Ticker

7/recent/ticker-posts

MRADI WA UMEME WA RUSUMO WAKAMILIKA KWA ZADI YA ASILIMIA 99

Mradi wa maporomoko ya umeme wa Rusumo wa megawati 80 unaotekelezwa kwa pamoja na nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi umefikia asilimia 99.9 na nchi hizo tayari zimeanza kupata umeme kutoka kwenye mradi huo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto  Biteko leo Desemba 18,2023 jijini Mwanza alipokuwa akiongoza kikao cha ngazi ya Mawaziri wa Nishati ambaye yeye ni Mwenyekiti wa Mawaziri wanaosimamia mradi huo kutoka nchi  Tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi.

"Tumeridhishwa na maendeleo mazuri ya mradi mpaka sasa, tunawapongeza Bodi na Watendaji kutoka kampuni ya umeme ya Rusumo na wakandarasi kwa usimamizi na utekelezaji wa mradi huu," amesema Dkt. Biteko


Dkt. Biteko amesema  Mawaziri hao wamekubaliana kuwa, mradi huo uzinduliwe mwezi Machi mwaka 2024 hivyo wamemtaka mkandarasi kukamilisha  mradi huo mapema na atoe cheti cha kukamilisha mradi. Amesema uzinduzi huo utafanyika katika eneo la mradi huku mwenyeji wa shughuli hiyo akiwa ni Tanzania.

Amesema kuwa, mradi huo una umuhimu kwa nchi zote tatu kwani bado nchi hizo zina changamoto ya upatikanaji wa uhakika wa umeme hivyo kukamilika kwa mradi huo kutapunguza changamoto hizo na kuongeza uimara kwenye gridi.

Dkt. Biteko amewashukuru Rais wa Tanzania, Mhe.  Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye na Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame kwa msukumo wanaotoa katika utekelezaji wa mradi huo ambao umepelekea kufikia asilimia 99.9.

Vilevile, Dkt. Biteko ameshukuru wadau mbalimbali waliopelekea  mradi huo kutekelezwa ikiwemo Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo Afrika ( AfDB) na amewakaribisha kuwekeza kwenye miradi mingine ya uzalishaji umeme inayotarajiwa kutekelezwa nchini.


Kutoka Rwanda kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Miundombinu, Dkt. Jimmy Gasore (ambaye alishiriki kwa njia ya mtandao) na kutoka Tanzania, viongozi waliohudhuria ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga ambaye ni Mwenyekiti  wa Bodi ya Kampuni ya Umeme ya Rusumo.

Mradi wa umeme wa Rusumo utazalisha megawati 80 ambapo kila nchi itapata megawati 27 za umeme.

Post a Comment

0 Comments