Ticker

7/recent/ticker-posts

‘JAMII ISIKWEPE WAJIBU KUWAHUDUMIA WENYE ULEMAVU’

Makamu wa Askofu,  Jimbo katoliki  la Morogoro, Padre Silvanus Kwembe

 NA VICTOR MAKINDA:MVOMERO, MOROGORO

Wito umetolewa kwa jamii kote nchini kutokwepa wajibu wa kuwahudumia watu wanaoishi na ulemavu sambamba na kuhakikisha kuwa kundi  linapata mahitaji mbali mbali ya msingi ikiwa ni pamoja na elimu na ujuzi utakao wawezesha kujimudu wenyewe.

Wito huo umetolewa na  Makamu wa Askofu,  Jimbo katoliki  la Morogoro, Padre Silvanus Kwembe, wakati alipokuwa akizungumza kwenye tamasha maalumu la kutoa hamasa kwa jamii kujali mahitaji ya watu wenye ulemavu linalojukana kama tamasha la la Usiku wa Mwangaza lililofanyika kijijini Mvomero wilayani Mvomero mkoani Morogoro jana.

Padre Kwembe alisema kuwa jamii kwa ujumla haipaswi kukwepa jukumu la kuwahudumiwa watu wenye ulemavu na kuuacha mzigo huo kwa wazazi pekee bali inatakiwa kila mmoja ajione kuwa anao wajibu wa msingi wa kuwahudumia watu wenye ulemavu sambamba na kuwapenda na kuwajali.

“ Kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kutoa mchango wake kuwahudumia watu wenye mahitaji maalum kwa kuwa ustawi wa kundi hilo unategemea upendo wetu na namna tunavyojitoa kwao kuwasaidia kupata mahitaji muhimu ka ajili ya ustawi wao”. Alisema.

 Aliongeza kusema kuwa watu wanaoishi na ulemavu wanakumbana  na changamoto nyingi, ikiwemo kukosa elimu, huduma duni za afya, chakula na maradhi huku baadhi yao wakiwa wanyanyapaliwa hata na ndugu wa karibu.

 “Hakuna ibada njema zaidi ya  kuwajali wahitaji. Watu wenye ulemavu wameumbwa kwa  sura na mfano wa Mungu. Waumini wa dini zote na madhehebu yote, kwa pamoja tunapaswa kuishi kwa kujaliana na kusaidia, kipekee kuwasaidia wenzetu ambao maumbile yao yana mapungufu kwa kugawana nao kile tulichojaaliwa kukipata ili nao wafurahie maisha.” Alisema Padre Kwembe.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye tamasha hilo la Usiku wa Mwangaza, wazazi wenye watoto wanaoishi na ulemavu walisema kuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi kwenye malezi ya watoto hao hususani watoto wenye ulemavu wa viungo na akili,  ikiwemo ukosefu wa  huduma za afya sambamba na huduma maalumu  za mazoezi kwa ajili ya urekebishaji wa viungo.

“ Sisi tunaoishi vijijini tunaiomba serikali ituletee huduma za mazoezi kwa watoto wetu wenye ulemavu kwani hospitali ambazo zinatoa huduma hizo zipo mbali sana.”  Anaeleza Jakline Paulo mmoja ya wazazi mwenye mtoto anayeishi na ulemavu.

Baadhi ya watoto wenye ulemabu wanaolelewa na EMFERD

Anaongeza kusema kuwa  sambamba na changamoto ya kukosa huduma za mazoezi kwa ajili ya mtoto wake pia anakabiliwa na umaskini mkubwa wa kipato kwa kuwa muda mwingi anautumia kumlea mtoto huyo na kukosa muda wa kwenda shamba kulima na kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali.

Akizungumza wakati wa tamasha hilo, muasisi wa taasisi ya EMFERD, taasis inayoshughulika na kulea watoto wenye ulemavu wa akili na viungo, Josephine Bakhita, ambayo ndiyo iliyoandaa tamasha hilo la Usiku wa Mwangaza kwa kushirikiana na Parokia katoliki ya Mtakatifu Aloyce Gonzaga Mvomero, alisema kuwa pamoja na mambo mengine taasisi yake inasadia watoto wanaoishi na ulemavu  kwa kuwapa huduma ya elimu na mazoezi kwenye vituo vyake na nyumbani. 

Taasisi ya EMFERD kwa kuzingatia  umuhimu wa huduma ya mazoezi kwa watoto waliozaliwa na ulemavu pamoja na huduma nyingine, tunatoa huduma za mazoezi ambapo mtaalamu wetu huwatembelea majumbani kwenye vijijiji vilivyo pembezoni  na kuwapatia huduma hiyo muhimu ya urekebishaji.”

 Bakhita anaongeza kusema kuwa uhaba wa wataalam wa huduma hiyo sambamba na ufinyu wa rasilimali fedha  unaikwamisha taasisi yake kulifikia kundi kubwa la wahitaji.

 “ Wahitaji ni wengi, watoa huduma ni wachache hivyo, tunaomba  serikali, watu binafsi na  taasisi mbali  mbali kushirikiana na taasisi ya EMFERD   kuhakikisha kuwa huduma ya mazoezi kwa watoto wanaoishi  na ulemavu wa viungo na akili inatolewa ili kuwawezesha watoto hao kujimudu wenyewe na kupunguza mzigo mkubwa wa malezi kwa wazazi wao” Anasema Josehine Bakhita.

                                           

 

Post a Comment

0 Comments