Ticker

7/recent/ticker-posts

BUNGE LARIDHIA MKATABA WA MABORESHO YA BANDARI

Bunge la Jamhuri ya Muungano limepitisha azimio la Bunge la mwaka 2023 kuhusu mapendekezo ya kuridhia makubaliano kati ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai juu ya ushirikiano wa kiuchumj na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari Tanzania.

Azimio hilo liliwasilishwa Bungeni na Waziri wa ujenzi na Uchukuzi, Makame Mbarawa leo Juni 10,2023 bungeni jijini Dodoma.

Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson aliwahoji wabunge juu ya azamio hilo na wengi walionesha kuliridhia na hivyo kushinda.

AZIMIO KAMILI

AZIMIO LA BUNGE KUHUSU MAPENDEKEZO YA KURIDHIA MAKUBALIANO KATI YA SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA SERIKALI YA DUBAI KUHUSU USHIRIKIANO WA KIUCHUMI NA KIJAMII KWA AJILI YA UENDELEZAJI NA UBORESHAJI WA UTENDAJI KAZI WA BANDARI TANZANIA LA MWAKA 2023  _____________________________

KWA KUWA, dhima ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuboresha Sekta ya Bandari nchini ili kuongeza ufanisi na mchango wa Sekta hiyo katika mapato ya nchi, ajira na kuchagiza ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi, ilionekana upo umuhimu wa kuendelea kushirikisha sekta binafsi katika shughuli za bandari nchini;

NA KWA KUWA, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) tayari ilishashirikisha sekta binafsi katika uendeshaji wa shughuli za bandari ambao ulikuwa na tija, Serikali imeona ni vema kuendelea kutafuta wawekezaji wapya wenye uwezo wa kuongeza tija na ufanisi wa bandari zetu ili ziendelee kushindana kikanda katika uhudumiaji wa shehena na kuongeza mchango katika mapato ya Serikali na maendeleo ya wananchi kwa ujumla;

NA KWA KUWA, kwa vipindi tofauti, TPA ilipokea na kuchambua mapendekezo ya wawekezaji mbalimbali walioonesha nia ya kuwekeza katika maeneo ya Bandari nchini iliamua kuingia Makubaliano ya Awali (Memorandum of Understanding - MOU) na Kampuni ya DP World (DPW) inayomilikiwa na Serikali ya Dubai mnamo tarehe 28 Februari, 2022 baada ya kudhihirika kwa tija iliyoipata Serikali ya Dubai kupitia Kampuni hiyo ya DP World na kupelekea huduma za uchukuzi kupitia bandari kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Serikali ya Dubai (Dubai GDP);


NA KWA KUWA, makubaliano hayo yalikuwa na lengo la kubainisha maeneo mahsusi ya ushirikiano ili kuboresha uendeshaji wa maeneo ya bandari nchini, kuwekeza katika maeneo yaliyotengwa katika Bandari Kavu; utunzaji wa mizigo (logistics parks) na maeneo ya kanda za kibiashara (trade corridors);

NA KWA KUWA, Serikali iliona tija ya kuishirikisha kampuni ya DP World inayomilikwa na Serikali ya Dubai kwa asilimia 100, ilianzisha majadiliano na Serikali ya Dubai na kufanikisha kuandaliwa na kuingiwa kwa Mkataba baina ya Nchi na Nchi (Intergovernmental Agreement) wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii kwa ajili ya Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji kazi wa maeneo ya Bandari nchini na ambao ulisainiwa na pande zote tarehe 25 Oktoba 2022;

NA KWA KUWA, kampuni ya DP World ina uzoefu mkubwa katika uendeshaji wa shughuli za bandari barani Afrika, Asia, Ulaya na Amerika ya Kaskazini na Kusini. Kampuni hii pia ina uzoefu na utaalamu wa kuchagiza mnyororo mzima wa usafirishaji (end to end total logistics chain solution) kutoka maeneo ambayo bidhaa zinatoka mpaka kufika kwa Walaji.

