuhatarisha maisha ya watu.

 

Pongezi hizo zimetolewa jana Mei 08, 2024 na Mwenyekiti huyo katika ziara iliyofanywa na Maofisa wa TAWA wilayani humo.

"Tumekuwa na matukio mbalimbali ya mamba na viboko kujeruhi watu, lakini kupitia elimu inayotolewa na Maofisa hawa wa TAWA na namna wanavyowadhibiti, wameweza kuokoa baadhi ya watu lakini pia wameweza kuwaondoa wale wanyama ambao wameshafikia hatua mbaya ya kudhuru watu," amesema

 

Katika maelezo yake, Mwenyekiti huyo amesema Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na Maofisa wa TAWA kutoka Kanda Maalumu ya Mwanza na imetoa ushirikiano mkubwa kwa Maofisa hao ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.

Afisa Habari wa TAWA wa kwanza kushoto, Beatus Maganja akiwa na baadhi ya maofisa wa mamlaka hiyo wilayani Ukerewe. 

Aidha amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kuwapatia Maofisa hao vitendea kazi  vinavyowafanya waweze kutekeleza majukumu yao kama sehemu ya taasisi muhimu nchini.

 

Kwa upande wao,  wananchi wa Kijiji cha Selema kilochopo Kata ya Bwiro wilayani humo wameipongeza na kuishukuru TAWA kwa elimu wanayoendelea kuitoa wilayani humo ambayo wamekiri kuwa imekuwa ni msaada kwao na itawawezesha  kuendelea na shughuli zao za kiuchumi huku wakiepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao.

 

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Selema wilayani humo,  Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja amesema katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu Serikali inahakikisha usalama wa mwananchi unakuwa ni kipaumbele cha kwanza.

 

“Maofisa wa TAWA wamekuwepo maeneo mbalimbali nchini kutoa elimu na kufanya doria katika maeneo ambayo yanatajwa kuwa na changamoto ya wanyamapori hao.”

 

Maganja ametoa wito kwa wananchi hao kuendelea kufanyia kazi maelekezo na elimu inayotolewa na wataalamu ili waendelee kuwa salama.

 


Post a Comment

0 Comments