Ticker

7/recent/ticker-posts

‘ANDIKENI HABARI ZA UCHUMI WA BULUU NA KIJANI KWA MASLAHI YA UMMA’



NA. JIMMY KIANGO
‘Sauti ya Wanahabari ni sauti ya umma’.

Kauli hii imewasukuma wadau wa masuala ya uhifadhi wa mazingira na uchumi endelevu wa Kijani na Buluu, kuwasihi kuandika kwa wingi habari zenye tija zinazigusa maeneo hayo muhimu.


Habari hizo kwa sasa huandikwa kwa uchache na kwa taarifa za juu juu, na sasa Wanahabari wameombwa kuongeza juhudi katika kuandika habari hizo kwa kuzingatia maslahi ya umma, wakieleza fursa za kiuchumi, mchango wake katika maendeleo ya taifa na umuhimu wa kulinda rasilimali za mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


Wito huo uliotolewa Oktoba 30,2026 na Mtaalamu wa masuala ya uhifadhi, Allan Mgaza, mkoani Morogoro mara baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo ya siku tatu, yaliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na 

Wanyamapori (WWF), unakuja wakati Tanzania ikiendelea kutegemea sekta zinazohusiana na maliasili na mazingira katika kukuza uchumi, ikiwemo uvuvi, utalii, kilimo, misitu, ufugaji nyuki, nishati jadidifu na biashara zinazotokana na rasilimali za bahari na maji.


Kwa waandishi wa habari, kuandika kuhusu uchumi wa buluu na kijani hakupaswi kuwa ni kuripoti shughuli za upandaji miti, usafi wa fukwe au uhifadhi wa bahari pekee. 


Ni muhimu kuchunguza uhusiano uliopo kati ya mazingira, ajira, uwekezaji, biashara, mapato ya wananchi, usalama wa chakula na ustawi wa jamii.


Habari hizi zinapaswa kuonyesha namna matumizi endelevu ya rasilimali yanavyoweza kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi, huku zikifichua changamoto za uchafuzi, uharibifu wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi na matumizi yasiyo endelevu ya maliasili.

BAHARI NI MTAJI WA TAIFA
Tanzania ina fursa kubwa ya kukuza uchumi wa buluu kutokana na rasilimali zake za bahari, maziwa, mito na maeneo oevu. 


Uchumi huu unahusisha matumizi endelevu ya rasilimali za maji kwa ajili ya uzalishaji mali, ajira, biashara, chakula, usafirishaji, utalii na uwekezaji bila kuharibu mifumo ya ikolojia inayotegemeza shughuli hizo.


Sekta ya uvuvi ni miongoni mwa maeneo yenye mchango mkubwa katika uchumi wa buluu. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya utafiti juu ya kupunguza umasikini REPOA mwaka 2025 kuhusu sekta ya uvuvi Tanzania Bara na Zanzibar unaonyesha kuwa sekta hiyo inachangia takribani asilimia 1.7 ya Pato la Taifa, inaajiri watu 255,000 moja kwa moja na kusaidia ajira nyingine takribani milioni 5.745 kwa njia zisizo za moja kwa moja. 


Takwimu hizo zinaonyesha kuwa uvuvi si shughuli ya kupata kitoweo pekee, bali ni mnyororo mpana wa kiuchumi unaohusisha wavuvi, wafugaji wa samaki, wachakataji, wasafirishaji, wauzaji wa samaki, watengeneza nyavu na wajasiriamali wengine.


Hata hivyo, fursa hizo haziwezi kudumu endapo kutakuwa na uvuvi haramu, uharibifu wa matumbawe, uchafuzi wa bahari, uharibifu wa mikoko na nyasi bahari pamoja na matumizi yasiyodhibitiwa ya rasilimali za maji.


Hapa ndipo nafasi ya mwandishi wa habari inapokuwa muhimu. Ni lazima habari zifuatilie si tu idadi ya samaki wanaovuliwa, bali pia hali ya mazalia ya samaki, mapato ya wavuvi, upatikanaji wa masoko, gharama za uzalishaji, athari za mabadiliko ya tabianchi na namna jamii zinazozunguka bahari zinavyonufaika na uwekezaji.


Mfano mzuri ni matumbawe, nyasi bahari na mikoko. Rasilimali hizi zina mchango katika kuhifadhi bioanuai, kutoa makazi na mazalia ya viumbe wa baharini, kunasa hewa ukaa na kupunguza athari za mawimbi katika maeneo ya pwani. 


