Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah Kairuki amesema wanafunzi 129,830 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2022 kutoka Tanzania Bara wakiwemo Wasichana 66,343 na Wavulana 63,487 sawa na 69% ya wenye sifa, wamechaguliwa kujiunga na Shule za Sekondari za Kidato cha Tano mwaka huu.
Akitoa taarifa hiyo leo Jijini Dodoma, Waziri Kairuki amesema “Wanafunzi 1,878 wakiwemo Wasichana 1,097 na Wavulana 781 wamepangiwa katika Shule za Sekondari Maalum nane za Kilakala, Mzumbe, Ilboru, Kisimiri, Msalato, Kibaha, Tabora Boys na Tabora Girls”
“Wanafunzi 122,908 wakiwemo Wasichana 62,731 na Wavulana 60,177 wamepangiwa katika Shule 519 za Sekondari za Bweni za Kitaifa za Kidato cha Tano na Wanafunzi 5,044 wakiwemo Wasichana 2,515 na Wavulana 2,529 wamepangwa katika Shule 11 za Sekondari za kutwa za Kidato cha Tano”
“Muhula wa kwanza kwa Wanafunzi wa kidato cha tano utaanza Agosti 14, 2023, hivyo wanafunzi wote waliopangwa kujiunga na kidato cha tano kwa mwaka, 2023 wanapaswa kuanza kuripoti Shuleni kuanzia Agosti 13, 2023, siku ya mwisho ya kuripoti itakuwa Agosti 31, 2023”
“Orodha ya Wanafunzi wote 188,128 waliokidhi vigezo Tanzania Bara na 129,830 kuchaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano huku wengine wakipangiwa vyuo vya Ualimu na vyuo vya Elimu ya Ufundi mwaka, 2023 inapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI ya selform. tamisemi.go.tz na Baraza la Taifa la Elimu ya Mafunzo ya Ufundi ya nacte.go.tz”
0 Comments