Ticker

7/recent/ticker-posts

TBS YATENGA ZAIDI YA MILIONI 250 KUHUDUMIA WAJASIRIAMALI WADOGO BILA MALIPO

                                     Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athumani Ngenya.

 NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI-DSM

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetenga kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 250 zilizoelekezwa kwenye kuwahudumia wajasiriliamali wadogo bila malipo kwenye eneo la utoaji wa leseni za Alama ya Ubora.

Kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini sawa na asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2,000

 

Kati ya leseni hizo, jumla ya leseni 1,051 zilitolewa bure na kwa Wajasiriamali wadogo. 

 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athumani Ngenya alipokutana na Wahariri na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya Habari nchini.

Alisema kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya viwango 1,721 vya kitaifa viliandaliwa sawa na asilimia 101.2 ya lengo la kuandaa viwango 1,700. Viwango hivyo viliandaliwa katika nyanja mbalimbali.

Aidha TBS imeshiriki katika uandaaji wa viwango vya kibiashara vya Afrika Mashariki na Afrika nzima.

 

MAFUNZO 

Kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya wadau 5,789 kutoka mikoa mbalimbali nchini walipewa mafunzo. 

TBS imeendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo (MSEs) na wazalishaji ili kuwawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango vya ubora na usalama na hatimaye kukidhi ushindani wa masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

Ikumbukwe kuwa TBS ilianzishwa mwaka 1975 kwa juhudi za Serikali kama sehemu ya jitihada ya kuimarisha Miundombinu ya sekta ya Viwanda na Biashara ili kukuza uchumi wa Taifa. 

Baadhi ya Wahariri na Waandishi wakiwamsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa TBS, hayupo pichani.

MAJUKUMU YA TBS 

Jukumu Kuu la TBS ni kuratibu uandaaji wa viwango na kusimamia utekelezaji wake (shughuli za utayarishaji wa viwango na udhibiti wa ubora wa bidhaa zote pamoja na kusimamia usalama wa  bidhaa za chakula na vipodozi)

Majukumu ya TBS yameainishwa katika Kifungu cha 4 (1) (a) – (v) cha Sheria ya Viwango Sura Na. 130. Majukumu (functions) hayo kwa ufupi ni kama yafuatayo: -

Kutayarisha na kutangaza Viwango vya ubora vya Tanzania kwenye sekta zote za uchumi. Kipaumbele kimewekwa katika viwango vya kitaifa katika nyanja za nguo, ngozi, kilimo na chakula, madawa (kemikali), uhandisi na mazingira;

Kutekeleza viwango vya ubora vilivyotangazwa kwa kutumia mifumo mbalimbali ya udhibiti ubora kama vile ukaguzi na upimaji wa bidhaa kabla ya kusafirishwa kuja nchini, upimaji wa bidhaa kwa kuzingatia matakwa ya kiwango au ya mzalishaji na usajili wa mifumo ya ubora;

Majukumu (functions) mengine: -

Kuchukua na kupima sampuli za bidhaa zinazokusanywa na wakaguzi wa TBS, kwa lengo la kutekeleza viwango au kwa kuzingatia maombi ya mzalishaji;

Kutoa mafunzo kwa wenye viwanda na biashara juu ya uzalishaji na utoaji huduma bora kwa kuzingatia viwango; na

Kuvifanyia ugezi vipimo vya vifaa vya upimaji viwandani na vya kibiashara katika nyanja za uzito, urefu, ujazo, nishati, halijoto, n.k. 

TBS katika utekelezaji wa majukumu yake imepata mafanikio yafuatayo:

 


UJENZI WA MAABARA

Shirika linatekeleza mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Shirika na maabara (Viwango House - Dodoma). Maabara hiyo itahudumia mikoa mitatu (3) ya kanda ya Kati ambayo ni Dodoma, Singida na Tabora pamoja na mikoa mingine ya karibu. 

 

Aidha TBS inatarajia kuanza ujenzi wa maabara ya kisasa katika kanda ya Ziwa (Mwanza) na kanda ya Kaskazini (Arusha). Maabara ya kanda ya ziwa inatarajiwa kuhudumia mikoa sita (6) ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu. 

