Na. Andrew Chale, Afrinews
Kaskazini Unguja, Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi amesisitiza suala la Amani na kulinda maadili ya Mzanzibar ni jambo jema kwa maendeleo na ukuaji wa nchi.
Rais Dkt Mwinyi amesema hayo mapema leo Septemba 3, 2023 katika dua maalum ya kumuombea pamoja na kuombea nchi kuwa na amani iliyoandaliwa na Wananchi katika eneo la Kaskazini A, kwenye msikiti wa Ijitimai, Kidoti Kaskazini A, Zanzibar.
Akizungumza katika dua hiyo, Dkt. Mwinyi amesisitiza wananchi kuendelea kuwa pamoja na mashirikiano kwa kufuata misingi ya dini ya Kiislamu ambayo itawasaidia kulinda maadili na kuepuka uvunjifu vya amani.
"Tuwe na amani, tuwe na umoja na tuwe na mshikamano kwa umoja wetu. Nchi ikikosa amani, hakuna lingine lolote linaloweza kufanyika.
Hivyo tunaomba tuendelee kuliombea dua taifa letu ili amani idumu," amesema Rais Dkt. Mwinyi
Ameongeza kuwa, amani tunayo, umoja upo, hili linapaswa kushukuriwa huku akitaka jambo hilo la dua kufanyika mara kwa mara.
"Nashukuru kwa dua hii, nimefarijika sana kwa kutuombea sisi viongozi ili kutimiza yale tulioahidi kutimiza.
Nitajitahidi kipindi kilichobakia, yale yote niliyotolea ahadi, nifanikiwe na kuendeleza kutimiza zaidi na zaidi," amesema Rais Dkt. Mwinyi.
Aidha, amesisitiza suala la maadili mema kwani kumekuwa na mmomonyoko wa maadili ikiwemo uzalilishaji na matumizi mabaya ya madawa ya kulevya.
"Zipo dalili za mmony'oko wa maadili kwa udhalilishaji na madawa ya kulevya.
Maadili haya yanaanzia ngazi ya familia, tunatakiwa kuwalea vijana wetu kwa maadili ya kiislamu, hii itasaidia hata jamii kujiondoa katika maadili mabaya."
Nae Waziri wa Katiba na Sheria, Harun Ali Suleiman ameomba jambo hilo liendelezwe na maeneo mengine katika kuhakikisha nchi inakuwa na maadili mema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayub Mohammed Ahmoud ameshukuru wananchi hao kumuandalia Rais dua maalum kwani ni jambo jema na ni ishara nzuri ya utendaji kwa Rais Dkt. Mwinyi ambaye ameweza kupeleka maendeleo ndani ya mkoa huo na Zanzibar kwa ujumla.
Mkuu wa mkoa huyo, amesema kuwa, watu zaidi ya 6000 wameshiriki dua hiyo kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa Kaskazini Unguja .
"Tunafarijika sana, Madrasa 250 zimetoa Wanafunzi na Walimu wao na kufanya idadi ya 3,000
Lakini pia Maimamu 700 kutoka misikiti ya ndani ya mkoa huu na wananchi wa maeneo yote wapo hapa, si jambo dogo na mimi nimefarijika sana." Amesema Ayub.
0 Comments