NA KWA KUWA, Kampuni hiyo ina uwezo wa Uendeshaji wa maeneo maalum ya kiuchumi (special economic zones) karibu na bandari, pamoja na usafirishaji baharini na nchi kavu (kupitia njia ya reli), uwekezaji katika mitambo na mifumo ya kisasa ya uendeshaji wa shughuli za kibandari. Pia, ina uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya bandari zikiwemo: kuwekeza katika mitambo na mifumo ya kisasa ya uendeshaji wa shughuli za kibandari na hivyo kuleta ufanisi; kuwekeza katika mnyororo wa usafirishaji ili kuongeza ufanisi wa bandari; kuwekeza katika vichocheo vya shughuli za kibandari zikiwemo maeneo huru ya viwanda, maeneo ya kuhifadhi shehena nje ya bandari; miundombinu unganishi ya usafirishaji; kuwekeza katika miundombinu wezeshi katika usafirishaji wa bidhaa zinazoharibika (perishables); na kuwekeza katika kutafuta masoko kutoka katika nchi zisizo na bandari na kuziunganisha na bandari;

NA KWA KUWA, lengo la Mkataba huu ni kuweka msingi wa kuanzisha majadiliano baina ya Serikali na mwekezaji ili kuwezesha kukubaliana maeneo mahususi ya ushirikiano na kuingia mikataba ya nchi mwenyeji ambayo baada ya kusainiwa, itawezesha TPA kuanza majadiliano na mwekezaji katika maeneo mahususi yatakayokuwa yamekubaliwa katika mikataba ya nchi mwenyeji;

NA KWA KUWA, Mkataba unaolengwa kuridhiwa unabainisha vipengele muhimu ikiwa ni pamoja na:-

i. Ibara ya 2 - Malengo ya Mkataba: Ibara hii inaelezea kuwa, lengo la Mkataba huo ni kuweka utaratibu wa kisheria wa maeneo ya mashirikiano kwa ajili ya kuendeleza, kuboresha na kuendesha Bandari za Bahari na Maziwa, miundombinu inayoendana na shughuli za bandari kama itavyopendekezwa na Serikali kupitia TPA kwa kuzingatia ulinzi na maslahi mapana ya Taifa. Pia maeneo ya mashirikiano yanajumuisha kujenga uwezo, kuhamisha ujuzi, teknolojia na utaalam, kuimarisha vyuo vya mafunzo na intelijensia za masoko.

ii. Ibara ya 3 - Ushirikiano: Ibara hii inaeleza kuwa, nchi zitashirikiana kwa lengo la kuanzisha na kuendeleza mazingira muhimu na bora kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za uwekezaji unaolengwa na kuwa wawakilishi wa nchi zetu watakutana kwa lengo la kujadili na kuingia mikataba kwa namna itakavyoonekana inafaa ili kuwezesha kuanza utekelezaji wa miradi inayokusudiwa. Ibara hii pia inaanzisha Kamati ya Ushauri ambayo ina jukumu la kuratibu shughuli za utekelezaji wa Mkataba husika na kuhakikisha kunakuwepo na utaratibu wa kubadilishana taarifa kuhusu malengo ya uwekezaji unaokusudiwa.

iii. Ibara ya 4 - Mawanda ya Ushirikiano na Taasisi za Utekelezaji: Ibara hii inafafanua kuwa, mawanda ya Mkataba huo ni kuwezesha utekelezaji wa ushirikiano kama ilivyoainishwa katika Kiambatisho cha kwanza cha Mkataba. Kiambatisho hicho, kimeainisha maeneo ya ushirikiano yatakayotekelezwa kwa awamu mbili. Serikali ya Tanzania inasisitiza kuwa TPA ndio yenye jukumu la kutekeleza maeneo ya ushirikiano kuhusu Mkataba huo na kwa upande wa Serikali ya Dubai, DP World na washirika wake ndio zitakuwa Taasisi za utekelezaji. Pamoja na ushirikiano huo, nchi yetu itakuwa na haki ya kuitaarifu Serikali ya Dubai kuhusu fursa nyingine za uwekezaji katika maeneo ya bandari, maeneo huru ili kuwezesha Taasisi za Dubai kuwasilisha mapendekezo ya uwekezaji katika maeneo hayo. Kuhusu uwekezaji husika, DP World na washirika wake ndio watakuwa na jukumu la kutafuta fedha kwa ajili ya uendelezaji wa shughuli za uwekezaji.