 

Maabara ya kanda ya Kaskazini inatarajiwa kuhudumia mikoa minne (4) ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara. 

 

OFISI ZA KANDA

Shirika limefanikiwa kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia ofisi za kanda saba ambazo ni Kanda ya Kaskazini (Arusha) ,Kanda ya Kusini (Mtwara) ,Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya) , Kanda ya Magharibi (Kigoma) ,Kanda ya ziwa (Mwanza) ,Kanda ya Kati (Dodoma) na Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam).

Kanda hizi zina ofisi katika mipaka, bandari pamoja na viwanja vya ndege.

 


UNUNUZI WA MASHINE

Shirika limewekeza kwenye ununuzi wa vifaa vya maabara via kisasa (state-of-the-art-equipment) kwa kutumia fedha za ndani pamoja na misaada kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo. 


ITHIBATI NA UMAHIRI

Shirika lina maabara 12 zilizopo Ubungo Dar es Salaam, maabara hizo zimehakikiwa na kupatiwa cheti cha ithibati ya umahiri wa kimataifa (accreditation). Hatua hiyo inapelekea majibu ya sampuli kutoka katika maabara hizo kuaminika kokote duniani na hivyo kurahisisha biashara.

 

HUDUMA KIDIGITALI

Shirika limetengeneza mifumo ya kielektroniki inayotumika kutoa huduma zake. Uanzishwaji wa mifumo ya kielektroniki imewezesha wateja kupata huduma za TBS popote walipo kwa wepesi na haraka hivyo kupunguza gharama kwa wateja.

 

UKAGUZI WA BIDHAA ZA NDANI

 

Shirika limeandaa utaratibu wa kukagua viwanda vyote hapa nchini ili kuhakikisha kwamba vinazalisha bidhaa zenye ubora unaotakiwa.

Kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini sawa na asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2,000.


UKAGUZI BIDHAA ZA NJE

TBS hudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje kwa kutumia mfumo wa Pre-Shipment Verification of Conformity to Standards (PVoC) pamoja na kufanya ukaguzi pindi bidhaa zinapowasili nchini (Destination Inspection).

Kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya shehena 100,851 kabla hazijaingizwa nchini sawa na asilimia 99 ya lengo la kukagua shehena 102,083. Pia, jumla ya bidhaa 151,570 kutoka nje ya nchi zilikaguliwa baada ya kufika nchini sawa na asilimia 77 ya lengo la kukagua bidhaa 197,417. 

 


KAGUZI ZA KUSHTUKIZA

TBS hufanya kaguzi za mara kwa mara sokoni na viwandani kwa ajili ya kuhakikisha bidhaa zilizopo zinakidhi matakwa ya viwango husika.

TBS pia hushirikiana na taasisi nyingine za Serikali kama TRA, FCC, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama kufanya ukaguzi ili kubaini bidhaa zisizokidhi matakwa ya viwango na kuchukua hatua stahiki. 

TBS hutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ili kukuza uelewa juu ya masuala ya viwango na udhibiti ubora. Njia hizo ni pamoja na:

Kushiriki katika makongamano, maonesho, warsha na semina;

Kuandaa mikutano na wadau wa masuala ya viwango (Stakeholder’s meeting);

Kuendesha kampeni za elimu kwa umma katika ngazi za wilaya na mashuleni;

Kutoa elimu kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii; 

Kuandaa matangazo, majarida na vipeperushi; na

Kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya ubora na usalama.

Shirika la Viwango Tanzania liko bega kwa bega na Serikali yetu tukufu katika kutekeleza azma ya kuwezesha ufanywaji wa biashara nchini utakaoendana na kuinua viwanda kwa kusimamia ubora wa bidha, kulinda usalama wa mlaji sambamba na kusimamia mapato ya Serikali. 

Hivyo, Shirika litaendelea kutekeleza majukumu yake yote kwa kuzingatia weledi na ufanisi wa hali ya juu ili kuhakikisha malengo ya nchi yanafikiwa kwa wakati uliokusudiwa. 

 

Post a Comment

0 Comments