Waandishi wa Habari, wanapaswa kuandika kuhusu thamani yake kiikolojia na kiuchumi, pamoja na changamoto zinazokabili jamii zinazozitegemea.


Serikali tayari imeweka mwelekeo wa kisera kupitia Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 na Mpango wa Utekelezaji wa Uchumi wa Buluu katika Uvuvi na Ufugaji wa Viumbe vya Majini wa mwaka 2025–2035. 


Mipango hiyo inafungua nafasi ya kuandika habari zinazochunguza utekelezaji, uwekezaji, matokeo na manufaa kwa wananchi. 


MAZINGIRA NI MSINGI WA MAENDELEO
Kwa upande mwingine, uchumi wa kijani unalenga kukuza uchumi na ustawi wa jamii huku ukipunguza uchafuzi, matumizi mabaya ya rasilimali na uharibifu wa mazingira. 


Unahusisha kilimo endelevu, nishati safi, uhifadhi wa misitu, utalii endelevu, viwanda vinavyotumia teknolojia safi, usimamizi wa taka na matumizi bora ya ardhi na maji.


Kwa Tanzania, eneo hili lina umuhimu mkubwa kwa sababu uchumi wa wananchi wengi unategemea shughuli zinazohusiana moja kwa moja na mazingira.


Kwa mujibu wa Takwimu za Taifa za mwaka 2025 zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), sekta ya kilimo ilichangia asilimia 26.3 ya Pato la Taifa, wakati huduma zilichangia asilimia 42.4 na viwanda pamoja na ujenzi asilimia 31.3. Pato la Taifa kwa bei za soko lilifikia Sh trilioni 234.1. 


Takwimu hizi zinaonyesha umuhimu wa kuunganisha maendeleo ya kiuchumi na matumizi endelevu ya rasilimali, hasa katika kilimo, misitu na uzalishaji wa nishati.


Mfano, mkulima anayetumia mbolea za asili, kupunguza matumizi ya viuatilifu hatarishi, kuhifadhi rutuba ya udongo, kutumia maji kwa ufanisi na kuwekeza katika kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi anaweza kuchangia kupunguza gharama za uzalishaji na kulinda mazingira.


Vilevile, uwekezaji katika nishati jadidifu kama jua, upepo, maji na bayogesi unaweza kupanua upatikanaji wa nishati, kuchochea biashara na kupunguza utegemezi wa nishati zinazochafua mazingira.


Tanzania ina Mkakati wa Taifa wa Nishati Jadidifu wa mwaka 2024–2034, unaoweka malengo ya kuongeza uwezo wa uzalishaji wa nishati ya jua, upepo, jotoardhi na maji. 


Mkakati huo unaweka malengo ya megawati 804 za nishati ya jua na megawati 750 za upepo ifikapo mwaka 2034. 


Hizi ni fursa muhimu za habari zinazoweza kuwasaidia wananchi kuelewa namna uwekezaji wa nishati safi unavyoweza kuleta ajira, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania.


Ukweli ni kwamba Sheria zipo, lakini wananchi wanahitaji kujua utekelezaji wake na kundi linaloweza kufanikisha hilo ni Waandishi wa Habari.


Umuhimu wa waandishi wa habari kuandika masuala haya unaongezeka kutokana na uwepo wa sheria, sera na mikakati inayolenga kusimamia rasilimali za taifa.


Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Sehemu ya XVI, Kifungu cha 182-203, katika Toleo la Marejeo la mwaka 2025, inaweka mifumo ya kisheria na kitaasisi wa kusimamia mazingira, tathmini ya athari za mazingira, udhibiti wa uchafuzi, adhabu, usimamizi wa taka na ushiriki wa wananchi katika masuala ya mazingira.


Sheria nyingine muhimu ni Sheria ya Uvuvi, Sura ya 279, Sheria ya Misitu, Sura ya 323, na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sura ya 283. Sheria hizi zinaweka misingi ya kusimamia na kutumia rasilimali husika kwa njia endelevu. 


Hata hivyo, kuwa na sheria pekee hakutoshi. Wananchi wanahitaji kufahamu haki zao, wajibu wao na namna taasisi zinazohusika zinavyotekeleza sheria hizo.


Waandishi wa habari wana nafasi ya kuchunguza kama miradi ya uwekezaji inazingatia tathmini ya athari za mazingira, kama jamii zinazozunguka maeneo ya uwekezaji zinapata manufaa, kama sheria zinatekelezwa na kama wanaoharibu mazingira wanachukuliwa hatua.


