Ticker

7/recent/ticker-posts

KATESH YAANZA KUREJEA KWENYE HALI YAKE YA KAWAIDA

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema hadi sasa urejeshaji wa miundombinu ya barabara na madaraja madogo  yaliyoharibiwa na maporomoko ya matope na mawe yaliyotokea Desemba 3, 2023 kwenye mji wa Katesh wilayani Hanang mkoani Manyara umefikia asilimia 75. 

Kasekenya amesema hayo leo  Disemba 12, 2023 mkoani Manyara mara baada ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa kazi hizo zinazofanywa na  Wakala ya Barabara (TANROADS) wakishirikiana na Wakala ya Barabara za  Vijijini na Mijini (TARURA). 

"Hadi sasa tumefikia karibu asilimia 75 ya kuirejesha Katesh katika hali yake na tutakachofanya kabla ya kuondoka tutakuwa tumehakikisha tumesafisha barabara zote na kuzirudisha katika hali yake ya awali kama tulivyokuwa tumeagizwa na Rais Samia Suluhu Hassan", amesema Kasekenya. 


Kasekenya ameongeza kuwa mitambo na magari imeshafika eneo la Katesh ambapo kuna magari 32 yenye uzito wa tani 13, vijiko 12, doza 3, magari ya kishindilia barabara mawili, mitambo ya kubeba matope (roller) miwili, na mitambo yote hiyo inaendelea kufanya kazi usiku na mchana. 

"Ninaposema magari yenye uzito wa tani 13 na yale yenye uwezo wa kubeba magunia 130 kwa wakati mmoja na mpaka sasa magari hayo yameweza kubeba tope na mawe zaidi ya safari 4,000 na kazi bado inaendelea", amefafanua Kasekenya 

Amesema Wizara hiyo kupitia Wakala hizo wanaendelea kufungua barabara za mitaa kwa ajili ya kuhakikisha njia zinafunguka kwa kutoa mawe na magogo ili kuhakikisha kama kuna mali za watu zilisalia katika makazi yao wanaweza kuingia na kufanya usafi. 


"Kwahiyo kazi kubwa ambayo tunafanya sisi Wizara, TANROADS na TARURA ni kurudisha maeneo yote ya mitaa, vichochoro na kusafisha eneo la soko na kuwarudisha wale waliokuwa wanafanya biashara au waliokuwa wanaishi waweze kuishi kwenye nyumba zao na tumejipangia mpaka kufikia kesho tuwe tumefikia walau asilimia 95", amesisitiza Mhandisi Kasekenya.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amesema kuwa mbali na Serikali kurejesha miundombinu pia imeendelea kuwa bega kwa bega na Wananchi .

Post a Comment

0 Comments