Ticker

7/recent/ticker-posts

MACHAFUKO GAZA-ISRAEL; VITA YA “NAKBA” NA MAGAIDI

VIFO Israel ni watu zaidi ya 1,000. Gaza maafa ni zaidi ya 900. Takriban watu 200,000 hawajulikani walipo Gaza. Makombora ya Israel, yameharibu makazi na miundombinu Gaza. Hii ni ripoti ya leo Jumatano asubuhi (Oktoba 11, 2023).

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema “shoo ndio kwanza imeanza”. Iran wamekana kuhusika na mashambulizi dhidi ya Israel, ila kiongozi wao, Ayatollah Khamenei, amesema: “Tunaibusu mikono iliyopanga na kuushambulia utawala wa Kizayuni.”

Shughuli ipo Mashariki ya Kati, ila anguko kubwa la sarafu linaikumba Urusi. Thamani ya rouble (fedha ya Urusi), imepata anguko la kihistoria. Pauni ya UK, nayo imeanguka kwa asilimia sita dhidi ya dola ya Marekani.

Siku nne za machafuko Gaza-Israel, zimethibitisha kuwa dola ya Marekani ndio sarafu salama zaidi duniani. Maelfu wanabadili fedha zao kwa dola ili kujiweka tayari kwa lolote.

Marekani wanaunga mkono Israel, vivyo hivyo UK. China wametoa tamko la kutaka kusitishwa kwa mapigano. Urusi wamesema kuundwa kwa dola ya Palestina ndio suluhu ya mgogoro wa Mashariki ya Kati.

Hoja ya kuundwa dola ya Palestina kama suluhu ya mgogoro Mashariki ya Kati, ilitamkwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, kisha ikarejewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov.


SHAMBULIZI LA KUSHITUKIZA

Jumamosi (Oktoba 7, 2023), asubuhi, wanajeshi wa Hamas walianza mashambulizi ya anga kuelekea Israel. Wakilenga zaidi miji ya Tel Aviv na Jerusalem.

Taarifa ya Israel imeeleza kuwa baada ya kupita saa moja, kutokea shambulio la kwanza la roketi, wanajeshi wa Hamas waliingia Israel kupitia ardhini, baharini na angani.

Ni shambulizi la ghafla mno kutoka Palestina (Ukanda wa Gaza) kwenda Israel. Waisrael wana maswali mengi kuhusu umakini wa vyombo vyao vya ulinzi na usalama, ikiwa wanaweza kupewa kipigo cha kushitukiza kama ilivyotokea Jumamosi, pasipo kutambua chochote.

Miji 22 ya Israel ilivamiwa na Hamas Jumamosi. Wanajeshi hao waliteka raia na kuwashikilia. Wengi wao waliwavusha mpaka  na kwenda nao hadi Gaza wanakowashikilia.

Israel, hasa majiji ya Tel Aviv na Jerusalem, inalindwa na mitambo maalum ya ulinzi wa anga ya Iron Dome. Mitambo hiyo hutambua na kusambaratisha makombora yanayoelekezwa Israel, kuanzia umbali wa kilometa nne hadi 70.

Shambulizi la Hamas walilolifanya  Jumamosi, linaonesha kuwa wapiganaji hao wameshazisoma Iron Dome za Israel na wanaelewa jinsi ya kuzizidi ujanja. Hamas walifyatua roketi karibu 5,000 ndani ya dakika 20, hivyo kufanikiwa kupenyeza makombora yalioua raia na kuharibu majengo na miundombinu Israel.


SABABU YA SHAMBULIZI

Kiongozi wa Kijeshi wa Hamas, Muhammad Deif, alizungumza Jumamosi katika ujumbe wa sauti uliorekodiwa na kusambazwa kuwa mashambulizi dhidi ya Israel ni oparesheni ya kuwafanya maadui kufahamu muda wao wa kuikalia Palestina bila kuwajibika, umefika mwisho.

Ujumbe huo wa Deif, unakita moja kwa moja kwenye kiini cha mgogoro Mashariki ya Kati. Unaanzia Azimio la Balfour, Novemba 2, 1917 (wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia), UK walipotangaza kuunga mkono Wayahudi kuanzisha taifa lao ndani ya Palestina.

Historia inaonesha kuwa wimbi la kwanza la Wayahudi kuhamia Palestina lilikuwa mwaka 1878 mpaka 1882. Uhamiaji huo unaitwa Aliyah. Tafsiri yake ni Wayahudi kutoka uhamishoni, kurejea kwenye ardhi yao ya kihistoria na kijiografia.

