SPIKA wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson amewataka mawaziri waliopumzishwa katika Baraza la Mawaziri wasiwe na wasiwasi, kwani hiyo ni hali ya kawaida ni kama kocha katika timu za Simba na Yanga anapofanya mabadiliko ya kikosi chake kutegemea na mechi iliyo mbele yao.
Akizungumza bungeni leo Agosti 4,2023 wakati akitoa salamu za pongezi kwa Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Dotto Biteko, Spika amesema wapo mawaziri ambao walipumzishwa na baadaye wakarejeshwa katika baraza, hivyo hilo ni suala la kawaida.
Spika Dkt. Tulia amesema Bunge litaendela kuwapa ushirikiano mawaziri na manaibu ambao wameendelea kuaminiwa, pamoja na wapya.
"Na wale ambao mmepumzika kidogo msiwe na wasiwasi, hili baraza lina watu ambao waliwahi kupumzika, wakarejea, wakapumzika tena, wakarejea." Amewataka wasiwe na wasiwasi kwani nafasi hizo ni kwa zamu.
“Mtu zamu yake inafika basi anapewa kufanya hiyo kazi, zamu yake inapopungua kidogo ni kama kocha anaweka huyu si kwamba wewe uliyetoka ni mbaya ama namna gani, bali kocha anataka kukupumzisha kwa ajili ya maandalizi ya shughuli nyingine hapo baadaye.”
Ametolea mfano wachezaji wa Simba na Yanga, zinapoamua kupumzisha wachezaji wao kwa ajili ya mechi fulani ngumu iliyo mbele yao.
“Kama vile timu za Simba na Yanga huenda timu inayokuja baadae ikawa ni Namungo, halafu ukapumzishwa kidogo ili wacheze na Namungo kwa sababu mechi inayokuja ni ngumu zaidi.”
0 Comments