iv. Ibara ya 5 - Haki za Kuendeleza, Kusimamia na Kuendesha: Ibara hii inaeleza kuwa, DP World itapewa jukumu la kuendeleza, kusimamia na kuendesha maeneo ya kipaumbele ya uwekezaji (priority projects) kama itakavyokubaliwa kupitia mikataba mahususi ya nchi mwenyeji. Jukumu hili ni kwa kipindi mahususi cha miezi kumi na mbili (12) kuanzia tarehe ya kusainiwa kwa mkataba huu, 25 Oktoba 2022 na baada ya kuisha kipindi hicho TPA itakuwa na haki ya kuwasikiliza wawekezaji wengine katika maeneo ya uwekezaji ya kipaumbele.

v. Ibara ya 8 - Haki ya Ardhi: Ibara hii inaitaka Serikali ya Tanzania kuhakikisha hatua muhimu zinachukuliwa ili kuwezesha DP World kupata haki ya matumizi ya ardhi na sio umiliki kwa lengo la utekelezaji wa miradi itakayokubali kupitia mikataba ya Nchi Mwenyeji. Serikali italinda haki za usalama wa umiliki ardhi na kubaki katika mikono ya Watanzania kwa kuzingatia Sheria na taratibu za nchi za kutoa na kutumia Ardhi kwa wawekezaji na kuhakikisha haki hizo zinabaki hai katika kipindi cha utekelezaji wa mradi tuu. Aidha, katika kutekeleza haki za ardhi, Serikali itahakikisha haki hizo zinatambulika, zinasajiliwa, hazina madai yoyote na zinatolewa kwa kampuni itakayotekeleza mradi kwa kuzingatia taratibu na sheria za nchi kwa kipindi cha upangishaji au utekelezaji wa mradi.

vi. Ibara ya 9 - Motisha za Uwekezaji: Ibara hii inaeleza kuwa, uwekezaji wa DP World utakuwa mkubwa na utaleta manufaa ya kiuchumi na kijamii hivyo utahitaji kutolewa motisha za uwekezaji. Hivyo, pande mbili zilikubaliana kutoa motisha za uwekezaji kwa kuzingatia Sheria za nchi na taratibu mahsusi za Tanzania kama itakavyoainishwa zaidi katika Mikataba ya nchi mwenyeji.

vii. Ibara ya 12 – Ulinzi na Usalama: Ibara hii inaeleza kuwa utekelezaji wa shughuli za miradi hautaathiri au kukiuka masuala ya ulinzi na usalama ikiwemo: Ardhi ya Mradi, mifumo, miundombinu ya juu na chini ya eneo la bandari, mitambo iliyosimikwa pamoja na masuala mengine ya usalama ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama yatakavyokubaliwa chini ya Mkataba wa Nchi Mwenyeji.

viii. Ibara ya 13 - Ushirikishaji wa Wazawa, Ajira na Majukumu kwa Jamii: Ibara hii inaeleza kuwa, mikataba itakayosainiwa ya utekelezaji wa mradi ni lazima iainishe: mpango wa ushirikishaji wa wazawa katika utekelezaji wa mradi husika; majukumu kwa jamii; undelezaji wa ajira zilizopo; kutoa ajira mpya kwa watanzania na kuwapatia mafunzo kuhusiana na utekelezaji wa miradi husika.