Mwaka 1920 ilianzishwa Mamlaka ya Palestina. Uingereza ikiikalia Palestina kama koloni lake, haikufanya Wayahudi na Wapalestina waelewane. Vilevile, wimbi kubwa zaidi la uhamaji wa Wayahudi, kutoka maeneo mbalimbali, kuingia Palestina, kufuatia Azimio la UK la kuwaunga mkono kuanzisha taifa lao ndani ya  Palestina.

Halafu ikaja Vita ya Palestina mwaka 1947 - 1949, ambayo ililigawa eneo la Mamlaka ya Palestina katika vipande vitatu. Kipande cha kwanza ndio Israel, cha pili ni West Bank, iliyotwaliwa na Jordan, kisha Ukanda wa Gaza, iliyomilikiwa na Misri.

Mei 14, 1948, Wayahudi walilitangaza eneo lao kuwa dola huru ya Israel, hivyo kukoma kwa mamlaka ya kikoloni ya UK. Halafu, mwaka 1967, Israel iliwashitukiza Waarabu kwa mashambulizi ya ghafla, hivyo kuchukua maeneo yote ya Palestina, Peninsula ya Sinai, Misri na Golan, Syria.Kwa mujibu wa hukumu ya mwaka 2004 ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), Ukanda wa Gaza na West Bank (inayojumuisha Jerusalem Mashariki) ni maeneo ndani ya miliki ya Palestina.

Tangu mwaka 1967, Jordan na Misri zilipofurushwa Palestina, Gaza na West Bank ni maeneo yaliyotambulika kuwa yanashikiliwa kijeshi na Israel mpaka mwaka 2005, Israel ilipojiondoa Gaza, lakini imeendelea kubaki West Bank.

Kwa mantiki hiyo, Deif anaposema oparesheni yao ni ukumbusho kuwa muda wa adui kuikalia Palestina umefika mwisho, ni tafsiri kuwa Israel inapaswa kuondoka West Bank pamoja na Jerusalem Mashariki.

Deif alifafanua kuwa kitendo cha Israel kuikalia West Bank, na hivi karibuni polisi wa Israel kuvamia Msikiti wa Aqsa, Jerusalem, vilevile Israel kuwaweka kizuizini maelfu ya Wapalestina kwenye jela za Kiyahudi, ni nyongeza ya sababu za mashambulizi ya Jumamosi.


PALESTINA INAVYOONGOZWA


Ndani ya Palestina kuna vyama vikuu viwili, Hamas na Fatah. Kwa muda mrefu, Fatah kilichoasisiwa na shujaa wa wakati wote wa Wapalestina, Yasser Arafat, kiliongoza Mamlaka ya Palestina (PA), yaani West Bank na Gaza, chini ya Israel.

Uchaguzi wa Bunge mwaka 2006, uliingiza Palestina kwenye machafuko ya wenyewe kwa wenyewe. Hamas walishinda viti 74 vya ubunge, Fatah walipata viti 45. Vyama vingine viliambulia viti 13. Wagombea huru wanne pia walishinda.

Fatah waligomea matokeo hayo. Yakaibuka mapigano baina ya Hamas na Fatah. Hamas waliunda serikali ambayo ilisusiwa na Fatah. Serikali ya Hamas ilikumbwa na kibano kikali kutoka Israel, ikiwemo vikwazo vya kiuchumi na mawaziri wake kukamatwa na kufungwa magereza za Kiyahudi.

Athari za uchaguzi huo ziliigawa Palestina mara mbili na ndivyo inavyoongozwa mpaka sasa. West Bank ipo chini ya Fatah kwa mwavuli wa Israel, na Ukanda wa Gaza ambao unatawaliwa na Hamas.

Fatah na Hamas ni vyama vyenye itikadi na mitazamo tofauti. Hamas wanataka kusimika dola ya Kiislam Palestina, wakati Fatah mtazamo wao ni kutofungamanisha dini na dola.

Mkakati wa Hamas katika kupigania dola huru ya Palestina ni mapambano ya kijeshi. Fatah wanaamini inawezekana kufanikisha dola huru ya Palestina kwa njia ya mazungumzo.

Malengo, Hamas hawaitambui kabisa Israel, ila wanakubali mipaka ya mwaka 1967, inayotambua uwepo wa Israel. Fatah, wanatambua uwepo wa Israel, na malengo yao ni kuunda dola ya Palestina kulingana na mipaka ya mwaka 1967.

