MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesisitiza kuwa hadi kufikia Desemba 31, mwaka huu kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea atatakiwa kuwa na Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi (TIN) bila kujali anayo biashara au la.
Hayo yameelezwa leo Juni 6, 2023 jijini Dar es Salaam na Afisa Mkuu wa Usimamizi wa Kodi nchini kutoka TRA, Hemed Mteri, katika semina iliyohusu masuala ya Kodi, kwa wanachama wa klabu ya waandishi wa Habari Dar es Salaam(DCPC) katika ukumbi wa Chuo cha Kodi ambapo amesema kukosa TIN itakuwa ni kosa la jinai.
“Kila Mtanzania aliyefikisha miaka 18 kuendelea anapaswa kuwa na namba ya utambulisho wa mlipakodi(TIN) bila kujali anayo biashara ama la hadi ifikapo Desemba 31, mwaka huu.
“Kila Mtanzania aliyefikisha umri wa miaka 18 anapaswa kuwa na TIN kutokuwa nayo litakuwa ni kosa la jinai. TRA tumeendelea kutoa elimu kwa wadau wa taaluma mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara na wengineo na kuendesha kampeni za ulipaji wa Kodi kwa wakati,” amesema Mteri.
Aidha, katika hatu nyingine mamlaka hiyo bainisha kuwa ina matarajio ya kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato kupitia mfumo wa utoaji huduma ya kidigitali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo imejiwekea malengo ya kukusanya mapato ya Sh Trilioni 23.1 kufikia mwishoni mwa waka wa fedha wa 2022/2023.
Awali akizungumza katika semina hiyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo, amesema mfumo huo umesaidia kukata mizizi ya vishoka, kupunguza gharama za usafiri kwa walipa kodi za kufika katika ofisi za TRA, mwamko mkubwa sababu ilikuwa ni kilio cha wananchi.
“Kupitia mfumo wa kidigitali matumaini ni kufikia malengo ambayo Kwa msaada wenu wanahabari na walipa Kodi na tunategemea ifikapo Juni 30, mwaka huu kutakuwa na habari njema,” amesema Kayombo.
Amesema wamefanikiwa kusogeza huduma kwa kufungua ofisi za TRA katika maeneo mbalimbali nchini, kuendelea kutoa elimu ulipaji Kodi kwa makundi mbalimbali.
0 Comments