Diwani wa Kata ya Mwakijembe, Letinga Matagi.
NA. JIMMY KIANGO-AFRINEWS SWAHILI-TANGA
WAKAZI wa vijiji vya Perani na Mbuta vilivyopo katika Kata ya Mwakijembe, wilayani Mkinga mkoani Tanga wamelipongeza Shirika la Kimataifa la WWF kwa kuwa mshirika mkuu wa kuumaliza mgogoro wa muda mrefu wa mpaka.
Kabla ya WWF kubeba jukumu la kuumaliza mgogoro huo kwa njia ya kukutanisha pande zote kwa kushirikiana Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, hali haikuwa nzuri kwa wakazi wa vijiji hivyo, ambapo walifikia hatua ya kila upande kutaka kumiliki eneo zaidi hali iliyokuwa ikiibua migogoro ya mara kwa mara.
Awali Kijiji cha Perani kilikuwa ni sehemu ya Kijiji cha Mbuta, ongezeko la watu na makazi lilisababisha kukigawa Kijiji hicho, hata hivyo ugawaji huo haukuzingatia urasimishaji wa mipaka.
Akizungumza na Afrinews Swahili, Diwani wa Kata ya Mwakijembe, Letinga Matagi alisema mpaka huo wa Maili nane ulikuwa ni kero kwa wananchi wa vijiji hivyo, kwani kila Kijiji kilitaka kujimilikisha ardhi zaidi hali iliyokuwa inasababisha uvamizi wa ardhi usio na sababu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbuta, Emmanuel Simba.
“Halikuwa jambo lenye afya kwa kata yangu, kukosekana kwa mpaka rasmi kulitusumbua sana, wana kijiji walikuwa wanaingia kwenye mgogoro wa mara kwa mara kwa sababu ya kila mmoja kuona ana haki na eneo jengine.
“Jambo la kushukuru ni ujio wa wenzetu wa WWF wametuwekea mambo sawa, kwa sasa hakuna mtu ataweza kuvuka mpaka wa Kijiji chake na kuvamia kwa mwenzake, hii ni hatua kubwa na nikiri wote tumeifurahia.
“Kutatuliwa kwa mgogoro huu kutawafanya wanakijiji wa vijiji vyote viwili kurejesha amani na umoja wao, hawata gombania tena mipaka badala yake watajielekeza kwenye kujiletea maendeleo, hawa ni ndugu maana awali walikuwa ni Kijiji kimoja, nimefurahishwa nah atua hii kwakweli,”alisema Matagi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbuta, Emmanuel Simba maarufu kama Mapambano, nae alizielekeza shukurani zake kwa WWF kwa kufanikisha kumaliza mgogoro huo uliokuwa ukikwamisha shughuli za maendeleo.
“WWF wamekuwa marafiki wakubwa wa wananchi, kwakweli kitendo chao cha kuumaliza mgogoro huu, kinaashiria kutufungulia milango ya kujiletea maendeleo badala ya kujielekeza kwenye migogoro zaidi.”
Mtendaji wa Kijiji cha Mbuta, Bi. Aisha Katuma aliyesimama akiongea na wanakijiji wa kijiji cha Mbuta.
Mtendaji wa Kijiji cha Mbuta, Aisha Katuma, alisema anaamini hatua hiyo ya kumaliza mgogoro wa mpaka ina faida kubwa na utawaunganisha zaidi wanakijiji wa vijiji hivyo.
Kwa upande wake Sadega Oleisai mkazi wa Kijiji cha Mbuta, aliishukuru WWF kwa kuwamalizia mgogoro huo ambao ulikuwa ukiwasababishia kutoelewana wenyewe kwa wenyewe.
“Hii ni hatua nzuri kwetu, tumeondokana na mgogoro wa mpaka sasa, ushirikiano wetu utarejea kama ilivyokuwa awali, haikuwa na maana yeyote kwa sisi kugombani mipaka, sasa tunajua sisi wa Perani tunaishia wapi na wenzetu wa Mbuta wanaishia wapi, hii ni hatua kubwa sana, tunaishukuru WWF kwa kutumalizia kero hii.
“Lakini pia tunamshukuru Diwani wetu (Matagi) amekuwa mstari wa mbele kutupigania, pamoja na kwamba anatoja katika jamii ya wafugaji, lakini hana ubaguzi, anatenda haki kwa wote.”
Akizungumzia suala hilo mmoja wa maofisa wa WWF ambae ni msimamizi wa Mradi wa Uongoaji wa Misitu ya Usambara Mashariki pamoja na Uandaaji wa mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi kwa vijiji vitano vya Wilaya ya Mkinga, Thomas Sawe, alisema mpaka huo ulikuwepo, lakini haukuwa rasmi.
“Mpaka ulikuwepo, lakini haukuwa rasmi, hakukuwa na alama zinazoonesha Kijiji hiki kinaishia hapa na hiki kinaanzia hapa, tulipofika kijijini katika kutekeleza mradi wa upangaji wa matumizi bora ya ardhi, tukakutana na changamoto hiyo.
“Kwakuwa lengo letu ni kuhakikisha ardhi haiwi sehemu ya maafa kwa binadamu na wanyama badala yake inakuwa faida, tukaamua kushughulika na mgogoro huo kwa kukutanisha pande zote mbili, haikuwa rahisi hasa kwa wafugaji, lakini tunamshukuru Diwani alisaidia sana, hakuwa upande wa wafugaji wala wakulima, badala yake alisimama kwenye usawa. “Jambo la kushukuru pande zote ziliafikiana na kwa pamoja na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mkinga tukapanda alama za kuonesha mpaka wa Kijiji, hii ni hatua kubwa kwetu na tunajivunia hili, yako mengi tumeyafanya na tutaendelea kuyafanya kupitia mradi huu na jambo kubwa ni ushirikiano tunaoupata kutoka kwa wanakijiji wenyewe, serikali ya Kijiji, serikali ya wilaya na hata ya mkoa,” alisema Sawe.
0 Comments