ix. Ibara ya 18 – Kodi, Tozo na Ushuru Nyinginezo: Ibara hii inaeleza kuwa kodi, ushuru na tozo nyinginezo zitakusanywa katika utekelezaji wa mradi kwa kuzingatia Sheria za Kodi zilizopo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia, Ibara hii inaeleza kuwa Motisha za Uwekezaji, misamaha ya kodi ama tozo nyinginezo zitatolewa kwa kuzingatia msingi wa sheria za kodi zilizopo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kama itakavyokubaliwa katika Mkataba wa Nchi Mwenyeji na Mikataba ya Utekelezaji wa Miradi kwa kuzingatia Sheria za Nchi.

x. Ibara ya 19 – Kurithiwa kwa Nchi: Ibara hii inaeleza kuwa, iwapo nchi itabadilika ama kuungana na nchi nyingine au zingine, nchi ambayo itarithi majukumu, itachukuliwa kuwa sehemu ya Mkataba huu kutoka tarehe ya kurithiwa kwa nchi husika, kwa kuzingatia kuwa, nchi inayorithi majukumu itatoa taarifa kwa upande mwingine kuhusu nia yake ya kuwa sehemu ya Mkataba huu.

xi. Ibara ya 20 - Utatuzi wa Migogoro: Ibara hii inaeleza kuwa, utaratibu wa utatuzi wa migogoro uliopendekezwa chini ya Mkataba huu ni kuanza kwa kutatua kwa Makubaliano “Amicable Settlement” kupitia njia za kidiplomasia au kupitia Kamati ya Ushauri ya IGA na kama mgogoro hautatatuliwa ndani ya siku 90 upande usioridhishwa unaweza kutangaza kuwepo kwa mgogoro “Declared Dispute”. Pale ambapo kunakuwa na mgogoro “Declared Dispute” utaratibu wa usuluhishi ni kupitia Baraza la Usuluhishi chini ya Kanuni za Usuluhishi za UNCITRAL. Sehemu iliyokubaliwa kuwa mgogoro utasikilizwa ni Johannesburg, Afrika Kusini na lugha ya usuluhishi ni Kiingereza.

xii. Ibara ya 21 - Sheria Zinayosimamia Mkataba: Ibara hii imeweka msisitizo kuwa, Sheria itakayosimamia Mkataba wa Nchi Mwenyeji Mikataba ya utekelezaji wa miradi zitakuwa Sheria za Tanzania.

xiii. Ibara ya 22 - Marekebisho ya Mkataba: Ibara hii inafafanua kuwa, Mkataba huu unaweza kurekebishwa muda wowote kwa upande mmoja kuwasilisha nia ya kurekebisha masharti ya mkataba kwa upande mwingine kwa njia ya maandishi na kukubaliwa kwa marekebisho hayo kwa pande zote.

xiv. Ibara ya 23 - Muda wa Mkataba na Usitishwaji: Ibara hii inaeleza kuwa, Mkataba utakuwa hai mpaka itakapotokea moja ya masuala mawili; usitishwaji wa shughuli za uwekezaji au kumalizika wa muda wa Mkataba wa Nchi Mwenyeji (Host Government Agreement). Pale ambapo moja ya Mkataba wa Nchi Mwenyeji itasitishwa kabla ya

kipindi chake kumalizika, Mkataba wa IGA utaendelea kuwa hai. Aidha, haki na wajibu wa pande mbili za mkataba zitaamuliwa kwa mujibu wa Mkataba husika.

xv. Ibara ya 25 - Kuanza Kutumika kwa Mkataba: Ibara hii inaeleza kuwa, mara baada ya kusainiwa kwa Mkataba huo pasipo kujali majukumu mengine, pande mbili za Mkataba zitachukua hatua stahiki kuhakikisha shughuli za awali za Miradi zinaanza kutekelezwa kwa mujibu wa Sheria za nchi. Pia, ndani ya siku 30 kutoka tarehe ya kusainiwa kwa Mkataba, Nchi Washirika zitaanzisha mchakato wa kuridhiwa na Mamlaka husika ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya nchi katika Mkataba kwa mujibu wa Sheria za Kimataifa. Pia, Mkataba huu utaanza kutekelezwa baada ya kubadilishana kwa Hati za Uridhiaji kwa mujibu wa Sheria za nchi husika.

