Ticker

7/recent/ticker-posts

MKAA UNAONDOA SUMU NA KUKATA POMBE MWILINI KWA HARAKA

 

Mkurugenzi wa Huduma ya Kwanza wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Bi.Moteswa Meda, akitoa mafunzo ya kumsaidia mtu aliyekwamwa na kitu kooni.

NA JIMMY KIANGO

Imekuwa ni jambo la kawaida kwa watu wengi nchini kudhani kuwa maziwa ya ng’ombe yanasaidia kuondoa sumu mwilini,sio kweli, kitu pekee ambacho kinaweza kuwa msaada wa kwanza kwa mtu aliyekunywa sumu ya aina yeyote ni Mkaa.

 

Mbali na mkaa kuwa na uwezo wa kuondoa sumu mwilini na kumpunguzia mtu uharaka wa kufa, lakini pia unasaidia kuondoa kabisa kiwango cha pombe mwilini.

 

Haya yamesemwa Januari 19,2024 na Mkurugenzi wa Huduma ya Kwanza wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Bi.Moteswa Meda wakati wa mafunzo ya OSHA  kwa Wahariri mbalimbali wa vyombo vya Habari nchini yaliyofunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule kwenye ofisi za Wakala hao zilizopo, Kinondoni, Dar es Salaam.

 

Bi. Meda alisema mkaa ni kitu muhimu kukaa nacho nyumbani kwani kina msaada mkubwa kwa binadamua hasa katika eneo la uokozi.

 

Akifundisha namna mkaa unavyoweza kuokoa maisha ya mtu aliyekunywa sumu, alisema kama mtu amekunywa sumu ya aina yeyote au idadi kubwa ya vidonge, kinachopaswa kufanyika si kumpa kimiminika chochote iwe maji au maziwa, badala yake ni kumpa mkaa atafune kama anaweza kutafuna na kama ahawezi basi apondewe ule mkaa hadi uwe unga na kumezweshwa bila maji.

 

“Kumnywesha maji au maziwa mtu aliyekunywa sumu ni kumuongezea uharaka wa kufa, maana unakwenda kuipa nguvu ile sumu isambae kwa haraka mwilini, muhimu ni kumpa mkaa atafune kwa wingi kama anaweza kutafuna, na kama hawezi basi huo mkaa upondwe pondwe na alishwe.

 

“Mkaa ukiingia tumboni kwa wingi unakwenda kuifyonza ile sumu iliyopo mwilini na kumpunguzia mtu hatarai ya kufa, hata hivyo pamoja na kutoa huduma hiyo ya kwanza, pia ipo haja ya kuhakikisha huyo aliyekunywa sumu anapelekwa hospitali kwa matibabu zaidi.”

 

Kuhusu kukata pombe, Bi. Meda alisema kwa mtu aliyelewa kwa kiwango kikubwa anaweza kurejea kwenye haliyake ya kawaida kwa muda mfupi sana endepo atatafuna mkaa.

 

“Kama mkaa unavyofanya kazi kwenye kuondoa sumu, ndivyo unavyofanya kazi kwenye kuondoa kiwango cha pombe mwilini,”alisema.

 

Aliongeza kuwa ingawa ipo mikaa inayouzwa kwa kazi hiyo, lakini pia mkaa wa kawaida unaotumiwa majumbani kwa shughuli za kupika unafaa kutumika katika kutoa huduma ya kwanza kwa mtu aliyekunywa sumu au kulewa zaidi.

 

Kuhusu sumu ya nyoka Bi. Meda alisema hakuna jiwe lolote linaloweza kuondoa sumu ya nyoka, badala yake mtu anayeweza kupona baada ya kung’atwa na nyoka huyo ajue ameng’atwa na nyoka asiye na sumu.

 

“Hakuna jiwe lolote linaloweza kuondoa sumu ya nyoka mwilini, ni uongo, ni hatari sana kudhani jiwe linaweza kuondoa sumu au kumfunga mtu Kamba katika eneo alilong’atwa kuwa kunaweza kuwa msaada, hakuna kitu kama hicho zaidi ni kumuongezea hatari huyo mtu.

 

“Zipo namna za kutoa huduma ya kwanza kwa mtu aliyeng’atwa na nyoka na sisi OSHA tunatoa mafunzo hayo kwa gharama ya shilingi 250,000, mtu anapewa mafunzo yote ya kutoa huduma ya kwanza kwa siku tatu na tunampa cheti,” alisema.

 

Mafunzo hayo yanajumuisha utoaji wa huduma ya kwanza kwa mtu aliyekwawa na mwiba wa sabaki, kung’atwa na nyuki, nge, tandu na kugongwa na nyoka wenye sum una wasio na sumu.

 

Mkuu wa Kitengo cha Sheria OSHA, Bi. Rehema Msekwa.
OSHA NI NINI?

OSHA ni kifupisho cha maneno ya kiingereza Occopational Safety and Health Authority na wenyewe wakiyatafsiri kwa Kiswahili kama Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi.

 

Taasisi hii ilianzishwa kwa mujibu wa sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi namba 5 (tano) ya mwaka 2003 ikiwa na lengo la kuweka viwango vya usimamizi wa afya, usalama na ustawi wa hali za wafanyakazi wawapo kazini.

 

Mbali na hilo lakini pia lengo la sheria hiyo ni kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vilivyopo kwenye maeneo ya kazi vinavyoweza kuhatarisha Afya na Usalama wa Mfanyakazi pamoja na kuondoa ama kupunguza mazingira hatarishi ya kazi na kuweka adhabu kwa waajiri na wamiliki wa maeneo ya kazi wanaokiuka sheria.


Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule (aliyesimama) akifungua mafunzo ya usalama kazını kwa Wahariri.

 
Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, aliwataka Wahariri kuwa Mabalozi wa OSHA popote watakapokuwepo na kwamba watu wa kwanza wanaopaswa kuhakikisha kuna usalama na afya mahali pa kazi ni wao.

 

“Ninyi Wahariri ndio kisemeo kikubwa cha wananchi wengi, niwaombe sasa mkayatumie mafunzo haya ninyi wenyewe, lakini pia mhakikisha jamii inaujua umuhimu wa OSHA,”alisema.

 

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Hadija Mwenda.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Hadija Mwenda alisema wameiona haja ya kuwapa mafunzo hayo Wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari nchini, kutokana na nafasi kubwa waliyonayo ya kuwasiliana na jamii kwa haraka.

 

“Ninyi ni watu muhimu sana kwenye maendeleo ya nchi hii, kama mnavyojua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kuwaletea wananchi maendeleo, na sisi OSHA tunauona umuhimu huo na ndio maana tunataka kuhakikisha wafanyakazi wanakuwa salama na wenye afya njema.

 

“Naamini uwepo wenu hapa utaibua chachu na umuhimu wa watu kuijua vema OSHA na litakuwa ni kimbilio la waajiri na waajiriwa katika masuala ya afya na usalama kazini,”alisema Bi. Mwenda. 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments