Ticker

7/recent/ticker-posts

TAWA YATOA MSAADA WA MAGODORO NA CHAKULA KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO RUFIJI

 Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge akipokea msaada wa godoro kutoka kwa Kamishna Msaidizi mwandamizi wa TAWA, Abraham Jullu.

NA. BEATUS MAGANJA

Katika kufanikisha dhamira yake ya kushirikiana na wananchi, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) leo Aprili16,2024 imetoa misaada mbalimbali kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea wilani Rufiji, mkoani Pwani.

 

 Misaada iliyotolewa ni pamoja na tani 6.4 za unga wa sembe, kilo 666 za maharage na magodoro 186, ambapo misaada yote ina thamani ya shillingi millioni 20.

 

Misaada hiyo  imekabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge na Kamishna Msaidizi mwandamizi, Abraham Jullu kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA.

 

Jullu amesema TAWA imeguswa na janga la mafuriko lililowapata wananchi wa Rufiji ambao wamehusika kwa kiasi kikubwa kulinda rasilimali za Hifadhi ya Selous na hivyo imelazimika kuwashika mkono.

 


Amesema tangu changamoto hii ya mafuriko imejitokeza TAWA ilifika kwa haraka na kuongeza nguvu kwa kutoa kikosi cha Askari 24  ili kusaidia katika zoezi la uokozi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya mbinu za kujikinga na madhara yatokanayo na wanyamapori hususani mamba na viboko.

 

Mpaka sasa  TAWA imetoa elimu hiyo kwa wananchi wapatao 4,225 na bado inaendelea na zoezi hilo.

Aidha TAWA imetoa boti moja lenye uwezo wa kubeba jumla ya watu 15 ili kusaidia katika shughuli za uokozi zinazoendelea wilayani humo.

 

Kwa upande wake Kunenge amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka misaada mbalimbali kupitia Serikali na Chama Cha Mapinduzi tangu wilaya hiyo ipate changamoto hiyo ya mafuriko.

 

Ameshukuru Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda kwa maamuzi ya haraka waliyoyafanya ya kupeleka misaada hiyo kwa wananchi wa Rufiji kwa wakati.

 

Pia ameshukuru hatua ya TAWA kwa msaada wa boti kwa ajili ya kufanya shughuli za  uokozi na ushiriki wao wa ujumla katika zoezi la uokozi kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya dola na kukiri kuwa wananchi wa Rufiji wanaona thamani na umuhimu wa uwepo wa Taasisi hiyo mkoani Pwani.

 

Nae Mkuu wa wilaya ya Rufiji Meja  Edward Gowele, amesema TAWA imekuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri na uongozi wa wilaya yake na ndio maana imekuwa rahisi kwao kuitikia wito wa kutoa msaada kufuatia janga lililoikumba wilaya hiyo.

 

Baadhi ya maofisa wa TAWA

Post a Comment

0 Comments