Ticker

7/recent/ticker-posts

TANZANIA INA FURSA YA KUWA KITOVU CHA USALAMA WA CHAKULA DUNIANI

 

NA. JIMMY KIANGO

Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani katika uzalishaji wa chakula, kutokana na ardhi yenye rutuba, hali mbalimbali za hewa, vyanzo vya maji na nguvu kazi inayotegemea kilimo.

Kwa sasa, nchi inazalisha chakula kinachokidhi mahitaji ya ndani na kuwezesha kuuza ziada katika masoko ya Afrika Mashariki, Kusini mwa Jangwa la Sahara na maeneo mengine ya dunia.

Hata hivyo, uwezo huo bado haujatumika kikamilifu. Changamoto za tija ndogo kwa baadhi ya mazao, mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa chakula baada ya mavuno na uhaba wa miundombinu ya uhifadhi zinaendelea kuzuia Tanzania kufikia nafasi yake halisi katika biashara ya chakula duniani.

KIASI CHA CHAKULA KINACHOZALISHWA TANZANIA 

Kwa mujibu wa ripoti kutoka Wizara ya Kilimo, Tanzania ilizalisha takribani tani milioni 22.8 za chakula katika msimu wa 2023/2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 11.8 kutoka msimu uliotangulia.

Uzalishaji huo ulijumuisha nafaka na mazao yasiyo nafaka. Ripoti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2023/2024 inaonesha kuwa uzalishaji wa nafaka ulifikia tani milioni 14.59, ukiwa na mchanganyiko wa mazao muhimu kama mahindi, mpunga, mtama, uwele na ngano.

Katika msimu huo, Tanzania ilizalisha Mahindi tani milioni 10.08, Mpunga tani milioni 3.05, Mtama na uwele tani milioni 1.34 na Ngano tani 118,521.

Kwa jumla, uzalishaji wa nafaka ulizidi mahitaji ya kitaifa kwa takribani tani milioni 2.89. Hata hivyo, uzalishaji wa ngano na baadhi ya mazao mengine bado haukutosheleza mahitaji ya ndani.

Katika msimu wa mwaka 2024/2025, takwimu za Wizara ya Kilimo zinaonesha uzalishaji wa mazao ya chakula uliongezeka hadi tani milioni 23.78, huku kiwango cha utoshelevu wa chakula kikifikia asilimia 130.

Hii ina maana kuwa uzalishaji ulikuwa takribani asilimia 30 zaidi ya mahitaji yaliyokadiriwa kwa kipindi husika.


UWEZO WA KUZALISHA MATUNDA NA MBOGAMBOGA

Tanzania pia ni mzalishaji muhimu wa matunda na mbogamboga, mazao ambayo yana nafasi kubwa katika lishe, biashara na ajira.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kilimo, katika mwaka wa 2023/2024 Tanzania ilizalisha Matunda tani milioni 6.21, Mbogamboga tani milioni 1.23 na Viungo tani 68,436.

Jumla ya uzalishaji wa mazao ya bustani ulifikia takribani tani milioni 7.52. Matunda yanayozalishwa ni pamoja na maembe, parachichi, ndizi, machungwa na mananasi, huku mbogamboga zikijumuisha nyanya, vitunguu na mazao mengine.

Takwimu hizi zinaonesha kuwa Tanzania si nchi ya nafaka pekee, bali pia ina uwezo wa kuimarisha uzalishaji wa chakula chenye virutubisho na kuongeza nafasi katika masoko ya kimataifa.

UWEZO WA TANZANIA KIMATAIFA

Uwezo wa Tanzania kuuza chakula nje unaonekana katika biashara ya nafaka.

Kwa mujibu wa takwimu za UN Comtrade zilizochapishwa kupitia World Integrated Trade Solution (WITS), mwaka 2024 Tanzania iliuza nje takribani tani 396,891 za mchele, zenye thamani ya dola za Marekani milioni 200.8.

Masoko makuu yalikuwa Uganda tani 284,381, Kenya tani 46,114, Rwanda tani 51,340,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) tani 4,549 na Zambia tani 2,718.

Uganda, Kenya na Rwanda zilikuwa miongoni mwa masoko muhimu zaidi ya mchele wa Tanzania.

Kwa mahindi, takwimu za biashara za mwaka 2025 zinaonesha Tanzania iliuza nje tani 640,436, zikienda Kenya, Zambia, Malawi, Rwanda, Uganda na Burundi.

Hii inaonesha umuhimu wa Tanzania katika usalama wa chakula wa Afrika Mashariki na nchi jirani za kusini mwa Afrika. Pia, Tanzania ina nafasi ya kupanua biashara ya chakula kwa nchi za DRC, Sudan Kusini na masoko mengine ya Afrika.


