Ticker

7/recent/ticker-posts

UHARIBIFU WA VYANZO VYA MAJI WAKAUSHA MTO UMBA


Tatu Maingi akichota maji kwenye moja ya mashimo yaliyochimbwa ndani ya mto Umba, ambao kwa sasa umekauka kabisa.


NA JIMMY KIANGO- MKINGA

MTO Umba upo Kaskazini Mashariki mwa Tanzania, unaanzia kwenye safu ya milima ya Usambara katika misitu ya Shagayu kwa kimo cha mita 2000 usawa wa bahari, unapita Mlalo na kuishia nchini Kenya.  

Kilomita chache kabla ya kukomea Bahari ya Hindi mto huo unavuka mpaka wa Kenya kwenye Kaunti ya Kwale na kimsingi mto huo unatazamwa pia kama ni sehemu ya mpaka wa Tanzania na Kenya.

 Kwa sasa mto huo ambao unatumiwa na maelfu ya watu na wanyama umekauka kabisa, hakuna hata tone la maji linalotiririka.

Afrinews Swahili ilipata nafasi ya kushuhudia sehemu ya mto huo inayopita kwenye Kijiji cha Mbuta, kilichopo Kata ya Mwakijembe, wilayani Mkinga mkoani Tanga ukiwa umekauka kabisa.

“Ni mto muhimu kwetu wakazi wa Mbuta na vijiji vingine vinavyopakana na mto huu, lakini kama unavyoona hakuna maji yanayotiririka, mto umekauka ni adha kwetu na kwa mifugo yetu,”anasema Tatu Maingi.

Sababu kubwa ya mto huo kukauka kabisa pamoja na kuwa ni ukame uliolikumba eneo kubwa la nchi, lakini uharibifu wa mazingira hasa ukataji wa miti na kilimo kwenye vyanzo vya maji ni miongoni mwa sababu kuu.


“Ni kweli watu wanalima pembezoni mwa mto na athari kubwa ziko kule kwenye chanzo cha mto huu, pamoja na ukame uliopo, lakini ukataji wa miti na kilimo na ufugaji unaogusa vyanzo vya maji ni sababu,”anasema Thomas Sawe mmoja wa maofisa wa Shirika la WWF.

Tatu Maingi anasema kwakuwa mto huo ndio kimbilio lao la maji, sasa wanalazimika kuchimba mashimo mafupi na marefu ndani ya mto huo ili kupata maji ya matumizi yao.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbuta Emmanuel Simba aliiambia Afrinews kuwa, serikali ya Kijiji kwa kushirikiana na wanakijiji na wadau wa maendeleo kama WWF wanaangalia namna sahihi ya kukabiliana na uharibifu wa vyanzo vya maji.


“Tunao mpango wa kupanda miti rafiki na maji pembezoni mwa mto huu, jambo la kushukuru ni wenzetu wa WWF ambao ni wadau wa maendeleo wamekubali kulifanya hili.

 “Hatuna namna ya kufanya zaidi ya kuhakikisha tunatunza vyanzo vya maji na njia pekee ni kuzitunza zile mita 60 za mto,”alisema Simba.

 Akilizungumzia hilo la kupanda miti rafiki na maji, mmoja wa maofisa wa WWF, Gladness Mtega, alisema ni kweli wanaompango huo ambapo watashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga na serikali ya Kijiji katika kulifanikisha hilo.

“Sisi tutawawezesha wenzetu hawa katika kufanikisha uoteshaji wa miti, tunaamini ili kulinda vyanzo vya maji ni lazima tupande miti pembezoni mwa mto huu.”

Ng'ombe wakilishwa pembezoni mwa mto Umba katika kijiji cha Mbuta, wilayani Mkinga.

 

Post a Comment

0 Comments