Ni muhimu pia kufuatilia bajeti zinazotengwa kwa ajili ya uhifadhi, matumizi ya fedha za miradi, fidia kwa jamii zilizoathirika na matokeo halisi ya uwekezaji.


Kwa maana hiyo, habari za uchumi wa buluu na kijani zinapaswa kuwa sehemu ya uandishi wa habari za uchunguzi, uwajibikaji na maendeleo.


WWF YAWEKA MKAZO 
Akizungumzia umuhimu wa habari za mazingira, Ofisa Programu Mwandamizi wa WWF, Happy Minja, amewataka waandishi wa habari kuweka mkazo katika masuala ya uhifadhi, mazingira na uchumi wa buluu ili kuhamasisha hatua zinazolinda rasilimali za taifa.


Minja amesema hayo wakati wa mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari za mazingira yaliyofanyika mkoani Morogoro, yaliyoandaliwa na WWF na kuzishirikisha Asasi zisizo za Kiraia, Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).


Amesema uhifadhi wa mazingira ni nguzo muhimu katika kuchochea maendeleo endelevu ya sekta mbalimbali, hivyo WWF imeamua kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kusaidia kusukuma ajenda hiyo kupitia kazi zao.


"Sisi kama WWF tunatamani waandishi wa habari waweke mkazo kwenye masuala ya uhifadhi kwa ujumla, kwa sababu uhifadhi na mazingira ni kila kitu, uhai wetu sisi unategemeana na mazingira," amesema.


Ameongeza kuwa waandishi wa habari wana uwezo wa kupaza sauti kuhusu changamoto za mazingira na kuifanya Serikali pamoja na taasisi nyingine kuchukua hatua zinazostahili.


Minja amesema WWF imeamua kuwajengea uwezo waandishi kwa kutambua nafasi yao katika kuhabarisha na kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi, mazingira, uchumi wa buluu na fursa za uwekezaji katika sekta hizo.


"Tunapowajengea waandishi uwezo, tunaamini wao watatumia elimu yao kuelimisha taifa na jamii kwa ujumla," amesema.


Amesema mafunzo hayo ni awamu ya nne ya programu hiyo, iliyoanza mwaka 2022, na kuendelea mwaka 2023, 2025 na 2026, huku akieleza kuwa wameona mabadiliko katika namna masuala ya uhifadhi na mazingira yanavyoripotiwa.


Minja amesema WWF inajivunia kushirikiana na kundi hilo la waandishi kwa kuwa wamekuwa wakisaidia kuibua changamoto za uhifadhi ambazo zimekuwa zikifanyiwa kazi.


MIRADI YA MAZINGIRA IANZE NA WAANDISHI
Kwa upande wake, Mkurugrnzi wa JET, John Chikomo, amesema ushirikiano kati ya WWF na JET katika kuwajengea uwezo waandishi ni muhimu katika kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi kuhusu uhifadhi na mazingira.


Chikomo amesisitiza umuhimu wa taasisi na watekelezaji wa miradi kuwashirikisha waandishi wa habari tangu hatua za mwanzo za utekelezaji wa miradi badala ya kuwaita wakati wa kutangaza mafanikio au changamoto zilizojitokeza.


"Nadhani kuna haja ya watekelezaji wa miradi kubadilika kwa kushirikisha kundi la wanahabari tangu mwanzo na sio kuja kuripoti matokeo au changamoto," amesema.


Ushauri huo una umuhimu mkubwa kwa sababu ushiriki wa waandishi tangu mwanzo unawawezesha kufahamu malengo ya mradi, bajeti, walengwa, teknolojia zinazotumika, changamoto na viashiria vya mafanikio.


Pia unawapa nafasi ya kufuatilia mabadiliko yanayotokea katika maisha ya wananchi na kutoa taarifa zinazotokana na ushahidi badala ya kutegemea taarifa za mwisho za taasisi zinazotekeleza miradi.


WAANDISHI WANA NAFASI YA KUHARAKISHA UCHUMI ENDELEVU
WWF imekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea uwezo wa waandishi wa habari za mazingira na uhifadhi, mafunzo hayo yanayofanyika kwa mara ya nne yameendelea kuongeza uelewa na weledi wa waandishi katika kuripoti masuala yanayohusu mazingira na maendeleo endelevu.