TANZANIA AFRIKA NA DUNIANI

Tanzania ina nafasi ya kuimarisha mchango wake katika usalama wa chakula wa Afrika, hasa katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao unakabiliwa na changamoto za uzalishaji, mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji wa chakula.

Hata hivyo, kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula duniani hakupimwi kwa kiasi cha uzalishaji pekee. Inahitaji kuangalia uzalishaji kwa kila hekta, gharama za uzalishaji, ubora, uwezo wa kuuza nje, uhifadhi na upatikanaji wa chakula kwa wananchi.

Kwa maana hii, Tanzania inaweza kuwa miongoni mwa nchi zinazochangia zaidi usalama wa chakula duniani ikiwa itaongeza tija, kuimarisha usindikaji na kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya kilimo.


DIRA 2025/50 TANZANIA KUWA MIONGONI MWA NCHI 10 BORA DUNIANI

Katika Dira yab 2025/50, Tanzania imeweka lengo la kuwa miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza duniani kwa uzalishaji wa chakula, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uchumi, kuongeza ajira na kuhakikisha usalama wa chakula kwa wananchi, kupitia uwekezaji katika sekta ya kilimo.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema azma hiyo imeainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2050, inayolenga pia kuifanya nchi kuwa mzalishaji mkuu wa chakula barani Afrika.

Akizungumza Oktoba 22, 2026, jijini Des Moines, Iowa, Marekani, wakati akiwasilisha mada kuu kuhusu mustakabali wa kilimo barani Afrika katika Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue), Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea kukipa kilimo kipaumbele kutokana na mchango wake katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa.

Amesema chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi shilingi trilioni 1.241 mwaka 2025/2026.

Matokeo ya uwekezaji huo yanaonekana katika kiwango cha utoshelevu wa chakula nchini, ambacho kimefikia asilimia 130, hali inayoiwezesha Tanzania kukidhi mahitaji yake na kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya kikanda na kimataifa.

Aidha, mauzo ya nje ya mazao ya kilimo yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 2.1 mwaka 2021/2022 hadi dola bilioni 3.7 mwaka 2024/2025.

Dkt. Mwigulu anaeleza kuwa kilimo ni moja ya nguzo kuu za uchumi wa Tanzania, kikichangia asilimia 24.6 ya Pato la Taifa, kuajiri asilimia 65 ya nguvu kazi na kuzalisha takriban asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje.


TANZANIA INAWEZA KUWA KINARA WA KILIMO ENDELEVU

Ili kufikia lengo la kuwa kinara wa Kilimo endelevu Tanzania, Serikali na sekta binafsi zinapaswa kuwekeza zaidi katika umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa mvua.

Tanzania ina vyanzo vingi vya maji, lakini matumizi yake katika kilimo bado hayajafikia kiwango kinachohitajika.

Matumizi ya mbegu bora, mbolea sahihi, teknolojia za kisasa na huduma za maafisa ugani yanapaswa kuimarishwa.

Vijana na wanawake wanahitaji mikopo, ardhi, teknolojia na mafunzo ili kushiriki kikamilifu katika kilimo biashara.

Nchi inahitaji kuwekeza katika maghala, viwanda vya usindikaji, barabara za vijijini na mifumo ya usafirishaji.

Hii itasaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na kuongeza thamani ya bidhaa kabla ya kuuzwa.

Kilimo endelevu kinapaswa kuzingatia afya ya udongo, matumizi bora ya maji, kilimo mseto, agroecology na matumizi salama ya viuatilifu.

Uzalishaji mkubwa usiozingatia mazingira unaweza kuharibu msingi wa uzalishaji wa chakula wa vizazi vijavyo.

Tanzania inapaswa kuimarisha viwango vya ubora, usalama wa chakula na mifumo ya kufuatilia mazao ili kukidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa.


AGCOT: TANZANIA INA NAFASI YA KUILISHA DUNIA

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya kituo cha uendelezaji wa Kilimo Tanzania (AGCOT) John Banga akiwa mkoani Morogoro kwenye mafunzo ya siku tatu ya masuala endelevu ya mazingira yaliyoandaliwa na WWF, aliiambia AFRINEWSSWAHILI kuwa Tanzania ina mchango wa asilimia ya asilimia 65 ya ardhi inayofaa kwa kilimo barani Afrika.

Banga amesema: Asilimia 60 hadi 65 ya ardhi inayofaa kwa kilimo duniani inapatikana katika bara la Afrika hususan ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako ndiko inapopatikana asilimia 65 ya ardhi yenye uwezo wa kuzalisha chakula kwa ajili ya vizazi vijavyo takribani miaka 50 mpaka 100 ijayo.

“Katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania peke yake tuna mchango wa asilimia 7 ya ardhi yenye uwezo wa kuzalisha chakula, tukumbuke sasa hivi Tanzania ina hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo na kati ya hekta milioni 20-28 ndio zimeanza kulimwa limwa kidogo.