xvi. Ibara ya 30 - Mazingira ya Kisheria Kutobadilika: Ibara hii inaeleza kuwa, mfumo wa sheria na mazingira yake kuhusu Mradi yatakuwa tulivu (stable) katika hali ambayo inaridhisha kwa pande zote. Utulivu huo utaanza tarehe ya kusainiwa kwa IGA. Pia, katika Ibara hii Tanzania imetakiwa kuchukua hatua stahiki ili kuwezesha makubaliano yatakayowekwa katika Mikataba ya Mradi au Mkataba wa Nchi Mwenyeji.

xvii. Ibara ya 31 - Kubadilisha Hati za Uridhiaji: Ibara hii inaeleza kuwa, Mkataba huo na Hati za Uridhiaji zitabadilishwa baina ya pande mbili za Mkataba.

NA KWA KUWA, Mkataba huu una manufaa mbalimbali ambayo ni pamoja na:

(i) Kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 5 kwa sasa mpaka masaa 24. Hii itapunguza gharama za utumiaji wa Bandari yetu. Matokeo yake itaongeza idadi ya meli zitazokuja Bandari ya Dar es Salaam kutoka meli 1,569 zilizohudumiwa mwaka 2021/22 mpaka kufikia takriban meli 2,950 ifikapo mwaka 2032/33;

(ii) Kupunguza muda wa ushushaji wa makontena kutoka siku 4.5 mpaka siku 2;

(iii) Kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka masaa 12 mpaka saa 1 kutokana na uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA;

(iv) Kupunguza gharama ya usafirishaji wa shehena kutoka nchi za nje kwenda nchi za jirani, kwa mfano kutoka US$ 12,000 mpaka kati ya US$6,000 na US$7,000 kwa kasha linalokwenda nchi ya Malawi, Zambia au DRC. Hii italeta Watumiaji wengi kwenye Bandari ya Dar es Salaam;

(v) Kuongezeka kwa shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni 18.41 za mwaka 2021/22 hadi kufikia tani 47.57 mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 158;

(vi) Kuongezeka kwa Mapato ya Serikali yatokanayo na Kodi ya Forodha inayokusanywa katika shehena inayopitishwa bandarini kutoka Shilingi Trilioni 7.76 za mwaka 2021/22 hadi Shilingi Trilioni 26.70 za mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 244;

(vii) Kuongezeka kwa ajira zinazotokana na shughuli za bandari kutoka 28,990 mwaka 2021/22 hadi 71,907 ifikapo mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 148;

(viii) Maboresho ya magati ya kuhudumia Majahazi na Abiria ikiwa ni pamoja na kushawishi uingiaji wa meli kubwa za kitalii zitakazo ongeza idadi ya watalii nchini na kuongeza pato la Taifa;

(ix) Mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa TPA katika Bandari zote (knowledge and skills transfer);

(x) Uanzishaji wa maeneo huru ya kiuchumi na kuchochea ukuaji wa sekta zingine za kiuchumi zikiwemo: Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Utalii; Viwanda na Biashara; na

(xi) kuchagiza ukuaji wa sekta ndogo za usafirishaji kwa njia ya reli (SGR, TAZARA na MGR) na barabara; na kujenga mahusiano ya kidiplomasia.

HIVYO BASI, kwa kuzingatia manufaa ambayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itayapata kutokana na Mkataba huu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wake wa 11 na kwa mujibu wa Ibara ya 63(3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, linaazimia kuridhia Makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai Kuhusu Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii kwa ajili ya Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji Kazi katika Bandari Tanzania (The Intergovernmental Agreement Between the United Republic of Tanzania and the Emirate of Dubai Concerning Economic and Social Partnership for the Development and Improving Performance of Sea and Lake Ports in Tanzania). Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja.

10 Juni,2023

M.M.M WUU

_____________

Post a Comment

0 Comments