Ticker

7/recent/ticker-posts

NIC YAONGEZA KASI YA MALIPO KWA WATEJA WAKE

MABADILIKO ya kiutendaji yaliyofaywa na Shirika la Bima la Taifa (NIC) yamelisaidia kuingia kwenye soko la ushindani pamoja na kuongeza kasi ya kuwalipa wateja wake.

Mafanikio hayo yameanza kupatika katika kipindi cha kuanzia mwaka 2019/2022 baada ya kujiimarisha  kibiashara.

Shirika hilo ambalo ni mali ya serikali limejikita katika kufanya biashara ya bima za mali na ajali pamoja na bima ya maisha kama ilivyo kwa taasisi binafsi zaidi ya 30 zinazotoa huduma hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Dkt. Elirehema Doriye aliwaambia wanahabari kuwa Shirika hilo limekuwa likichukua hatua mbalimbali za mabadiliko ya kiutendaji na kibiashara tangu Julai,2019.

Hatua hiyo imewasaidia kumudu ushindani ambao umewawezesha kufanya vizuri kwenye soko.

Alisema mabadiliko yamefanyika kwenye  uongozi lengo likiwa ni  kuongeza ufanisi, weledi na tija, pia wamewekeza kwenye rasilimali watu kwa kuajiri wafanyakazi wenye sifa stahiki, wenye weledi na wabunifu.

Aidha, Dkt.Doriye alisema NIC pia  wamewekeza kwenye mifumo ya TEHAMA ambayo imewasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato, kuondoa matumizi ya karatasi, kupunguza muda wa kulipa madai hadi kufikia siku saba na kurahisisha utoaji wa huduma.

Alisema, kutokana na hatua za mabadiliko walizozichukua kuanzia mwaka 2019, wamefanikiwa kuondoa hasara kwa kuongeza mapato kutoka Shilingi Bilioni 76.45, mwaka 2019/2020 Hadi Shilingi Bilioni 103.94 mwaka 2021/22. 

“Ongezeko hili ni sawa na asilimia 17.98 kwa mwaka.

“Vilevile usimamizi madhubuti wa matumizi pamoja na kutoa mafunzo kwa watumishi kumeongeza ufanisi na kuondoa matumizi yasiyo na tija, jambo lililoshusha gharama za uendeshaji na kuongeza faida,” alisema Dkt. Doriye.

Katika kipindi cha miaka mitatu, NIC wamefanikiwa kulipa madai ya bima za wateja, ambapo hadi kufikia Juni 2022, wamelipa Shilingi Bilioni 33.79 kwa bima za Maisha na Shilingi Bilioni 40.18 kwa bima za mali na ajali.

“Tumeweza kulipa kodi ya mapato Serikalini kutokana na faida inayopatikana, ambapo ulipaji huo umeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 11.86 mwaka 2019/20 hadi Shilingi Bilioni 15.14 mwaka 2021/22 sawa na wastani wa asilimia 13.80 kwa mwaka,” alisema Dkt. Doriye.

Akizungumzia faida iliyopatikana kwa kipindi hicho, Dkt. Doriye alisema, faida ghafi imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 33.65 hadi Shilingi Bilioni 63.21 ambayo ni sawa na asilimia 43.91.

“Kutokana na faida mfululizo, tumeweza kupata malimbikizo ya faida ya Shilingi Bilioni 45.74 kufikia Juni 2022 kutoka kiasi cha malimbikizo ya hasara ya Shilingi Bilioni 19.31,” alisema.

Mbali na hayo, alizungumzia kukua kwa mali za NIC kutoka mali zenye thamani ya Shilingi Bilioni 350.36, hadi kufikia mali zenye thamani ya Shilingi Bilioni 423.99, ambapo ukuaji huo ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 10.51 kwa mwaka.

“Ufanisi katika uendeshaji umewezesha ukuaji wa mtaji wa wanahisa  kutoka Shilingi Bilioni 72.16 hadi Shilingi Bilioni 217.07, ukuaji huu ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 100.40 kwa mwaka,” alisema Dkt. Doriye.

Katika kipindi cha miaka mitatu, NIC pia imefanikiwa kuongeza uwekezaji katika hati fungani za Serikali, kutoka Shilingi Bilioni 51.58 hadi Shilingi Bilioni 105.64, ongezeko hili ni sawa na wastani wa asilimia 52.40 kwa mwaka.

“Uwekezaji katika amana ya benki umefikia Shilingi Bilioni 32.23 ukilinganisha na Shilingi Bilioni 19.53 kilichokuwepo mwaka 2019/20, ongezeko hili ni sawa na wastani wa asilimia 32.54 kwa mwaka,” alisema Dkt. Doriye.

Mwaka  2022 NIC wametoa gawio la Shilingi Bilioni 2.0 kwa Serikali, ukilinganisha na gawio la Shilingi Bilioni 1.5 walilotoa mwaka 2021.

Katika hatua nyingine, Dkt. Doriye alisema, ili kukabiliana na uwezo mdogo wa kuhimili hasara inayoweza kutokea l wamefanikiwa kuongeza mtaji wa Shilingi Bilioni 12.05 Aprili, 2022 sawa na ongezeko la asilimia 408.47.

“Hii ni kutoka mtaji uliokuwepo wa kiasi cha Shilingi Bilioni 2.95 na kufikia mtaji wa Shilingi Bilioni 15, kilichopo sasa,” alisema Dkt. Doriye na kusisitiza kuwa, NIC itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya bima nchini na kutoa elimu ya bima kwa wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili watanzania wengi wajiunge na huduma zinazotolewa na Shirika hilo.

“Bidhaa na huduma zetu zinapatikana Kidijitali,” alisema.

Post a Comment

0 Comments