Ticker

7/recent/ticker-posts

TAWA YAFURAHIA MATUNDA YA ROYAL TOUR, KILWA KISIWANI YAPOKEA WATALII KUTOKA MATAIFA 18 KWA SIKU MOJA

 

Meli ya Silver Cloud iliyobeba watalii 230 waliotembelea Kilwa Kisiwani.

NA. BEATUS MAGANJA 

 

Meli ya Silver Clouds iliyobeba takribani watalii 230 kutoka katika mataifa 18 duniani, leo Aprili 24,2024 imetia nanga kwenye Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa dunia wa Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.

 

Watalii hao wamepokewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA kwa ajili ya shughuli za utalii.

 

Watalii hao wametoka kwenye mataifa ya Australia, Ubeligiji, Brazil, Canada, Chile, China, Ujerumani, Ireland, Norway, Italia, Ureno, Afrika ya Kusini, Hispania, Sweden, Switzerland, Ukraine, Uingereza na Marekani.

 

Hatua hiyo ni mwendelezo wa safari za watalii kutoka kona mbalimbali za Dunia kuja nchini kujionea fahari ya urithi wa Dunia wa utamaduni, historia na malikale uliopo katika Hifadhi hiyo inayosimamiwa na TAWA.

 

Ikumbukwe kuwa Hifadhi hiyo imekuwa ikipata wageni wengi wa ndani na nje ya nchi yambapo hivi karibuni (Februari, 2024) Hifadhi hiyo ilipokea zaidi ya watalii wa nje 900 kutoka sehemu mbalimbali  Duniani kwa ajili ya shughuli za utalii, idadi inayotajwa kuvunja rekodi katika Hifadhi hiyo.

 

Watalii hao ambao wanaongozwa na Kampuni ya Utalii ya Takim Holidays walipokelewa na kukaribishwa kwa ngoma za asili ya watu wa Kilwa Kisiwani iitwayo kitupolo.

 

Tanzania  inaendelea kunufaika na filamu kubwa iliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Tanzania The Royal Tour ambayo imefungua milango kwa watalii wengi kuingia nchini kwa ajili ya shughuli za utalii.

Kundi la watalii kutoka mataifa 18 wakitembelea vivutio vya Utalii vilivyopo Kilwa Kisiwani


 

Post a Comment

0 Comments