Ticker

7/recent/ticker-posts

WAFUGAJI WAINGIZA NG’OMBE 261 HIFADHI YA BURIGI-CHATO, ASKARI WAZIKAMATA

Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Juma Kuji

MWANDISHI WETU-CHATO

Jamii ya wafugaji imeendelea kuwa miongoni mwa makundi yanayosababisha migongano baina ya binadamu na wanyamapori kutokana na mwenendo wao wa kuingiza mifugo ndani ya hifadhi.

Hivi karibuni Askari wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi -Chato wamefanikiwa kukamata ng'ombe 261  walioingizwa kwenye hifadhi hiyo kwa lengo la kutafuta malisho.

Tukio hilo la kukamatwa kwa mifugo hiyo limethibitishwa na Afisa Uhifadhi Mkuu wa ldara ya Ulinzi, Deogratius Mwageni.

Mwageni ameweka wazi kuwa Ng'ombe hao wamekamatwa wakiwa katika eneo la Kimbogo na Miringa katikati ya hifadhi hiyo.

"Tumekamata Ng'ombe 261 ndani ya hifadhi, hatua hii inatokana na mwendelezo wa operesheni zetu ambazo tunafanya ili kukabiliana na wahalifu hifadhini,"alisema. 

Imeelezwa kuwa uimarishaji wa ulinzi ndani ya hifadhi umesaidia kwa kiasi kikubwa kukamata mifugo ambayo inaingizwa hifadhini kinyume cha sheria huku  viongozi wa vijiji wakitajwa kushirikiana na wafugaji wakubwa kuingiza Mifugo hifadhini.

Kwa mujibu wa Mwanasheria na afisa wa kitengo cha uchunguzi na uendeshaji kesi katika hifadhi ya Burigi -Chato, Emmanuel Zumba amesema Mifugo hiyo iliyokamatwa itafikishwa Mahakamani.

"Tumekuwa na operesheni ya kukamata Mifugo hifadhini kuanzia Julai 2024 hadi sasa tumekamata Ng'ombe zaidi ya 1000 na tunakesi 165 na 74 zimetolewa uamuzi na tumeshinda  "amesema.

Mkuu wa hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi,Ismail Omar amesema Ulinzi wa hifadhi hiyo sasa umeimarika hali ambayo inasabisha utulivu ndani ya hifadhi unaowasaidia  Wanyamapori kuanza kuongezeka.

Mkuu wa Idara ya Ulinzi Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato, Deogratius Mwageni.

Hata hivyo Omar amekiri kuwa bado kuna changamoto ya mifugo kuingizwa hifadhini, hata hivyo wanaendelea kukabiliana nayo.

Alipoulizwa kama mifugo hiyo inayoingizwa hifadhini ni ya wafugaji wa ndani ya nchi ama wanatoka nchi jirani, Omari alikiri kuwa mifugo mingi ni  kutoka nchi jirani na wahusika wamekuwa wakipata usaidizi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa vijiji wasio waadilifu .

"Tuna vijiji 38 vinavyozunguka hifadhi, sasa baadhi ya maeneo kuna viongozi wanapokea wafugaji kutoka nchi jirani na kuingiza Mifugo hifadhini hasa katika maeneo ya milima na mabonde,"amesema

Hata hivyo, amesema kutokana na matumizi ya Teknolojia za kisasa katika Ulinzi Mifugo imekuwa ikikamatwa na kufikishwa Mahakamani.

"Tunaomba viongozi wachache wa vijiji waache kuhujumu hifadhi na wajuwe lazima tutawakamata wao na mifugo iliyoingizwa hifadhini"amesema.

Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Juma Kuji akizungumza na waandishi wa habari za Utalii amesema TANAPA imejipanga kukomesha matukio ya ujangili na uvamizi wa Mifugo hifadhini. 

"Tumeanza kutumia Tecknolojia za kisasa kabisa kulinda hifadhi kwa  kutumia ndege zisizo na rubani  na nyingine za kawaida, lakini pia tunaongeza doria katika hifadhi ili kuhakikisha wahalifu wanakamatwa."amesema

Kamishna Kuji ametoa wito kwa Wananchi kuacha mara moja tabia za kuingia hifadhini na kufanya uhalifu ikiwepo kuingiza mifugo kwani lazima watakamatwa .



Post a Comment

0 Comments