“Hii ina maana, zaidi ya nusu ya eneo letu linalofaa kwa kilimo halijaguswa na katika eneo hilo la hekta milioni 28 lilioanza kulimwa, eneo lililoendelezwa kwa kilimo cha kisasa ni chini ya asilimia moja.

“Pamoja na uwezo tulio nao sasa wa kulisha Afrika Mashariki na sisi wenyewe kujilisha na ziada kulisha ukanda wa Afrika Mashariki na kati ukweli ni kwamba tumetumia chini ya nusu ya ardhi tuliyo nayo.

FURSA YA KUKUZA UCHUMI KWA KILIMO IPO

Banga anaweka wazi kuwa bado Tanzania tunayo fursa ya kukuza uchumi wetu kwa kutumia sekta ya kilimo kwa miaka mingi ijayo.

“Takwimu zinaonesha kuwa Watanzania tuko takribani milioni 67 kwa sasa na tunaweza kufikia milioni 130 miaka 50 ijayo na pengine mwaka 2100 tukafukia takribani watu milioni 200 na sehemu kubwa ya watu wetu ni vijana wa chini ya miaka 24, hii inamanisha kuwa kundi hili la vijana ndilo litakaloweza kutumia fursa ya ardhi iliyopo vizuri au vibaya.

“Mimi naamini wataitumia fursa hiyo vizuri katika kuwekeza katika kilimo cha kisasa na endelevu ili tuweze kuwa na uchumi endelevu.”

WITO KWA WAKULIMA WA SASA

Banga amewakumbusha wakulima wa sasa kuzingatia kilimo endelevu ili hilo ongezeko la watu la kufikia milioni 130 au milioni 200 liweze kuikuta ardhi yetu ikiwa katika hali ya usalama na uhai mzuri ili waweze kuzalisha chakula kama tunavyozalisha sasa hivi.

“Hili ni moja ya mambo muhimu tuliyojifunza kwenye semina yetu ya siku tatu tuliyoifanya Morogoro, lengo lilikuwa ni kuangalia ni kwa kiasi gani kilimo endelevu kinaweza kunufaisha kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

AGCOT NI NINI?

Ni kirefu cha neon: Agricultural Growth Corridor of Tanzania ambao ni mpango au mradi wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi (Public-Private Partnership - PPP) uliozinduliwa rasmi mwaka 2010 kwa jina la SAGCOT katika Mkutano wa Jukwaa la Kiuchumi Duniani (WEF) kuhusu Afrika uliofanyika Dar es Salaam.

Malengo Makuu ya AGCOT ni kuendeleza Kilimo cha Biashara, kubadilisha kilimo cha asili na kwenda kwenye kilimo cha kisasa, chenye tija na cha kibiashara Tanzania.

Kuwawezesha Wakulima Wadogo, kuwasaidia wakulima wadogo kuunganishwa na masoko makubwa na ya kimataifa ili kuongeza kipato chao.

Usalama wa Chakula na Kupunguza Umaskini: Kuongeza uzalishaji wa chakula (ambapo kwa wakati huo ilitazamwa kuwa ukanda wa kusini huchangia kiasi kikubwa cha chakula nchini) na kupunguza umaskini vijijini.

Uwekezaji Kwenye Miundombinu: Kuboresha miundombinu kama barabara, reli, na usambazaji wa maji (umwagiliaji) ili kurahisisha usafirishaji wa mazao.

Utunzaji wa Mazingira: Kuhakikisha shughuli za kilimo zinafanyika kwa kuzingatia uendelevu wa mazingira.


MAENEO YA KIMKAKATI

AGCOT inazingatia hasa uendelezaji wa minyororo ya thamani ya mazao mbalimbali ya kimkakati, ikiwemo Chai, Soya, Nyanya, Viazi NA Mazao ya maziwa (Dairy)

Kimsingi Tanzania ina uwezo wa kuwa kitovu cha uzalishaji na biashara ya chakula Afrika Mashariki, Kusini mwa Jangwa la Sahara na duniani. Takwimu za uzalishaji na mauzo ya nje zinaonesha kuwa msingi wa mafanikio hayo tayari upo.

Changamoto iliyobaki ni kubadilisha uwezo huo kuwa tija kubwa, mapato ya wakulima, ajira kwa vijana na chakula bora kwa wananchi.

Kwa kuwekeza katika sayansi, teknolojia, miundombinu, masoko na kilimo endelevu, Tanzania inaweza kutimiza azma ya kuwa miongoni mwa nchi 10 bora duniani kwa uzalishaji wa chakula na kuwa mchangiaji muhimu wa usalama wa chakula duniani.

Post a Comment

0 Comments