Ticker

7/recent/ticker-posts

WANANCHI WAENDELEA KUONDOKA KWA HIYARI NDANI YA HIFADHI YA NGORONGORO

Wananchi ambao wengi wao ni wafugaji wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wanaendelea na utaratibu wa kuondoka kwa hiyari kwenye hifadhi hiyo na kuhamia Msomera Wilaya ya Handeni, mkoanii Tanga. 

Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, jana Januari 5,2024 kundi la pili la wananchi hao lilitarajiwa kuhamia kwenye kijiji cha Msomera na  kwamba taratibu za kujiandikisha zinaendelea kwa wale wote wenye utayari.

Ikumbukwe kuwa Serikali ndio imebeba jukumu la kuwahamisha wananchi hao walio kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kwa hiyari  na  kundi la kwanza lililohusisha kaya 551 likiwa na watu 3,010 na mifugo 25,521 lilishahama kwenye kijiji hicho ambacho kimeboreshwa kwa kuwekwa huduma zote muhimu za kijamii.

Mobhare alisema kwa wale watakaohamia maeneo mengine mbali na Msomera, serikali itawapa Sh. milioni 15 badala ya Sh milioni 10 wanazopewa wanaohamia Msomera. 

Wananchi hao pia wanapewa mahindi gunia mbili kwa kila miezi mitatu kwa muda wa miezi 18 kwa kaya, awamu ya pili ya wananchi hao wanaohama kwa hiyari inahusisha kaya 30 zenye watu 224 na mifugo 393. 

 “Tunaendelea na utaratibu huu kwa sababu tayari kuna wananchi 500 waliojiandikisha kutaka kuhama kwa hiyari na 400 tayari washafanyiwa tathmini ya mali zao zilizoko Ngorongoro kwa ajili ya malipo,” alisema Matinyi. 

Post a Comment

0 Comments