NA JIMMY KIANGO-MOROGORO
Ushirikiano kati ya Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF) Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), na asasi za kiraia waibua fursa mpya za kuimarisha uandishi wa habari endelevu za mazingira, uwekezaji rafiki kwa mazingira na uchumi wa buluu.
Fikiria mkulima anayelima kandokando ya Mto Ruvu, mvuvi anayevua katika Bahari ya Hindi na mfanyabiashara anayeendesha kiwanda cha uzalishaji kemikali za sumu na kutiririsha maji mtoni. Ingawa watu hawa shughuli zao zinaonekana kuwa tofauti, lakini wote wanategemea kitu kimoja, mazingira salama na rasilimali za asili zinazosimamiwa kwa uendelevu.
Lakini je, jamii inaelewa kwa kiasi gani namna uamuzi wa uwekezaji, sera za biashara na matumizi ya rasilimali za asili yanavyoathiri maisha yake ya kila siku. Na je, taarifa hizo zinafikishwaje kwa umma kwa lugha rahisi, yenye ushahidi na inayochochea uwajibikaji!
Maswali hayo ni sehemu ya mjadala mpana ulioandaliwa na WWF na kuwakutisha wataalamu wa Sekta ya Habari, Mashirika ya Kiraia (CSOs) na Sekta binafsi mjini Morogoro, katika mafunzo ya siku tatu (Oktoba 28-30,2026) yaliyolenga kujenga uelewa kuhusu uendelevu, misingi ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG), uchumi wa kijani na uchumi wa buluu.
Mafunzo hayo hayakuwa tu darasa la kujifunza dhana mpya za maendeleo endelevu, bali pia ni mwendelezo wa jukwaa la kuzikutanisha sekta ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikifanya kazi katika maeneo yanayofanana, lakini wakati mwingine bila mawasiliano na ushirikiano wa kutosha.
Kwa misimu minne sasa kiini cha mafunzo hayo kimekuwa wazi, maendeleo endelevu hayawezi kujengwa na sekta moja pekee. Yanahitaji uwekezaji wenye uwajibikaji, jamii inayoshiriki katika kuamua, asasi zinazofuatilia uwajibikaji na wanahabari wenye uwezo wa kuibua mijadala inayotokana na ushahidi.
Mabadiliko ya tabianchi yabeba ajenda ya uendelevu
Umuhimu wa ushirikiano huo unaonekana zaidi tunapotazama takwimu za athari za mabadiliko ya tabianchi nchini Tanzania.
Ripoti ya Benki ya Dunia ya ‘Tanzania Country Climate and Development Report’, iliyochapishwa Desemba 2024, inaonya kuwa iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa, mabadiliko ya tabianchi yanaweza kupunguza ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa hadi asilimia nne ifikapo mwaka 2050.
Ripoti hiyo pia inakadiria kuwa watu milioni 2.6 zaidi wanaweza kuingia katika umaskini, huku hadi watu milioni 13 wakalazimika kuhama maeneo yao ndani ya nchi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa mabadiliko ya tabianchi si suala la misitu, bahari au wanyamapori pekee. Ni suala linalogusa uzalishaji wa chakula, ajira, biashara, afya, miundombinu na kipato cha kaya.
Kwa mfano, mvua zisizotabirika zinaweza kuathiri uzalishaji wa mazao ya mkulima, wakati mafuriko yanaweza kuharibu barabara, madaraja na miundombinu ya biashara. Kwa jamii za pwani, mabadiliko ya mifumo ya bahari na uharibifu wa mifumo ikolojia ya baharini vinaweza kuathiri shughuli za uvuvi na utalii.
Hapa ndipo dhana ya fedha za kijani na buluu inapopata umuhimu mkubwa. Fedha za kijani (Green Finance) zinahusisha kuelekeza mitaji katika shughuli na miradi inayochangia kulinda mazingira, kupunguza uchafuzi, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi bioanuwai.
Kwa upande mwingine, fedha za buluu (Blue Finance) zinaangazia uwekezaji unaosaidia matumizi endelevu ya rasilimali za maji na bahari, ikiwemo uvuvi endelevu, uhifadhi wa mifumo ikolojia ya baharini na miundombinu inayosaidia uchumi wa buluu.
Kwa mfano, badala ya kuwekeza katika shughuli za uvuvi zinazochochea uharibifu wa mazingira ya baharini, fedha zinaweza kuelekezwa katika teknolojia za uvuvi endelevu, ufugaji wa viumbe vya majini na mifumo ya kuongeza thamani ya mazao ya baharini bila kuharibu rasilimali hizo.
Kwa mujibu wa Tathmini ya Hiari ya Taifa ya Tanzania iliyotolewa na Wizara ya Fedha kuhusu utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (VNR) ya mwaka 2023, sekta ya uvuvi ilichangia wastani wa asilimia 1.8 ya Pato la Taifa katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2021, huku ikichangia takribani asilimia 9.9 ya mauzo ya nje ya nchi.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa bahari na rasilimali za maji si urithi wa mazingira pekee, bali pia ni msingi wa uchumi, biashara na maisha ya mamilioni ya watu.
