Mwanaharakati Cyprian Musiba
Kifo cha kachero na mwanasiasa nguli nchini Bernard Membe hakijaondoa Wala kufuta deni lake kwa mdai wake Cyprian Musiba.
Hili ni kwa mujibu wa Wakili Jonathan Mdeme, aliyekuwa akimwakilisha Membe (69) kwenye kesi dhidi ya Musiba.
Amesema deni la waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Nje kwa Musiba liko palepale na msimamizi wa mirathi ataendelea alipoishia.
Membe ambaye alikuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne, amefariki jana Ijumaa Mei 12, 2023 katika Hospitali ya Kairuki iliyopo Dar es Salaam wakati akipatiwa matibabu.
Itakumbukwa kuwa Oktoba 28, 2021, Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam ilimuamuru Musiba anayejitambulisha kama mwanaharakati huru kumlipa Membe fidia ya Sh6 bilioni.
Katika kesi hiyo namba 220 ya mwaka 2018, Membe alimdai Musiba fidia ya Sh10.3 bilioni kwa madai ya kumkashifu kupitia magazeti yake ya Tanzanite.
Wakili Mndeme amesema madai dhidi ya Musiba hayatafutika kwa sababu msimamizi wa mirathi ataendelea kufuatilia madeni ya marehemu.
“Katika makosa ya jinai, mtuhumiwa akifariki kesi inaisha hapo, katika makosa ya madai ni tofauti. Anateuliwa msimamizi wa mirathi ya marehemu halafu anavaa viatu vya marehemu kukusanya madeni na mapato kama yapo.
“Kama madeni yanalipwa, kama ni mapato yanagawanywa kwa mrithi halali kwa maana mke na watoto. Kwa hiyo kesi ya madai dhidi ya Musiba ni shauri la madai hivyo halitafutika kwa sababu msimamizi wa mirathi ataendeleza pale alipoishia,” amesema Mndeme.
Amesema kesi iko katika hatua ya kukazia hukumu au utekelezaji wa hukumu na maombi yaliwasilishwa mwaka 2022 na kupewa namba 26 ya mwaka 2022 na Mahakama Kuu Dar es Salaam.
Wakili huyo amesema alishateuliwa dalali kuendelea na kazi kukazia hukumu.
0 Comments