Ticker

7/recent/ticker-posts

KATIMBA AWAJENGEA UWEZO WATENDAJI WA VIJIJI,KATA, NA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII MALINYI

  

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Khamis Jaaphar Katimba

NA MWANDISHI WETU-MALINYI

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Khamis Jaaphar Katimba amewajengea uwezo wa kiutendaji  Maafisa maendeleo ya Jamii wa  Kata, Watendaji wa Vijiji na Kata ili waweze kusimamia na kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

 

Watendaji hao wamefahamishwa majukumu yao ambayo wanatakiwa kuyasimamia  kikamilifu ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa miradi na kuendeleza utawala bora.

 

Kwa upande wa mapato  Watendaji hao wametakiwa kuwa na orodha ya  vyanzo vyote vya ukusanyaji  wa mapato vilivyo katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuwa na orodha ya wamiliki wote  wa  biashara  katika maeneo yao na kuhakikisha  kuwa katika kipindi hiki cha Novemba  wanawafikia Wafanyabiashara wote  na kuwahamasisha kulipia leseni zao za biashara, na wasio na leseni wakate na kuwa Disemba mwanzoni kitafanyika kikao  cha tathimini ya utekelezaji wa maelekezo hayo.

 

Kuhusu miradi, watendaji hao wameelekezwa kuwa wao ndiyo wasimamizi wakuu wa miradi hiyo hivyo ni wajibu wao kuhakikisha kuwa  fedha zote zinazoenda katika utekelezaji wa miradi zinafanya kazi iloyokusuidiwa, wawe karibu na miradi hiyo na inapotokea changamoto watafute namna ya kutatua  badala ya kukaa kimya.

 

Ameelekeza   ufanyikaji wa vikao vya menejimenti za Kata ambapo  Maafisa maendeleo ya Jamii  watakua Waratibu, na kuwa miradi isipotekelezwa kwa wakati  wao ndio watakaowajibika , Maafisa hawa watahusika na shughuli zote ambazo zinaendelea katika Kata na Vijiji.

 

 Katimba amesema kuwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wamekumbushwa pia kuwa wao  ndio kiungo kikubwa  katika maendeleo ya Kata zao, lakini uzoefu unaonyesha kuwa wanajikita  sana kwenye masuala ya mikopo na kusahau majukumu yao mengine.

 

Aliwaelekeza kuwa ni lazima washirikiane na Wataalam wengine wa Kata  kuhakikisha wanabadilisha mitazamo  hasi iliyopo katika Jamii na kuielekeza jamii katika mwelekeo  unaohitajika.

 

“Katika maeneo yetu kuna  baadhi ya watu ambao wana mitazamo tofauti kuhusu shughuli za maendeleo, kuna Watu ambao wanaamini mila na desturi hatarishi katika Jamii hivyo ni jukumu lenu kubadili mitazamo hii katika Jamii,”  alisema Katimba.

 

Akifunga mafunzo hayo Katibu Tawala wa Wilaya ya Malinyi, Bi.Saida Mhanga  aliwataka Watendaji hao kutimiza wajibu wao  hasa katika utawala bora , wakae ofisini  kusikiliza  na kutatua kero za Wananchi.

 

“Kumekua na  malalamiko mengi yanayotoka kwa Wananchi  yanapelekwa kwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya  ambapo ukichunguza kwa makini  unaona kwamba  ni kutotekeleza majukumu ya Watendaji katika maeneo yao ambapo masuala haya  yangeweza kutatuliwa katika maeneo yao”alisema Bi.Mhanga

 

Aidha amewataka  Watendaji hao kuandaa kasha la kupokea maoni/mapendekezo  kutoka kwa Wananchi, na kuongeza kuwa Watendaji hao waendeshe vikao vya kisheria  na wasome taarifa za mapato na matumizi ili wananchi wawe na imani na Serikali yao.

 

Akitoa mada ya kuzuia na kupambana na  rushwa Kamanda wa TAKUKRU Wilaya ya Malinyi Bi. Sikujua Kimweri  aliwataka Watumishi kuzingatia miongozo na taratibu za kazi.

 

Kamanda huyo alisema kuwa TAKUKURU  ina lengo la kuhakikisha kuwa  shughuli zote za Serikali  zinapangwa na kufanyika  kwa mujibu wa taratibu  ili Wananchi waone kazi zinazofanywa na Serikali yao.

 

Bi. Kimweri aliwataka  Watendaji hao kuhakikisha kuwa mapato ya Halmashauri yanakusanywa na yanatumika kwa usahihi  kulingana na bajeti ilivyo.

 

Aliwataka Watendaji hao kuwa makini na fedha  za miradi  ambazo zinaenda kutekeleza miradi katika maeneo yao na kuongeza kuwa miradi hiyo itekelezwe kwa mujibu wa BOQ miongozo na kanuni za Serkali .

 

Amewataka Watendaji  hao kuzingatia  taratibu  hizo kwasababu  wakienda kinyume watakutana  na mkono wa sharia, na kuwa ni vema wakafanya kazi kwa weledi  na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

 

Kwa upande wa kilimo, mifugo na uvuvi , Mkuu wa Idara hiyo Gipson Absalom amewaambia Watendaji kuwa Idara yake  inafanya kazi kwa ukaribu na mamlaka ya hali ya hewa  na kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa , Wilaya ya Malinyi itakua  na mvua chache, za wastani na chini ya wastani, hivyo amewataka Watendaji  washirikiane na maafisa kilimo waliopo katika Kata na Vijiji  kutoa elimu kwa Wananchi  kuhakikisha kuwa wanapanda  mazao yanayostahimili  maji au mvua chache  na wale wanaotaka kulima mpunga wachague maeneo ambayo yana majimaji.

 

 

Post a Comment

0 Comments