Dkt. Numan (mwenye fulana ya bluu) akiwa pamoja na washiriki wa semina iliyoandaliwa na WWF.
Ogezeko la watu na shughuli za kibinadamu zinatajwa kuwa kichocheo kikuu cha kuyaharibu mapito 58 ya wanyama (ushoroba) nchini.Kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika mwaka 2019, zimeonesha kuwa shoroba 30 zinazotambulika na 28 ambazo hazijatambulika rasmi,pamoja na wanyama kuzitumia, hali yake si nzuri.
Dkt. Numan Amanzi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) amelieleza hili wiki iliyopita mkoani Morogoro kwenye semina iliyoendeshwa na Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori Duniani (WWF) na kushirikisha
wadau wa mazingira nchini.
Dkt. Numan alisema shughuli za ujenzi wa makazi, kilimo na shughuli nyingine za kibinadamu zimekuwa zikiathiri na kuhatarisha uendelevu na uhai wa mapito ua nyama.
Alisema kuharibu shoroba hizo kutafanya baadhi ya wanyama kutoweka kwenye baadhi ya maeneo kwani watashindwa kuhama hama kama maisha yao yanavyotaka na kujikuta wakisalia kwenye eneo moja hatua ambayo inaweza kutishia uhai wao.
“Shoroba zote nchini zimeingiliwa na shughuli za kibinadamu kama vile ujenzi ama kilimo, lakini zipo zenye nafuu, ingawa nazo zinaweza kuharibiwa maana kasi ya ufanyaji wa shughuli za binadamu ni kubwa,” alisema.
Aliitaja shoroba ya Loazi – Kalambo kuwa na hali mbaya zaidi, huku shoroba za Burigi-Moyowosi/Kigosi, Gombe-Kwitanga, Greater Gombe Eco Syestem- Masito Ugala, Igando-Igawa na Katavi Mahale angalau zina afadhali.
Akijibu swali kwanini Tembo ndio wanakuwa vinara wa kuvamia makazi ya watu,lililoulizwa na mmoja wa washiriki wa semina hiyo Jimmy Kiango, kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), Dkt. Numan alisema wanyama hao wanahitaji eneo kubwa zaidi la malisho yao, hali hiyo imekuwa ikiwafanya kurejea hata kwenye maeneo yao ya zamani.
“Tembo anahitaji eneo kubwa sana la kupata chakula chake na bahati mbaya huwa anatunza sana kumbukumbu, hali hiyo humfanya kurudi kwenye mapito yao ya kale hata kama ni mjukuu au kitukuu, huwa wanatabia ya kukumbuka mapito yao,”alisema.
Dkt. Numan alitoa wito kwa wadau wote wa mazingira nchini pamoja na wananchi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kulinda mapito ya wanyama.
Kwa upande wake afisa miradi wa WWF, Gladness Mtega, alisema wamejipanga kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kulinda mapito ya wanyama, misitu na mazingira kwa ujumla.
Mtega alisema pamoja na mambo mengine, wamefanikiwa kupanda miti 24,300 kwenye msitu wa asili wa Pugu Kazimzumbwi.
0 Comments