Awamu hii imejikita zaidi katika uchumi wa buluu na uendelevu katika uhifadhi, maeneo ambayo yana nafasi kubwa katika maendeleo ya Tanzania.


JET kwa kushirikiana na wadau wengine imekuwa ikiwapeleka wanachama wake katika maeneo mbalimbali ambako shughuli za uhifadhi zinafanyika, ikiwemo mkoani Tanga, ambako walipata fursa ya kujifunza kuhusu umuhimu wa nyasi bahari katika kulinda mifumo ya ikolojia ya baharini na shughuli za wakulima wa mwani.


Hata hivyo hali ya uandishi wa habari za mazingira imeendelea kubadilika ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, ambapo masuala hayo hayakuwa yakipewa nafasi ya kutosha katika vyombo vya habari.


KILIMO ENDELEVU NI SEHEMU YA UCHUMI WA BULUU NA KIJANI
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Shoroba kutoka Taasisi ya Kuendeleza Shoroba za Kilimo Tanzania (AGCOT), John 


Banga, amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhamasisha matumizi ya mbinu endelevu katika kilimo ili kulinda mazingira na kuongeza tija kwa wakulima.


Amesema elimu inayotolewa kwa wakulima kuhusu kilimo endelevu inaweza kuwasaidia kuboresha uzalishaji, kutafuta masoko ya kisasa na kuongeza ushindani wa bidhaa zao.


"Vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhamasisha kilimo endelevu kinachotunza mazingira na kutafuta masoko ya kisasa na kufikia adhma ya taifa ya uchumi wa buluu na kijani," amesema.


Banga amesema kilimo na mazingira vina uhusiano wa karibu kwa kuwa uzalishaji wa mazao unategemea mifumo ya asili ikiwemo mvua, rutuba ya udongo, maji, viumbe hai na uwiano wa kiikolojia.


Amesema kuelimisha wakulima kuhusu mbinu bora za kilimo na matumizi endelevu ya rasilimali ni hatua muhimu katika kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuchangia maendeleo ya taifa bila kuathiri mazingira.


HABARI MUHIMU

Ili kuimarisha mchango wa uandishi wa habari katika uchumi wa buluu na kijani, kuna maeneo muhimu yanayohitaji kupewa kipaumbele ambayo ni 


Uchumi wa buluu unaozingatia uvuvi endelevu, ufugaji wa samaki, kilimo cha mwani, utalii wa baharini, usafirishaji wa majini, uhifadhi wa mikoko, matumbawe na nyasi bahari.


Uchumi wa kijani unaobeba kilimo ikolojia, nishati jadidifu, matumizi ya teknolojia safi viwandani, uhifadhi wa misitu, utalii endelevu na usimamizi wa taka.


Ajira na uwekezaji ni fursa za vijana na wanawake katika biashara zinazotokana na rasilimali za mazingira, masoko ya bidhaa endelevu na uwekezaji wa kijani na buluu.


Uwajibikaji ni uchunguzi kuhusu uharibifu wa mazingira, uchafuzi wa maji, ukataji miti, uvuvi haramu, matumizi ya kemikali hatarishi na utekelezaji wa sheria.


Mabadiliko ya tabianchi: Athari zake kwa wakulima, wavuvi, wafugaji, jamii za pwani na uchumi wa taifa, pamoja na suluhisho zinazotekelezwa.


Manufaa kwa wananchi: Kufuatilia kama miradi ya uhifadhi na uwekezaji inazalisha ajira, kuongeza kipato, kuboresha maisha na kutoa fursa sawa kwa jamii zinazozunguka maeneo husika.


HABARI ZIWE DARAJA
Mustakabali wa uchumi wa buluu na kijani Tanzania hauwezi kutegemea Serikali na wawekezaji pekee. 


Unahitaji pia wananchi wanaoelewa thamani ya rasilimali zao, taasisi zinazowajibika na vyombo vya habari vinavyoweza kuunganisha taarifa za mazingira na maisha halisi ya watu.


Waandishi wa habari wanapaswa kuacha kuandika mazingira kama suala la kitaalamu linalohusu wataalamu pekee, bali wayaangalie kama suala la uchumi, afya, ajira, biashara, uwekezaji na haki ya wananchi kupata mazingira safi na salama.


Kila habari kuhusu samaki, mikoko, misitu, kilimo, nishati safi au mabadiliko ya tabianchi inapaswa kujibu maswali muhimu.

Post a Comment

0 Comments