Hii ni dhana inayohimiza taasisi na kampuni kutathmini shughuli zao kwa kuzingatia athari zake kwa mazingira, wafanyakazi, jamii na namna zinavyoendeshwa.
Kwa mfano, kampuni ya uzalishaji inaweza kuwa na faida kubwa, lakini endapo inamwaga maji taka kwenye mto unaotegemewa na jamii, inakiuka misingi ya uwajibikaji wa kimazingira.
Vilevile, kampuni inayotumia nguvu kazi bila kuzingatia usalama wa wafanyakazi, haki zao na mazingira bora ya kazi inaweza kuwa na changamoto katika kipengele cha kijamii.
Katika eneo la utawala bora, uwazi wa taarifa za kampuni, mifumo ya kudhibiti rushwa, uwajibikaji wa viongozi na usimamizi wa hatari ni mambo yanayozingatiwa.
Tume ya Ulaya inaeleza kuwa kuingiza masuala ya mazingira, jamii na utawala katika uamuzi wa uwekezaji kunasaidia kuelekeza mitaji katika shughuli endelevu za muda mrefu.
Kwa mantiki hiyo, ESG inatoa fursa kwa wawekezaji, taasisi za fedha na kampuni kuangalia zaidi ya faida ya kifedha na kutathmini thamani ya shughuli zao kwa jamii na mazingira.
Hata hivyo, suala muhimu ni kuhakikisha kuwa taarifa za kampuni kuhusu uendelevu zina ushahidi unaoweza kuthibitishwa, badala ya kutumia kauli nzuri za kutangaza mafanikio yasiyothibitishwa, jambo linaloweza kujenga taswira ya uongo ya utunzaji wa mazingira (greenwashing).
Wanahabari wanatarajiwa kwenda zaidi ya kuripoti mikutano na kutangaza taarifa za taasisi. Wanapaswa kuchunguza nani anafaidika na uwekezaji unaoitwa wa kijani, fedha hizo zinakwenda wapi, jamii inashirikishwa kwa kiwango gani na matokeo yake yanapimwaje.
Kwa mfano, habari kuhusu ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha nishati jadidifu inaweza kuwa na maana zaidi kwa jamii endapo itaeleza idadi ya ajira zinazotarajiwa, gharama za uwekezaji, athari kwa mazingira, manufaa kwa wananchi na namna mradi utakavyowajibika kwa jamii inayouzunguka.
Huo ndio umuhimu wa uandishi wa habari unaotumia takwimu, tafiti, ushahidi wa kisayansi na sauti za wananchi.
Akizungumzia uzoefu wake katika mafunzo hayo, Silvia Farae, mwakilishi kutoka sekta binafsi, alisema mafunzo hayo yamemfungua macho kuhusu namna vyombo vya habari vinavyofanya kazi na jinsi vinavyoweza kutumika kufikisha ujumbe wa uendelevu kwa watu wengi zaidi.
"Kwa kweli mafunzo haya yamenifungua macho kuhusu namna vyombo vya habari vinavyofanya kazi na jinsi tunavyoweza kuvitumia vizuri zaidi kuwasilisha masuala ya fedha za kijani na uendelevu.
“Sasa nina uelewa mzuri zaidi wa namna ya kushirikiana na wanahabari na kufikisha ujumbe wetu kwa njia zinazoweza kuwafikia watu wengi zaidi. Natarajia kutumia maarifa haya katika kazi zangu," alisema.
Kauli yake inaonesha umuhimu wa kujenga uhusiano wa kitaaluma kati ya kampuni na wanahabari, ili taarifa kuhusu uwekezaji endelevu zisibaki ndani ya taasisi husika, bali ziwafikie wananchi na kuwasaidia kuelewa mabadiliko yanayoendelea katika uchumi na mazingira.
Ushirikiano ni msingi wa mabadiliko
Kwa upande wake,Msimamizi wa Utekelezaji wa Mradi kutoka WWF, Happy Minja, alisema kuzikutanisha sekta hizo ni hatua muhimu katika kujenga uelewa wa pamoja na kuweka msingi wa ushirikiano wenye matokeo.
"Wanahabari, mashirika ya kiraia na sekta binafsi wanapokutana, wanapata fursa ya kuelewa majukumu ya kila mmoja na kubaini maeneo wanayoweza kushirikiana. Ushirikiano imara unaweza kuongeza uelewa wa umma, kuhimiza uwekezaji wenye uwajibikaji na kuhakikisha masuala ya uendelevu yanapata uzito unaostahili.
Nimefurahishwa na matokeo ya mafunzo haya na sasa tuko tayari kupeleka ushirikiano huu katika hatua nyingine ya ushirikishwaji," alisema Minja.
Kauli hiyo inaakisi ukweli kwamba kila sekta ina nafasi yake katika kujenga maendeleo endelevu.
