Timu ya Taifa ya Argentina imeshindwa kuilinda rekodi yake ya kutopoteza mchezo tangu kombe la dunia baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Uruguay katika mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya kombe la dunia mwaka 2026.
Argentina walikuwa hawajapoteza mchezo tangu walipopoteza Novemba 22, 2022 dhidi ya Saudi Arabia katika michuano ya kombe la dunia iliyofanyika nchini Qatar na kipigo dhidi ya Uruguay kinakuwa cha kwanza tangu kombe la dunia mwaka jana.
Baada ya kupotezwa kwenye mchezo huo Nahodha wa Argentina Lionel Messi amesema mchezo dhidi ya Uruguay haujawahi kuwa mwepesi
“ Sisi tuna timu nzuri na ipo hivyo siku zote lakini haijawahi kuwa rahisi tukicheza na Uruguay kwa sababu ni watu wanaomwaga jasho jingi uwanjani” amenukuliwa Messi
Kocha wa Argentina, Lionel Scalon amesema siku zote amekuwa akisema kwakuwa wao ni Mabingwa wa Kombe la Dunia haimanishi kuwa hawawezi kupoteza mchezo.
Kipigo hicho katika Uwanja wa Bombonera huko Buenos Aires nchini Argentina kinakuwa ni cha kwanza kwa Argentina wakiwa nyumbani tangu walipofungwa 1-0 na Paraguay mwaka 2016.
Hata hivyo bado Argentina wanashika usukani katika kampeni ya kufuzu kombe la dunia 2026 kwa timu za Amerika Kusini wakiwa na alama 12 wakifuatiwa na Uruguay wenye alama 10 baada ya michezo mitano huku Brazil wakiendelea kusota baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Colombia.
0 Comments