Aliyetangaza kifo cha Mzee Mwinyi ni Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo akiwa na majonzi ameueleza umma wa Watanzania kuwa: Kwa majonzi makubwa nasikitika kutangaza kifo cha Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, ambaye amefariki dunia leo Ijumaa tarehe 29, Februari mwaka 2024, saa 11:30 jioni katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio mzena, Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa saratani ya mapafu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akilihutubia Taifa kupitia Vyombo mbalimbali vya Habari kuhusu kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi kilichotokea katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar es salaam alikolazwa kwa matibabu ya Saratani ya Mapafu tarehe 29 Februari 2024.
“Kwa niaba ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu mkubwa kwa Taifa letu.
Hayati Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi (kulia) alipokuwa akizungumza na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. |
“Nchi yetu itakuwa katika kipindi cha siku saba za maombolezo, ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia kesho Machi 1,2024. Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi atazikwa tarehe 2 Machi 2024 huko Unguja, kisiwani Zanzibar. Inna Lillahi wa inna ilayhi raaji’un.” Amehitimisha Rais Dkt. Samia.
Kimsingi huu ni msiba mzito kwa taifa la Tanzania, ni msiba unaomgusa mtu aliyefikia ngazi ya urais kama ilivyokuwa kwa Baba wa taifa aliyefariki dunia Oktoba 14,1999, akafuatiwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliyefariki dunia Julai 23,2020.
HAYATI ALI HASSAN MWINYI NI MTU WA PEKEE
Ali Hassan Mwinyi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 98, alizaliwa Mei 8,1925 na amefariki katika tarehe ambayo hujirudia kila baada ya miaka minne, hii inamaanisha huenda kumbukumbu ya kifo chake itakuwa inaadhimishwa kwa namna ya kipekee kila maka ama ikawa mara mbili tu katika kila kipindi cha muongo mmoja na kumbukumbu ya kwanza ya tare rasmi ya kifo chake itakuwa ni Jumanne ya Februari 29,2028.
Mzee Mwinyi aliyezaliwa Kivure, mkoani Pwani na baadae kuhamia Unguja akiwa mdogo na wazazi ndie Mtanzania pekee aliyeweza kuongoza pande zote mbili za Muungano katika nafasi ya urais.
Mwaka 1933 alianza kupata elimu ya msingi na baadae sekondari kwenye shule za Mangapwani na Dole, ambako alihitimu mwaka 1942.
Baadae aliendelea na masomo ya ualimu kwenye Chuo Kikuu cha Durham nchini Uingereza, alianza kazi akiwa mwalimu wa kawaida baadae alipanda cheo na kuwa mkuu wa chuo cha Ualimu Unguja.
Hayati Rais Mwinyi (aliyeshika tama) akiangalia Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere akicheza bao. |
Akiwa kwenye majukumu yake ya taaluma ya Elimu mwaka 1963 aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu ya Zanzibar.
Mwaka 1970 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, aliendelea kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo ya Waziri wa Afya, Waziri wa Mambo Ndani, Waziri wa Utalii na Balozi wa Tanzania nchini Misri.
Januari 1984 aliteuliwa kuwa rais wa Zanzibar baada ya mtangulizi wake Aboud Jumbe Mwinyi kulazimishwa kujiuzulu.
Akiwa katika nafasi ya Rais wa tatu wa Zanzibar pia alikuwa akishikilia wadhifa wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Maungano wa Tanzania.
Kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 1985 Mzee Mwinyi aliteuliwa na chama chake Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea kwa nafasi ya Raisi wa Muungano na alichaguliwa bila kupingwa, wakati huo nchi ilikuwa iko chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa.
Aliiongoza Tanzania kuanzia Novemba 5,1985 mpaka 1995 kisha alimuachia nchini Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa, aidha aliiongoza CCM kwa nafasi ya Mwenyekiti Taifa kwa miaka sita, kutoka 1990-1996.
Mzee Mwinyi anatambulika kama ndie kinara wa mageuzi ya uchumi huru kwa Tanzania, yeye ndie alizibadili sera za ujamaa kuwa sera za soko huria.
Alipunguza masharti magumu ya kuingiza bidhaa kutoka nje ya nchi, alitoa nafasi kwa watu binafsi kuanzisha biashara.
Sera za soko huria za Hayati Mwinyi zilieendelezwa na aliyemkabidhi nchi Hayati Mkapa na kwakuwa hakuwa mtu mwenye kujikweza mara baada ya kumaliza urais wake, aliamua kujiondoa kabisa kwenye uga wa siasa za ushindani badala yake alikuwa akishauri pale alipotakiwa kufanya hivyo.
MUUMINI WA SIASA ZA USHINDANI
Wakati wa utawala wake ni yeye ndie aliyearidhia uwapo wa siasa za vyama vingi. Mwaka 1991 Hayati Mwinyi alianzisha Tume ya Nyalali ambayo ilipendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.
Ingawa watu wengi walipingana nah atua hiyo, lakini ni serikali yake ndio iliridhia wachache wasikilizwe na hatimae mwaka 1995 nchi ilifanya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi vya kisiasa.
KAZI
Kama nilivyotangulia kuandika hapo juu alikuwa mwalimu wa shule za msingi za Mangapwani na Bumbwini, Zanzibar.
SIASA
Hayati Ali Hassan Mwinyi alijiunga na chama cha Afro Shiraz(ASP) mwaka 1964 na kushika nyadhifa mbali mbali za serekali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katibu mkuu, Wizara ya Elimu Zanzibar 1963, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1970 na kati ya mwaka 1982 hadi 1983 alikuwa Waziri wa Afya, Wizara ya Mambo ya Ndani, Maliasili na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Misri.
Mwaka 1984 alichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ELIMU
Ni muhitimu wa cheti cha umahiri wa lugha ya Kiingereza, alichokipata katika taasisi ya Regent ya Uingereza mwaka 1960 na cheti cha umahiri wa lugha ya Kiarabu alichohitimu, Cairo, Misri, mwaka 1972-74.
NISHANI
Mwaka 2011 alitunukiwa nishani ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
SHAHADA ZA HESHIMA
Mwaka 2012 Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kilimtunuku udaktari wa heshima na mwaka 2013 Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, kilimtunuku udaktari wa heshima.
0 Comments