Mashirika ya kiraia yanaweza kuunganisha jamii na watunga sera, kufanya utetezi wa masuala ya mazingira na kufuatilia utekelezaji wa ahadi za taasisi na kampuni. Sekta binafsi inaweza kutoa mitaji, teknolojia na ubunifu, huku wanahabari wakihakikisha taarifa kuhusu shughuli hizo zinawafikia wananchi kwa uwazi na usahihi.
Felister Peter, Mwandishi wa habari za Mazingira kutoka The Guardian amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wanachama wa JET na yatasaidia kuongeza ubora katika kuripoti habari za mazingira endelevu.
Kwa upande wake Allan Mgaza mmoja wa watoa mada kwenye mafunzo hayo, aliweka wazi kuwa amefurahishwa na namna darasa lilivyokuwa shirikishi. “Niwe mkweli nimefueahi, washiriki wa mafunzo haya wamekuwa ‘active’ mwanzo mwisho, unaona kabisa kuna kitu wanakielewa na wako tayari kukifanyia kazi”.
Kauli hiyo inasisitiza umuhimu wa kuongeza uwezo wa wanahabari kuchunguza masuala ya kiuchumi na kimazingira kwa pamoja, badala ya kuyaandika kama ajenda zinazojitegemea.
JET kuimarisha uandishi wa habari za uchumi wa kijani na buluu
"Kwa kutengeneza fursa kwa sekta hizi kujifunza kutoka kwa kila mmoja, mafunzo haya yameweka msingi wa ushirikiano imara, ushirikishwaji wenye uelewa mpana na ubia unaoweza kuchangia mustakabali endelevu wa Tanzania.
“JET itapeleka maarifa haya kwa wanachama wake wengine, na tunatarajia kuona habari nyingi zaidi zenye tafiti na uchambuzi wa kina kuhusu uchumi wa kijani na buluu katika vyombo vya habari nchini Tanzania. Tunatarajia pia kuendelea na ushirikiano zaidi na WWF," alisema Chikomo.
Kauli hiyo inaweka matarajio mapya kwa sekta ya habari nchini, hasa katika kipindi ambacho maamuzi kuhusu uwekezaji, matumizi ya rasilimali za asili na mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuwa na athari katika maisha ya wananchi.
Ni muhimu kwa wanahabari kujiuliza maswali kama vile: Je, miradi inayopata fedha za kijani inatekeleza ahadi zake? Je, jamii zinazozunguka maeneo ya uwekezaji zinanufaika? Je, kampuni
zinatoa taarifa sahihi kuhusu athari za shughuli zao kwa mazingira? Na je, fedha zinazotengwa kwa ajili ya uhifadhi zinafikia malengo yaliyokusudiwa?
Maswali hayo yanaweza kusaidia kuibua habari zenye thamani kwa umma na kuimarisha uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za taifa.
Kutoka kwenye mafunzo kwenda kwenye vitendo
Kwa kuzingatia changamoto zinazokabili Tanzania, umuhimu wa kuimarisha ushirikiano huu unaongezeka.
Benki ya Dunia imeeleza kuwa sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kuhamasisha uwekezaji kwenye nishati safi, majengo rafiki kwa mazingira, uzalishaji usiochafua mazingira na miundombinu inayohimili athari za tabianchi.
Pia imesisitiza umuhimu wa kutumia mifumo mbalimbali ya kifedha ili kuongeza rasilimali zinazohitajika kukabiliana na changamoto hizo.
Hata hivyo, fursa hizo haziwezi kutafsiriwa kuwa mafanikio bila kuwepo kwa taarifa sahihi, mifumo ya uwajibikaji, ushiriki wa wananchi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi.
Kwa wanahabari, hatua inayofuata ni kutumia maarifa waliyoyapata kuandaa habari zinazochunguza uhusiano kati ya fedha, mazingira na maisha ya watu. Kwa mashirika ya kiraia, ni kuimarisha utetezi, utafiti na ushirikishwaji wa jamii. Kwa sekta binafsi, ni kuyafanya masuala ya uendelevu kuwa sehemu ya uamuzi wa biashara na uwekezaji.
Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoandaliwa na WWF-Tanzania ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa miaka mitatu wa SIVSA unaofadhiliwa na Serikali ya Norway.
Hatua iliyochukuliwa Morogoro sasa inaweka swali muhimu mbele ya washiriki wote, maarifa yaliyopatikana yatabadilisha kwa kiasi gani namna kazi itakavyofanyika na kushirikiana?
Jibu lake halitapatikana kwenye chumba cha mafunzo au idadi ya mikutano itakayofanyika, bali katika ubora wa habari zitakazoandikwa, uwajibikaji utakaoboreshwa, uwekezaji endelevu utakaohamasishwa na manufaa yatakayofikiwa na jamii.
Ikumbukwe kuwa kujenga Tanzania endelevu si jukumu la wanahabari, wafanyabiashara au mashirika ya kiraia peke yao. Ni wajibu wa pamoja unaohitaji maarifa, maamuzi sahihi na hatua zinazolinda ustawi wa watu na mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

0 Comments