Tangu mwaka 2007, Hamas walipowafukuza Fatah Gaza, ukanda huo umekuwa ukipitia vikwazo vingi vya kiuchumi. Misri ndio imekuwa msaada mkuu wa Gaza kwa kipindi chote hicho.

Israel imedhibiti Gaza kuingiza bidhaa za kielektroniki, zikiwemo kompyuta. Hilo limefanyika kuhakisha Hamas hawatengenezi silaha. Kingine, Israel inadhibiti watu kuondoka na kuingia Gaza.

Tangu mwaka 2005, Israel ilipojiondoa Gaza rasmi, eneo hilo limekuwa likishambuliwa mara kwa mara na ndege za kivita za Israel pamoja na Fatah, kutokea West Bank. Chuki na roho ya kisasi inaishi ndani ya Wapalestina, hasa wa Gaza.

HATIMA NI NGUMU

Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel, amesema Waisrael wameingia kwenye vita kamili ya kujilinda. Ameagiza kukata umeme, chakula, mafuta na huduma nyingine za kijamii.

Kutokuundwa kwa taifa la Palestina kunasabisha nchi hiyo iwe tegemezi wa huduma nyingi za kijamii. Mathalan nishati, West Bank inapokea kutoka Jordan na Israel, wakati Gaza wanategemea Israel na Misri. Ndio sababu Netanyahu amekuwa na jeuri ya kuwakatia huduma.

Mkuu wa Sera za Kimataifa wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amesema tamko la Netanyahu linakiuka sheria za kimataifa na sheria za kibinadamu. “Israel wana haki ya kujilinda, ila kuwakatia umeme watu na kuwanyima chakula ni kinyume na sheria za kimataifa,” alisema Borrell.

Wapalestina wanaiita Israel “Nakba”, yaani janga. Kwamba kuingia kwa Wayahudi kwenye ardhi yao na kuanzishwa kwa taifa la Israel mwaka 1948, kulizima ndoto ya wao (Wapalestina), kuunda taifa lao.

Waisraeli, huogopa hata kutaja neno “Wapalestina”, kwa kuhisi jina hilo ni mtego wa Waarabu dhidi ya Wayahudi. Zaidi, ndani ya Israel, Palestina ni neno lenye tafsiri ya uhalifu. Wezi na wahalifu mbalimbali, huitwa Wapalestina.

Maswali ni mengi kuhusu Hamas walivyoizunguka Iron Dome za Israel na kufanikiwa kufikisha mashambulizi yao dhidi ya Israel. Hata hivyo, ukweli ni huu; wanajuana kwa uimara na udhaifu. Haikuwa vigumu Hamas kuandaa mashambulizi kwa kupigia hesabu udhaifu wa Iron Dome.

Matamko ya China na Urusi kuhusu dola mbili, yaani taifa la Palestina na Israel kama ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro wa Mashariki ya Kati ndio wito wa muda mrefu. Hata Marekani walishakuwa na sera hiyo.

Mwaka 2019, nchi 138 kati ya 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, ziliridhia Palestina kuwa dola huru na kuunga mkono ipewe kiti UN. Amerika Kusini, Afrika, Asia na visiwa vya Caribbean, wanaunga mkono Palestina kuwa dola rasmi.

Kikwazo kikubwa kwa Palestina ni nchi za Ulaya, Australia, Canada, Mexico na Marekani yenyewe. Kadiri taifa la Palestina linavyocheleweshwa, chuki inaongezeka. Uadui unakuwa mkubwa.

Shirika la kimataifa la haki za binadamu, Amnesty International, ripoti yake ya mwaka 2022, ilieleza kuwa Israel ni serikali ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Wapalestina. Amnesty International waliitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), kuifungulia mashitaka Israel.

Kwa Israel, Marekani na washirika wake, Hamas ni magaidi. Kwa Wapalestina, Waisrael ni “Nakba”. Msimamo huo unaungwa mkono na mataifa karibu yote ya Kiarabu na Waajemi.

Saudi Arabia, UAE, Bahrain na Morroco, ni mataifa ya Kiarabu yenye matamanio ya kujenga uhusiano mkubwa na Israel. Saudia wanaamini Iran ndio kikwazo cha amani Mashariki ya Kati kwa sababu wanawafadhili Hamas.

Ndimi Luqman MALOTO

Post a Comment

0 Comments