Ticker

7/recent/ticker-posts

TCB YATIMIZA AHADI YA KUMRAHISHIA MTEJA WAKE HUDUMA YA VIKOBA KIDIGITALI

Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Adam Mihayo akiwa pamoja na baadhi ya maofisa wa TCB wakati za uzinduzi wa huduma ya Vikoba kidigitali.

NA MWANDISHI WETU

BENKI ya Bisahara Tanzania (TCB), jana Mei 8,2024 imetimiza ahadi yake kwa Watanzania ya kuanzisha huduma ya Kikoba kidigitali itakayowarahisishia watumiaji wa kikoba kuweka fedha na kukopeshana bila usumbufu.

 

Katika kikao kazi kinachoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kati ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na taasisi za serikali, wakati wa kikao kazi cha TCB na Wahariri, kuliibuka hoja ya uhitaji wa kuwa na mfumo wa wanachama wa kikoba kupata nafasi ya kushiriki pamoja huku wakiwa na mitandao tofauti ya simu.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Adam Mihayo aliwaahidi Wahariri hao kwa niaba ya Watanzania kulifanyia kazi haraka suala hilo na jana alitimiza ahadi hiyo kwa kuzindua kikoba kidigitali kilichokuja na suluhisho hilo.

 

Akizungumza katika uzinduzi wa huduma hiyo jijini Dar es Salaam, Mihayo alisema, mapinduzi waliyoyafanya yanalenga kwenye dhana ileile inayotumika katika vikundi vilivyozoeleka vya kuweka na kukopa.

 

Mapinduzi hayo ni kuwa na aina mbili ya kikoba cha kwanza ni cha wanachama wanaotumia mtandao mmoja wa simu na kingine kikoba Mix ambacho kinajumuisha wanachama wa mitandao tofauti.

"Tunawasogezea wateja wetu huduma hii viganjani mwao ikiwa na ufanisi zaidi na urahisi maradufu...ubunifu huu ni hatua muhimu katika sekta ya kibenki katika ulimwengu huu wa kidigitali," alisema.

 


Alisema huduma hiyo inapatikana kwa urahisi zaidi kupitia simu za mkononi na benki hiyo imeshirikiana na kampuni zote za simu nchini ikiwemo Airtel, Tigo,  Vodacom na Halotel  ili kurahisisha namna ya kujisajili na kujiunga na kikoba mtandaoni.

 

"Ukiwa na kikoba mtandaoni ni salama zaidi ni rahisi kuona miamala yako na inaleta uwazi kati ya kikundi chenu cha kikoba,"alisema.

 

Akifafanua zaidi Mihayo alisema kikoba kidigitali kitakuwa na aina mbili ya vikoba, ya kwanza ni ile ya mteja kujisajili au kujiunga na kikoba kupitia mtandao wake wa simu, hicho inaweza kuwa kwa ajili ya Marafiki na familia walio kwenye mtandao mmoja.

 

"Aina ya pili ni kikoba mix ambacho hicho kinawezesha watu kutoka mitandao tofauti kuunganika kwa pamoja na kuunda kikoba kwa namba zao na ili ufungue kikoba mix utapiga *150*21# na utapelekwa moja kwa moja kwenye menu ya TCB, utafuata maelekezo na kukamilisha usajili, ni rahisi," alisema.

 


Mihayo alisema Kikoba ni zaidi ya fursa ya kidigitali kwani inabeba dhana pana ya uwazi, ujumuishi na usalama katika uwekaji wa akiba na usimamizi bora wa kifedha.

“Tukitumia nyenzo hii ya teknolojia tunaviwezesha vikundi nchini kote kusimamia mategemeo yao ya kiuchumi, kukua kiuchumi na kujitegemea," alisema.


Kwa miaka ya karibuni kumekuwa na vikundi kadhaa vya vikoba kupitia mitandao ya simu na  humo wanachama huweka akiba na kukopeshana kwa riba nafuu na TCB ndio inayohusika na huduma hiyo ya fedha kwa kushirikiana na mitandao ya simu.


Vikoba hivyo huvunjwa baada ya mwaka mmoja na vingine huvunjwa baada ya miaka mitatu hadi mitando na wanachama kugawana faida kabla ya kuanza kuwekeza tena.

 

 

Post a Comment

0 Comments