Afisa Wanyamapori wa Kitengo cha Upelelezi kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Tryphone Kanon |
Na Sidi Mgumia, Bagamoyo
Uchache wa rasilimali
fedha na askari wa wanyama pori katika hifadhi nchini unatajwa kuwa ni miongoni
mwa changamoto kubwa wanazokabiliana nazo wahifadhi katika kudhibiti ujangili
nchini.
Hayo yamesemwa jana Julai
19,2023 na Afisa Wanyamapori wa Kitengo cha Upelelezi kutoka Mamlaka ya
Wanyamapori Tanzania (TAWA), Tryphone Kanon alipokuwa akiwasilisha mada juu ya
masuala ya wanyamapori katika semina ya wahariri iliyofanyika Bagamoyo, mkoani
Pwani.
Semina hiyo ya siku mbili (Julai 19 na 20, 2023) imeandaliwa
na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikiana
na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia mradi wake wa Tuhifadhi Maliasili.
Washiriki wa semina wakiwa katika picha ya pamoja |
“Tuna askari wachache sana
na inawawia vigumu kuangalia maeneo yote kwa wakati muafaka, hii ni changamoto
sana hasa katika suala zima la kukabiliana na ujangili nchini,” alisisitiza
Kanon
Pamoja na hilo, Kanon
alisema kuwa ongezeko la migogoro ya binadamu na wanyama pia bado ni tatizo
ambapo wanyama wanawavamia wananchi na wananchi kuwavamia wanyama jambo ambalo
imeilazimu TAWA kujenga vituo vingi vya kudhibiti wanyama waharibifu kitu
ambacho kinawafanya washindwe kugawa askari wao kwenda kuwadhibiti.
Aliongeza kuwa, “Ujenzi wa
makazi na kuwepo kwa shughuli za kibinadamu katika mapito ya wanyamapori
(shoroba) kumeendelea kuwa changamoto katika suala zima la kudhibiti ujangili
kwasababu wanyama wanaposhindwa kupita kutoka eneo moja na kwenda jingine, TAWA
wanalazimika kuwarudisha walikotoka jambo ambalo linawagharimu rasilimali
nyingi kama watu, magari, mafuta na nyingine ambazo kama isingekuwa kuzuiwa kwa
wanyama basi rasilimali hizo zingetumika kukabiliana na ujangili.”
Kwa upande mwingine
amevitaja viumbe vamizi pia kuwa bado ni changamoto ambayo inaharibu na kuleta shida
kubwa kwa wanyamapori haswa majani ambayo yamekuwa yakiota maeneo ya hifadhi
ambayo sio rafiki kwa wanyama kwasababu ni majani ambayo hayaliki.
Pamoja na changamoto hizo, Kanon amesema TAWA bado wanaendelea kushirikiana na wadau wengine wa mazingira katika kuzikabili changamoto zilizopo na ni kwa lengo ya kuhakisha wanapambana na ujangili nchini.
Meneja Ufuatiliaji na Tathmini wa Mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) wa Tuhifadhi Maliasili, John Noronha akifafanua jambo kwa wahariri wakati wa semina |
Akizungumzia juu ya changamoto ya migogoro kati ya wanyama na binadamu, Meneja Ufuatiliaji na Tathmini wa Mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) wa Tuhifadhi Maliasili, John Noronha alisema bado wanaendelea kutoa elimu kwa watanzania juu ya umuhimu wa wanyamapori, namna bora ya kuvumilia kuishi nao pia kukabiliana na migongano hiyo.
“Tumeendelea kuwaelimisha watanzania
kuanzia shuleni na hii ni muhimu sana kwasababu tangu wakiwa wadogo wanaanza
kufahamu wanyama jambao ambalo linawasaidia sana kubadilisha namna
wanavyofikiri, inawaongezea viwango vya uvumilivu haswa katika suala zima la
kuishi na wanyamapori karibu na kuelewa ni hatua gani za kuchukua katika
kuitatua hiyo migogoro kati yao,” alisisitiza Noronha
Akizungumzia
lengo la semina hiyo, Mjumbe wa Bodi ya Chama cha Waandishi wa Habari za
Mazingira Tanzania (JET), Bakari Kimwanga amesema kuwa mafunzo hayo ambayo ni
sehemu ya mradi wa Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na USAID na kutekelezwa na
JET ni kuwajumuisha
wahariri katika mapambano dhidi ya ujangili na uharibifu wa mazingira lakini
pia mahususi kwa kuendelea kuwasisitiza wahariri
juu ya suala zima la umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori na amzingira kwa ujumla
wake.
Mjumbe wa Bodi ya Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), Bakari Kimwanga
“Kama JET tunawashukuru
wahariri kama wakuu wa vyombo vya habari kwa kazi kubwa wanayoifanya katika
kuchakata habari na kuelimisha umma lakini pia tunawasisitiza kuendelea kuzipa
kipaumbele habari za uhifadhi wa wanyamapori na mazinginra kwa ujumla wake,”
alisema Kimwanga
0 Comments