Ticker

7/recent/ticker-posts

TAWA YATOA POLE KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO RUFIJI, YABEBA JUKUMU LA KUWAPA ELIMU YA KUEPUKA MADHARA YA MAMBA NA VIBOKO

 

Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja


NA BEATUS MAGANJA

Mafuriko yaliyoikumba wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani yameifanya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kutoa pole kwa waathirika pamoja na kutoa elimu kwa wananchi wa eneo hilo juu ya namna bora ya kuepukana na madhara yanayoweza kusababishwa na mamba au  viboko.

 

Imeelezwa kuwa katika kipindi hiki cha mafuriko ni wazi wanyama hao nao wanahaama au kuhamishwa na maji hayo, hivyo kuna haja ya kuwaandaa wananchi kuepukana na madhara kabla hayajatokea.

 

Timu ya Maofisa uelimishaji kutoka TAWA tayari imeweka kambi wilayani Rufiji ikiwa na lengo la kutoa elimu ya kuepuka madhara yatokanayo na mamba na viboko.

 

Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja ameyasema hayo jana, Aprili 15,2024  alipokuwa akiongea na waandishi wa Habari wilayani humo.

 

"TAWA tumeweka Kambi katika wilaya ya Rufiji kufuatia mafuriko yaliyojitokeza katika wilaya hii yaliyoathiri Watanzania wenzetu.

Baadhi ya Maofisa wa TAWA wakizungumza na wanafunzi, wilayani Rufiji.

 "Jambo lililotuleta hapa, kwanza ni kutoa pole kwa watanzania wenzetu ambao wamekumbwa na mafuriko haya, lakini pia tumekuja mahsusi kwa ajili  ya kutoa elimu ya namna  wananchi hawa wanaweza kuchukua tahadhari kwa madhara yanayoweza kusababishwa na mamba na viboko" ameongeza Maganja

 

Kwa upande wake Afisa uelimishaji kutoka TAWA Kanda ya Kusini Mashariki, Jimmy Mshana amesema TAWA ilianza kutoa elimu hiyo katika maeneo mbalimbali wilayani humo ikiwemo Kata ya Chemchem na vitongoji vyake vyote na jana Aprili 15, 2024 elimu hiyo imeendelea kutolewa katika Kata ya Mgomba na vijiji vyake vyote na kukiri kupata mwitikio mzuri kutoka kwa wananchi.

 

Mwenyekiti wa kijiji cha Mgomba Kusini, Kassim Ally Mtumbei ameishukuru Serikali na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa TAMISEMI ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mohamed Mchengerwa kwa msaada wao kwao.

 

Pia ameishukuru TAWA kwa kuweka kambi wilayani humo ili kutoa elimu ya kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na mamba au viboko.

 

Baahi ya akina mama wakisikiliza maelekezo ya namna ya kujiepusha na madhara yanayoweza kusababishwa na mamba na viboko, wilayani Rufiji.

Imeelezwa kuwa mafuriko katika wilaya hiyo mbali na kuharibu makazi ya watu na mali zao,  yameambatana na athari mbalimbali ikiwemo ongezeko la matukio ya wanyamapori hususani mamba na viboko ambao wametoka kwenye maeneo yao ya asili na kusogea karibu na makazi ya watu kwa kusafirishwa na mikondo ya maji.

 

Ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao, TAWA imepeleka vikosi vya doria kwa ajili ya kuwadhibiti na kutoa elimu kwa jamii ya kuchukua tahadhari kuepukana na madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao, na hii ni katika kuonesha namna ambavyo TAWA inavyothamini na kujali maisha ya binadamu


 

 

Post a Comment

0 Comments