Ticker

7/recent/ticker-posts

HALMASHAURI YA MSALALA KUVUKA MALENGO YA UKUSANYAJI MAPATO

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala, Khamis Katimba aliyesimama.
Na Mwandishi Wetu

Halmashauri ya Msalala imejipanga kuhakikisha inavuka malengo yake ya ukusanyaji mapato kwa mwaka wa Fedha wa 2023/24.

 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Khamis Katimba wakati wa ufunguzi wa stendi mpya ya Isaka ambapo alisema, miradi mbalimbali iliyopo kwenye Halmashauri hiyo, ndio vyanzo vikuu vya mapato ya serikali.

 

Katimba amesema, katika kipindi cha miezi tisa, halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 4.6 ikiwa ni asilimia 90 ya malengo waliyojiwekea ya kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 5.

 

Katika kipindi kilichobaki amesema, halmashauri hiyo inatarajia kufikisha asilimia 100 kwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 500.

Katimba alisema wamefanikisha hilo kutokana na ushirikiano wa watumishi wa halmashauri hiyo na mikakati iliyowekwa.

 

“Katika miezi tisa pekee tumefanikiwa kufikisha asilimia 91 (Bil 4.6) ya mapato, hii maana yake tunao uwezo wa kuvuka lengo letu la kukusanya Bil 5 kwa miezi 12,” alisema.

 

Akizungumzia ujenzi wa stendi mpya ya mabasi Isaka, Katimba alisema stendi hiyo itaongeza wigo wa uchumi kwa wananchi pamoja na mapato ya halmashauri hiyo. 

 

“Serikali inajitahidi kutekeleza malengo yake kama ilivyoahidi hivyo, wananchi nao wajitahidi katika ulipaji tozo na kodi mbalimbali za serikali.

 

“Serikali ni ya wananchi, tunapaswa kulipa tozo mbalimbali za serikali na kujiepusha na utoroshaji au ukwepaji wa kulipa kodi kwa kuwa, fedha zinazokusanywa hutumika kwa shughuli za maendeleo ya jamii ikiwemo ujenzi huu wa tendi,” alisema Katimba.

 

Kwenye ufunguzi huo, mkurugenzi huyo alisema, stendi ya Isaka ni moja ya mipango ya muda mrefu ya serikali na kwamba, ufunguzi wake utaeleta afueni pia utaongeza wigo wa uchumi kwa wananchi na serikali.

 

“Natoa wito kwa wananchi wa Halmashauri ya Msalala na maeneo jirani kuitumia stendi hii kwani uwepo wake ni moja ya sababu za ukuaji wa mji wa Isaka.

 

“Pia changamkieni viwanja kwani halmashauri imevipima karibu na stendi pembezoni mwa Barabara ya Isaka – Rwanda,” alisema.

 

Mkurugenzi huyo alisema, pamoja na mambo mengine, stendi hiyo imelenga kutoa huduma ya usafiri na usafirishaji pia halmashauri hiyo kuongeza kipato kwa ajili ya kuhudumia wananchi kwani ni chanzo cha uhakika.

 

Aliahidi kuwa, yeye na timu yake ya wataalam wataendelea na jitihada za kuhakikisha mapato yanakusanywa na kutumika kama inavyoelekezwa na serikali. 

 

Pia alisema, hadi kufika Machi 31, 2024 halmashauri hiyo tayari imekusanya asilimia 91 ya makusanyo ya Mfuko Mkuu ambayo ni sawa na 4.6 Bilioni.

 

Ofisa Mapato wa Halmashauri hiyo, Salehe Msosole alishukuru uongozi wa halmashauri kwa kuweka msisitizo utendaji uliotukuka kwa watumishi wake ambao umesaidia kuongeza mapato ya halmashauri.

 

“Ukweli ulio wazi ni kuwa, ushirikiano wa Mwenyekiti wa Halmashauri, Mibako Mabubu na mkurugenzi wetu (Katimba) pamoja na watumishi umesaidia sana halmashauri hii.

 

“…hasa kuweka kipaumbele cha kwanza katika utendaji kazi wa kila siku, jambo ambalo limesababisha usimamizi mzuri wa mapato hasa msisitizo wa kila diwani katika eneo lake huhakikisha tozo za serikali zinalipwa kama inavyotakiwa,” alisema Msosole.

 

Ofisa mapato huyo alisema, mkurugenzi wa halmashauri hiyo aliunde kikosi kazi ambacho anakisimamia.

“Mimi nasimamia kikosi hicho, tunafanya doria usiku na mchana kuhakikisha tunadhibiti utoroshaji wa mapato, tangu tuanze usimamizi huu kila siku tunakamata magari yasiyopungua manne na Bajaj mbili. 

 

“Natoa wito kwa wafanyabiashara kulipa tozo za halmashauri kwa hiari ili kujenga uchumi wa nchi yetu na kumuunga mkono Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan.

 

Mgeni rasmi katika ufunguzi wa stendi hiyo, Majuto Pazi ambaye ni Diwani wa Kata ya Isaka aliwaomba wananchi hasa wana Isaka kutumia fursa ya stemndi hiyo hiyo kujiongezea kipato.

 

Ofisa Mipango wa halamahauri hiyoi, alisema kukamilika kwa stendi hiyo, ni jitihada za pamoja za mkurugenzi mtendaji, madiwani, wataalam wa halmashauri ngazi za vijiji, kata, wenyeviti wa vijiji na wananchi wote.

 

“Namshukuru Rais Samia kwa kuleta fedha za kuwezesha kujenga stendi hii sambamba na Mbunge wa Jimbo la Msalala, Idd Kassim Idd kwa ushawishi, kusimamia na  kuhakikisha serikali na wawekezaji wanatoa fedha kwa wakati ili kutekeleza miradi ndani ya halmashauri.

 

Wananchi wanaozunguka stendi hiyo wameeleza kufurahishwa kwao na ufunguzi huo kwani, uongozi wa kijiji umetangaza kugawa maeneo ya biashara ndani ya stendi hiyo.

Post a Comment

0 Comments